MAKAMU wa
Rais Dk. Gharib Bilal ameutangaza msiba wa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Issa Shaaban
bin Simba uliotokea juzi asubuhi katika hospitali ya TMJ kuwa wa kitaifa.
Kiongozi
huyo aliyasema hayo jana, Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete kwenye
viunga vya msikiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa ajili ya
kumsomea dua marehemu Mufti.
“Msiba wa
Mufti ni wa kitaifa na nadiriki kusema kuwa serikali imepoteza kiungo muhimu
baina yake na waislamu katika suala la kudumisha amani,”alisema.
Dk. Bilal alisema
kuwa Mufti Simba alikuwa kiongozi tegemeo katika uhamasishaji wa amani na
maendeleo ya binadamu kwa watu wa imani tofauti tofauti hapa nchini.
Makamu huyo
wa Rais alimuelezea Mufti Simba kama mtu ambaye hakuwa mbinafsi, mbaguzi, hakuwa
mtu mwenye makuu na wala hakuwa mwenye majivuno na kujiona.
Naye Mwenyekiti
wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyezungumza kwa niaba ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amemuelezea Mufti kama mtu wa watu ambaye
anastahili kukumbukwa kwa kufanya mazuri aliyoyaacha.
Mwingine
aliyemzungumza Mufti katika viwanja hivyo vya Bakwata alikuwa Mwenyekiti wa
Kampuni ya IPP Abraham Mengi alisema kuwa atamkumbuka kama rafiki na mtu
aliyekuwa mnyenyekevu.
“Hata baada
ya kupata uongozi wa juu hakubadilika, aliwapenda watu kuliko alivyojipenda
mwenyewe, Sheikh Mkuu amefariki kimwili lakini mawazo yake yataendelea kuishi
katika roho yangu kutokana na namna alivyokuwa akijitolea kuwasaidia watu,”
alisema.
Mussa Zungu alitumia
muda huo kwa niaba ya Spika na Bunge la Tanzania kwa kuwapa pole waislam,
watanzania na familia ya marehemu na kuwaomba waendeleze wema na amani aliyokuwa
akiuhubiri marehemu.
Naye Mkurugenzi
wa Msama Promotion Alex Msama alimuelezea Sheikh Simba kama mtu wa watu, aliyekuwa
akipinga kufanyiwa uonevu watu na alikuwa akijaribu kuwaunganisha waislam na
wakrito hivyo kuondoka kwake imekuwa pengo kubwa.
Waliohudhuria
katika dua hiyo ni pamoja na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Salim Ahmed Salim,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Mohammed Abood, Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Dk Wilbrod Slaa, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe.
Wengine ni Sitti
Mwinyi, Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kingunge Ngombare Mwiru, mabalozi wa
nchi za Sudan, Comoro, Palestina na Iran.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni