KUTOKANA na kuanza kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wafanyabiashara katika masoko mbalimbali wamepandisha bei za baadhi ya vyakula hali iliyoanza kuleta usumbufu kwa wananchi.
BLOG hii ilitembelea masoko kadhaa katika jiji la Dar es Salaam, leo na kubaini kuwa baadhi ya vyakula vimepanda bei mara tu baada ya Mfungo kuanza.
Katika soko la Kisutu mfanyabiashara wa ndizi za kupika, Japhary Abdallah alisema bei ya bidhaa hiyo imepanda kutoka 15,000 hadi 30,000 kwa mkungu mmoja hivyo kumlazimu yeye kuuza sh.1,000 kwa ndizi tatu.
“Leo(jana) nimenunua mkungu wa ndizi kwa sh. 30,000 kutoka kwa wakulima unategemea mimi nitauza kwa bei gani?,” alihoji Abdallah.
Mfanyabiashara wa mihogo na viazi katika soko la Mabibo, Juma Selemani alisema kiloba kimoja cha mihogo au viazi vitamu kilichokuwa kikiuzwa kwa sh.70,000 jana kimeuzwa kwa sh.110,000 na sh.100,000.
“Hali ya biashara leo ni ngumu kwa tunaofunga kutokana na vyakula hasa vinavyotumika kwa futari kuuzwa kwa bei kubwa na wakulima wanaoleta katika soko hili,” alisema Selemani
Katika soko la Kariakoo, mmoja wa wafanyabiashara wa Magimbi, Athanas Issa alisema alipata bidhaa hiyo maradufu ya bei ya awali.
“Awali magimbi mdima tulikuwa tukiyapata kwa sh.40,000 kwa kiloba cha kilo hamsini lakini leo tumepata kiloba hicho hicho kwa sh.80,000 tunauza fungu 3000, huku magimbi maji yaliuzwa kwa bei ya sh.90,000 na leo ni 150,000 kwa kiloba kikubwa nasi tunauza 4000 kwa gimbi moja,” alisema Issa.
Kwa upande wake Meneja mipango na shughuli za biashara wa soko la kariakoo, Mrero Mgheni alisema kupanda huko kwa baadhi ya vyakula kunatokana na mahitaji kuwa makubwa kuliko upatikanaji wake.
“Wiki ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani vitu hupanda kutokana na uhitaji mkubwa tofauti na upatikanaji wake” alisema Mgheni.
Alisema mpaka Juni 14, kiloba cha magimbi katika soko hilo kiliuzwa kwa sh.100,000, mihogo sh.45,000 rejareja 1,000, viazi vitamu sh.100,000 rejareja 1500na ndizi mkungu sh.16,000 hadi 19,000 na rejareja 1,000.
Naye mteja wa ndizi katika soko hilo, Asia Mohamed alisema serikali iangalie upandishaji holela wa vyakula katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani.
“Tunaiomba serikali iangalie kwa makini suala la upandishaji holela wa vyakula kwani tunapata shida sisi tuliofunga , huku ni kutufanyia makusudi ili wafanyabiashara wajipatie fedha nyingi kipindi hiki,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni