Jumapili, 31 Mei 2015

MLEZI ASASI YA NEW HOPE FOR GIRLS ANAOMBA MSAADA



MLEZI wa asasi ya kiraia inayohudumia wasichana wanaotoka katika mazingira magumu (New Hope for Girls organization), Consoler Wilbert, amewaomba wananchi kumchangia nauli ya kwenda kwenye matibabu nchini India baada ya hospitali hapa nchini kumpa rufaa akatibiwe huko.
Consoler ambaye amekuwa ni muhanga wa unyanyasaji wa watoto wa kike, alisema anasumbuliwa na maumivu ya kichwa na mgongo mara kwa mara yaliyotokana na kupigwa kwa masaa sita na walimu wake wakati akisoma sekondari ya Jitegemee iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya hedhi salama duniani jijini Dar es Salaam Consoler alisema alilazimishwa kuolewa akiwa na umri mdogo na alipokataa alikuwa anapigwa mara kwa mara shuleni na nyumbani.
“Siku moja nilipigwa sehemu mbali mbali za mwili hasa kichwani na mgongoni na walimu wanne huku wakiniambia nisali sala yangu ya mwisho kutoka saa nne asubuhi hadi saa 10 jioni.
“Nilikuwa nikiishi maisha ya kuomba omba mitaani ili nipate fedha kwa mahitaji ya shule nikiwa nimevaa sare za shule nikawa naitwa ‘malaya aliyejificha kwenye unifomu za shule’ iliniuma sana,”alisema Consoler.
Alisema baada ya kipigo hicho amekuwa na maumivu makali ya  kichwa na mgongo ambayo humfanya asiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kwani muda mwingi huutumia kwa kulala tu.
Anaomba kwa yeyote atakayeguswa na matatizo yake amsaidie kwa hali na mali ili akapate tiba na anayetaka kuwasiliana nae kwa namba za simu ambazo ni 0715025565 na 0787025565.
Alisisitiza kuwa  kwa sasa amewasamehe wote waliomfanyia anachohitaji ni kutibiwa ili arudi katika hali yake ya kawaida.
Aidha aliwataka wototo wa kike wasinyamaze wanapokutana na manyanyaso ya aina yoyote yale ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa majirani.
Kwa sasa asasi ya New Hope For Girls inawahudumia watoto wa kike 147 ambao wanatoka katika mazingira magumu na kati yao 24 wanaishi pamoja na mlezi huyo.
mwisho                                                 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni