Alhamisi, 14 Mei 2015

JK AWACHANA WATENDAJI WA MANISPAA YA KINONDONI



RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Manispaa ya Kinondoni kubomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye mikondo ya kupitisha maji huku akiwataka wakazi wa mabondeni kuhama mara moja.
Akizungumza na wakazi wa Manispaa ya hiyo mara baada ya kukagua athari za mafuriko zilizotokea baada ya kunyesha kwa mvua, Rais Kikwete alisema kuwa, athari ya mvua ni kubwa kuliko watu wanavyofikiria.
Alisema, nyumba ambazo zimejengwa kwenye mikondo ya kupitisha maji zinapaswa kubomolewa ili kuruhusu yaweze kuelekea baharini, jambo ambalo linaweza kupunguza kutokea kwa mafuriko.
Alisema Manispaa inapaswa kuchukua hatua za dharura za kutatua matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kujenga mitaro inayoweza kupitisha maji kwa haraka ili kuondoa tatizo hilo.
“Ninawaagiza watendaji kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye mikondo inayosafirisha maji ambayo imechangia kuongezeka kwa mafuriko  katika maeneo mbalimbali.
“Mpango kama huo ulifanywa na wakazi wa Buruguni ambapo Manispaa ya Ilala ilibomoa nyumba 17 zilizojengwa kwenye maeneo  ya kupitisha maji , jambo ambalo lilichangia kupunguza ukubwa wa tatizo,”alisema Kikwete.
Alisema, tangu watatue tatizo hilo,hakuna nyumba iliyoingiliwa na maji  katika mvua zinazoendelea kunyesha.
Aliwashangaa mpaka sasa watendaji wa Manispaa hiyo wameshindwa kutumia maarifa ya kuondoa maji kwenye makazi ya watu hadi yamesababisha malalamiko.
 “Ninashangaa mpaka leo hamjafanya lolote huku wananchi wakikimbia nyumba zao, jambo ambalo limeongeza malalamiko, kutokana na hali hiyo, mnapaswa kutumia maarifa ili kutatua kero hii,”alisema.
Aliongeza, Manispaa Kinondoni ina bahati kwa sababu Mkurugenzi wake ni Mhandisi, lakini ameshindwa kutumia maarifa ya kuondoa maji kwenye nyumba za watu mpaka wananchi wamekimbia nyumba zao.
 “Wewe si Mhandisi? taaluma yako unaitumiaje! Umeshindwa hata kutafakari kidogo namna ya kutatua tatizo hili mpaka leo, haya nimewaletea maarifa yangu ingawa ni ya kizee lakini yatawasaidia kutatua tatizo,”alisema.
Alibainisha, Manispaa hiyo imepenga kutekeleza mpango wa muda mrefu ambao una gharama kubwa ya  utekelezaji wake bila ya kutafakari mpango wa dharura wa kutatua tatizo lililopo.
“Mmekuja na gharama kubwa za utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kutengeneza mitaro huku mkishindwa kutafakari mpango wa dharura wa kuondoa maji kwenye makazi ya watu, hilo ni tatizo,”alisema Kikwete.
Alisema Manispaa ina pampu 28 ambazo zinafanya kazi mpaka sasa lakini wameshindwa kuzipeleka kwenye maeneo hatarishi ambayo yaliyoathirika zaidi na tatizo hilo, badala yake wamesambaza moja moja mtaani huku maji yakishindwa kuondoka.
“Kitendo cha kusambaza pampu moja moja kwenye makazi ya watu hakujasaidia lolote, hata kama mlitaka kuwafurahisha watu lakini hawawezi kuwashukuru, hivyo basi mlipaswa kuzichukua zote mkazipeleka sehemu moja ili ziweze kunyonya kwa maji kwa haraka na kuhamishia sehemu nyingine,”alibainisha.
Akizungumza mara baada ya kukagua ofisi za Ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa) eneo la Tegeta ambazo zimezingilwa na maji, Rais Kikwete alisem akuwa mamlaka hiyo inapaswa kukaa na Wakala wa Barabara(TANROADS) na Manispaa ya Kinondoni ili kuangalia namna ya kuondoa maji yaliyojaa kwenye ofisi hizo.
Alisema ili maji yaweze kuondoka kwenye maeneoe hayo, lazima wajenge mifereji ya kupitisha maji ambayo yataelekea baharini moja kwa moja bila ya kuathiri makazi ya watu.
Hata hivyo, Kikwete aliwataka wakazi wote wa mabondeni na maeneo hatarishi kuhama sehemu hizo na kwenda kujiandikisha kwenye ofisi za Manispaa ili waweze kupewa viwanja.
Alisema maeneo ambayo tayari washalipwa hawezi kulipwa tena ila wale ambao hawajapewa maeneo na wako tayari kuhama serikali itawapa viwanja.
“ Kuna baadhi ya watu washalipwa lakini mpaka sasa bado wanaendelea kung’angania maeneo haya ambayo ni hatarishi kwa maisha, hakuna jawabu zaidi ya kuondoka tu, kwa sababu serikali haina uwezo wa kuzuia mvua,”alibainisha Kikwete.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manipaa  hiyo, Mhandisi Mussa Naty alisema kuwa Manispaa hiyo imepanga kutumia Sh bilioni 3.5 kwa ajili ya kujenga mitaro katika maeneo mbalimbali ya manispaa.
Alisema kiasi hicho ni kikubwa hivyo basi hawana uwezo wa kuzipata katika kipindi hiki zaidi ya kuiomba serikali kuu iwasaidie.
“Tutatumia pampu zetu kuondoa maji kwenye maeneo hatarishi ili wananchi waweze kurudi kwenye makazi yao, lakini pia kuna wengine ambao wamejenga kwenye maeneo ya kupitisha maji ambayo yamesababisha athari hii kuongezeka,’alisema Naty.
Alisema wakati wanajaribu kutatua tatizo la maji kutuhama katika eneo la Dawasa walimtafuta mkandarasi kutoka China ili aweze kutengeneza mitaro ya maji lakini walikwama baada ya kutaja gharama kubwa.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni