WAKALA wa
Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Bodi ya mikopo ya elimu
ya juu(HESLB)wametoa onyo kali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakaofanya udanganyifu wa vyeti vya
kuzaliwa na vifo ili wapatiwe mkopo.
Onyo hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa
wa RITA, Emmy Hudson alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wametoa onyo hilo kutokana na kubainika kwa vyeti
kughushi takribani 500 vya kuzaliwa na vifo kwa waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa
mwaka wa masomo 2016/17.
Alisema vyeti
hivyo havikuwa katika kumbukumbu zao na hivyo walishindwa kuvitambua.
“Sheria ya
vizazi na vifo inamtia hatiani mtu yeyote ambaye atatoa taarifa za uongo hivyo
vyombo vya dola vitawashughulikia wanaofanya udanganyifu huu,” alisema Emmy.
Alisema kwa
kushirikiana na HESLB wameanzisha mfumo maalumu wa uhakiki kwa kutumia mtandao
ambapo mwombaji atatuma cheti cha kuzaliwa na vya vifo kutumia email na
vitahakikiwa.
“Waombaji
watatakiwa kuhakikiwa katika ofisi za wilaya zilizotoa vyeti hivyo na makao
makuu ya RITA na walioko mbali watumie barua pepe ya uhakiki@rita.go.tz wakiambatanisha vyeti na risiti za benki baada ya kulipia,” alisema
Emmy.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdulrazaq Badru alisema wanufaika wa mikopo
wanatakiwa kuwasilisha cheti cha kuzaliwa , vyeti vya masomo na vyeti vya vifo
kama alifiwa na wazazi wake.
“Nyaraka
hizi ni muhimu sana katika usajili wa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ili
kupata wanaostahili kunufaika,”alisema Badru.
mwisho