WAZAZI na walezi wa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi
katika chuo cha kimataifa cha Kampala(KIU), wamepanga kuandamana kwenda chuoni
hapo ili kupata ufafanuzi kuhusu madai ya watoto wao kuhusu usajili kamili wa
kozi ya famasia.
Wakizungumza kwa wakati tofauti na MTANZANIA wazazi hao
wamesema wameamua kujikusanya ili watambuane na kujua hatima ya watoto wao
kielimu.
Mmoja wa wazazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Hassan
Bumbuli alisema wametengeneza kundi kwenye mitandao ya simu inayowawezesha
kuwasiliana ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
“Sisi ndio tunalipa ada na ndio tunaojua ada tunapata wapi,
Chuo itabidi kitueleze ukweli ni lini watasajili kozi na si kutudanganya kama
wanavyowaambia wanafunzi kwani sisi si watoto wadogo,” alisema Bumbuli.
Alisema ilibidi wawaambie watoto wao waahirishe muhula
mpaka hapo kozi hizo zitakaposajiliwa lakini uongozi wa Chuo hicho unawakatalia
kitu ambacho kinawatia hofu.
Naye Mohamed Khasimu alisema chuo kimekuwa na gharama
zisizojulikana kama kulipia mitihani na gharama nyingine ambazo kipindi cha
mkataba hazikuwepo hivyo wataenda chuoni hapo kabla ya mitihani kuanza ili
kupata maelezo ya kina.
“Tutakutana na Uongozi wa Chuo watujibu madai ya watoto
wetu kama hatutoridhika basi tutajua nini cha kufanya,” alisema Khasimu.
Alisema wototo wao wamekuwa wakikaripiwa na kutishiwa
kufukuzwa chuo kila walipojaribu kuhoji usajili wa kozi.
Hivi karibuni wanafunzi wa kada ya famasia chuoni hapo waligoma
kuingia darasani kuushinikiza uongozi kutoa ufafanuzi kuhusu usajili wa kozi
wanazosoma pamoja na madai mengine sita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni