SHIRIKA lisilo la kiserikali la Women In Society(WoInSo) inatarajia kutambulisha programu maalumu itakayotoa
elimu kuhusu afya, maisha na mazingira ya malezi ya mtoto ndani ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa bodi ya shirika hilo, Juliana Madereke alisema
utambulisho huo utaambatana na sherehe za siku ya mtoto duniani zitakazofanyika
juni 6 mwaka huu Millennium tower ambapo Mkurugenzi wa Chama Cha
Uzazi na Malezi Bora Tanzania(UMATI), Lulu Ng’wanakilala anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi.
Madereke alisema elimu hiyo itawasaidia
watoto kujitambua pamoja na kuwashawishi wazazi kubadili tabia ambazo
zinamfanya mtoto asifikie malengo yake.
“Mtoto anafanyishwa kazi ambazo si sawa na
umri wake na jamii inaangalia tu bila kuhoji kwanini mzazi anafanya hivyo,”
alisema Madereke.
Alisema wameandaa filamu itakayogawiwa
bure nchi nzima iitwayo thamani yetu leo yenye maudhui ya ukatili wanaofanyiwa
watoto na wanajamii.
Alisema jamii iondokane na kauli ya zamani
ambayo watoto wanaambiwa kuwa kila anachosema na kufanya mkubwa ni sahihi kitu
ambacho humfanya aogope kusema anapotendewa mabaya.
Nae Mwenyekiti wa Nidhamu, Zenais Mtebe
aliiomba serikali kutoa ushirikiano na kuwapa kipaumbele watoto ili kuwasaidia
katika matatizo yanayowakabili.
“Jamii ione thamani ya mtoto na kumuona
hata mtoto wa mwenzako nae ni wako na kuvunja ukimya majumbani na kuzungumza
yale yanayotokea kwa watoto,” alisema Mtebe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni