Jumanne, 16 Juni 2015

JAJI MUTUNGI: MCHAKATO WA KUTAFUTA MGOMBEA URAISI KWA SASA HAUNIHUSU



MSAJILI wa Vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi amesema  mchakato wa kutafuta wagombea  urais unaoendelea ndani  ya vyama hauhusiani  na ofisi yake na kuwataka wananchi kuacha demokrasia ifanye kazi  ndani ya vyama husika.
Akizungumza jijini jana Jaji Mutungi alisema jamii inapaswa iache kila chama ifanye kazi kwakukuza demokrasia   katika mchakato huo wa hatua za awali na endapo kuna mtu ataenda kinyume na taratibu sheria itaweza kumbana badae kupitia pingamizi za wananchi.
“Watu wengi walikuwa wakifikiri ofisi ipo kimya  na hili suala si kweli,huwa tunawasiliana na wadau husika kwa mujibu wa taratibu   hatua ya kwenda kwenye public(umma) ni ya mwisho,kama chama kimesajiliwa tuache demokrasia ifanye kazi yake  mchakato wa ndani ya chama huwa hatuna mamlaka nao,”alisema Jaji Mutungi.
Alisema ni mapema sana kutoa tathimini ya utekelezaji wa sheria ya gharama za uchaguzi kwakuwa kwa sasa ofisi hiyo kazi yao ni kuangalia tu na si vinginevyo   muda ukifika watachukua hatua kwa mujibu wa sheria kwakuzingatia malalamiko ya wahusika.
Alisema sheria ya gharama za uchaguzi madhumuni ina lengo la kudhibiti matumizi katika chaguzi na vitendo vinavyokatazwa  na sheria ya nchi.
Alisema wananchi na wadau wa siasa wanapaswa kuzingatia sheria ya gharama za uchaguzi na kanuni zake za kikomo cha gharama ili kuondoa usumbufu  badae.
“Natoa tahadhali na angalizo kwa vyama vya siasa na wanasiasa wasipuuzie sheria  na kanuni hizi zitawaathiri nje na ndani ya chama,wanaweza wakahatarisha uteuzi wao na chama kisipofuatilia na kupitisha mgombea atawekewa pingamizi  harakati zote wanazozifanya zitakuwa hazina maana,”alisema Jaji Mutungi.
Akizungumzia kuhusu vikundi vya ulinzi na usalama vya ndani ya vyama Jaji Mutungi alisema sheria ya vyama vya siasa inapiga marufuku vyama kuanzisha vikundi ambayo vinavyofanya kazi sawa na jeshi na polisi.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa vikundi vya wanachama vilikuwa na jukumu la kuangalia usalama wa mali za chama  bila kupewa mafunzo ya kijeshi na vyeo kama wanavyofanya sasa.
“Kwa bahati mbaya kutokana na sababu ambazo zinafahamika kwa vyama vya siasa,vyama hivi vimebadili mfumo,jina,uendeshaji na muelekeo wa vikundi hivi na kuwa na mfumo wa kijeshi .
Baadhi ya vyama vikaviita vikosi vya ulinzi na usalama wa vyama(guard) kuanzisha mafunzo maalum ya kujilinda,ukakamavu  na kupambana na hata kuwekwa vyeo kama vya jeshi,jambo hili ni ukiukwaji wa sheria ya nchi hivyo navitaka vyama vilivyofanya hivyo kuvivunja vikundi mara moja,”alisema Jaji Mutungi.
Alisema katiba ya chama chochote yenye kipengele cha kuwa na jeshi ndani ni batili  na endapo wanataka mabadiliko ya wanapaswa kufuata taratibu  ikiwemo kushawishi kubadilika kwa sheria hiyo.
                     


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni