Jumanne, 16 Juni 2015

CHAMA CHA SIASA CHA AFP WAVURUGANA



CHAMA cha Taifa cha Alliance For Tanzania Farmers Party (AFP) kimemshauri msajili wa vyama vya siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi kujiepusha kuingilia migogoro ya ndani ya vyama vya siasa kutokana na kuwa inaonekana kukuza zaidi migogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Taifa wa chama cha AFP, Mwarami Uwesu, alisema kuwa msajili wa vyama anatakiwa kuacha kuingilia migogoro ya ndani ya vyama vya siasa na badala yake anatakiwa kuhimiza demokrasia.
Alisema Kamati Kuu ya AFP ilikutana machi 13 kwenye ofisi za makao makuu ya chama zilizopo Temeke na kuamua kumsimamisha Katibu Mkuu , Rashid Rai kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya chama uamuzi ambao msajili wa vyama anaupinga na kudai kutotambua.
Alisema maamuzi ya msajili ya kutotambua kusimamishwa kwa katibu mkuu wa chama hicho yanaingilia katiba yao ibara ya 10.a(3) inayosema kuwa kiongozi anaweza kukata rufaa kwa kikao cha juu iwapo hakuridhika na uamuzi wa kikao cha chini dhidi yake.
“Kutokana na maelekezo ya katiba yetu chama hakikubaliani wala hakijaridhishwa na maamuzi yaliyofanywa na ofisi ya msajili hivyo tumeamua kumpinga kwa kumuandikia barua yenye kumbukumbu namba. A.F.P/HQ/08/F1/2015 ambayo tuliiandika juni 11 na kumuomba kupitia ofisi yake kushughulikia shauri hilo kwa umakini,” alisema Uwesu.
Alisema katika barua hiyo pia walimtaka kuzingatia taratibu za ofisi yake pamoja na kuheshimu katiba ya chama chao kutokana na kuwa bado wana nafasi ya kuweza kulishughulikia suala hilo kwenye vikao vya halmashauri kuu pamoja na mkutano mkuu kwa kuwa katibu huyo hakufukuzwa moja kwa moja.
“Maamuzi ya kumsimamisha Katibu Mkuu yalifanywa na Kamati Kuu ya utekelezaji ya AFP Taifa kutokana na kuwa ndio chombo kinachofanya shughuli zote za chama kwa mujibu wa katiba yetu ibara ya 16.8(d) na 16.8(f) lakini bado Rashid anatambulika kama katibu mkuu wa chama,” alisema Uwesu.
Aidha alisema kuwa Kamati Kuu ya utekelezaji imeanza kutoa fomu kwa wagombea wa ngazi zote katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba na mwisho wa kutoa fomu hizo utakuwa Juni 30.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni