Jumapili, 31 Mei 2015

MLEZI ASASI YA NEW HOPE FOR GIRLS ANAOMBA MSAADA



MLEZI wa asasi ya kiraia inayohudumia wasichana wanaotoka katika mazingira magumu (New Hope for Girls organization), Consoler Wilbert, amewaomba wananchi kumchangia nauli ya kwenda kwenye matibabu nchini India baada ya hospitali hapa nchini kumpa rufaa akatibiwe huko.
Consoler ambaye amekuwa ni muhanga wa unyanyasaji wa watoto wa kike, alisema anasumbuliwa na maumivu ya kichwa na mgongo mara kwa mara yaliyotokana na kupigwa kwa masaa sita na walimu wake wakati akisoma sekondari ya Jitegemee iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya hedhi salama duniani jijini Dar es Salaam Consoler alisema alilazimishwa kuolewa akiwa na umri mdogo na alipokataa alikuwa anapigwa mara kwa mara shuleni na nyumbani.
“Siku moja nilipigwa sehemu mbali mbali za mwili hasa kichwani na mgongoni na walimu wanne huku wakiniambia nisali sala yangu ya mwisho kutoka saa nne asubuhi hadi saa 10 jioni.
“Nilikuwa nikiishi maisha ya kuomba omba mitaani ili nipate fedha kwa mahitaji ya shule nikiwa nimevaa sare za shule nikawa naitwa ‘malaya aliyejificha kwenye unifomu za shule’ iliniuma sana,”alisema Consoler.
Alisema baada ya kipigo hicho amekuwa na maumivu makali ya  kichwa na mgongo ambayo humfanya asiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kwani muda mwingi huutumia kwa kulala tu.
Anaomba kwa yeyote atakayeguswa na matatizo yake amsaidie kwa hali na mali ili akapate tiba na anayetaka kuwasiliana nae kwa namba za simu ambazo ni 0715025565 na 0787025565.
Alisisitiza kuwa  kwa sasa amewasamehe wote waliomfanyia anachohitaji ni kutibiwa ili arudi katika hali yake ya kawaida.
Aidha aliwataka wototo wa kike wasinyamaze wanapokutana na manyanyaso ya aina yoyote yale ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa majirani.
Kwa sasa asasi ya New Hope For Girls inawahudumia watoto wa kike 147 ambao wanatoka katika mazingira magumu na kati yao 24 wanaishi pamoja na mlezi huyo.
mwisho                                                 

MBARONI KWA KUJIFANYA ASKARI WA JIJI




MKAZI wa Kariakoo Mjini Dar es Salaam Godfrey Kwikwilukiza (33),jana amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo akikabiliwa na tuhuma za kujipatia kiasi cha fedha Sh 20,000 kwa njia ya udanganyifu.
Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Christine Ruguru,Karani wa Mahakama hiyo Lucy Rutabanzibwa, alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 23 mwaka huu eneo la Stesheni.
Rutabazibwa alidai Mahakamani hapo kwamba mtuhumiwa alijipatia fedha hizo toka wa mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Shabaan Salum, kwa kudanganya kuwa yeye ni askari wa jiji.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea ambapo Hakimu alidai kuwa mshtakiwa anatakiwa alete wadhamini wawili wenye barua kutoka serikiali za mitaa watakaoweka bondi ya maandishi ya Sh. Laki 1 kwa kila mmoja.
Hata hivyo mshtakiwa alirudishwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kesi hiyo itakuja tena kusikilizwa hoja za awali Juni 11 mwaka huu.

TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA HEDHI SALAMA KWA MARA YA KWANZA



TANZANIA kwa mara ya kwanza imeadhimisha siku ya hedhi salama duniani ambapoWizara ya Elimu kwa kushirikiana na wadau wataendelea kusimamia sera inayotaka kuondoa vikwazo vyote vinavyomsababisha mwanafunzi kutohudhuria masomo hasa kwa wanafunzi wakike wanapokuwa hedhi.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Hedhi duniani jijini Dar es Salaam, Afisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi, Madina Kemilembe alisema kukosekana kwa miundombinu rafiki mashuleni kunasababisha wanafunzi kukosa masomo.
Alisema ukosefu wa mazingira bora kama vyoo, maji safi na salama, sabuni ya kunawia pamoja chumba cha kubadilishia nguo hasa kwa watoto wakike wanapokuwa hedhi mashuleni kunasababisha utoro mashuleni.
“Nawashukuru wadau Water Aid, Shirika la maendeleo la Uholanzi(SNV), Kasole Secret pamoja na wengine kwa kuisaidia serikali kuandaa mazingira rafiki kwa watoto wetu kwa kuwajengea vyumba vya kubadilishia na kuwapelekea maji safi na upatikanaji wa pedi kwa baadhi ya shule,” alisema Kemilembe.
Alisema kutokana na ukosefu wa pedi baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitumia vitambaa visivyosalama na wanapovifua vinaanikwa chini ya godoro hivyo kusababisha magonjwa mbalimbali kama fangasi kwa kutokauka vizuri.
Alisema ifikie wakati jamii ivunje ukimya kwa kuongelea suala la hedhi kwa uwazi kwani linamyima mtoto wa kike masomo hasa kipindi anapokuwa hedhi.
“Elimu itolewe kwa wazazi pamoja na wanafunzi wote wa kike na wa kiume ili kuondoa unyanyapaa ili kuboresha mazingira ya kusoma kwa mtoto wa kike,” alisema Kemilembe.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Girls in control menstral hygien management kutoka Shirika la Maendeleo Uholanzi, Rozalia Mushi alisema mradi wake utaendelea kuangalia jinsi ya kumsaidia mtoto wa kike aliyeko mashuleni ili kumuongeza ufaulu katika masomo yake.
“Mtoto wa kike anakosa vipindi 450 kwa mwaka anapokuwa katika hedhi kitu ambacho kinampunguzia ufaulu katika masomo yake kutokana na kutokujiamini na unyanyapaa anapokuwa darasani,” alisema Mushi.
Alisema walimu pia walikuwa wakitoroka kufundisha kutokana na kuwa katika hali hiyo hivyo waliamua kujenga vyumba vya kubadilishia katika shule mbalimbali.
Nae Mkurugenzi wa Water Aid, Ibrahimu Kabole alisema kuna uelewa mdogo pamoja na mila potofu zinazofanya jambo la hedhi kuonekana ni la aibu.
“Asilimia 40 ya wanafunzi wa kike hutoroka shule kutokana na kuzomewa,kunyanyapaliwa pamoja na kukosa mazingira rafiki wanapokuwa kwenye hedhi,” alisema Kabole.
Alisema jamii ipewe uwezo kujua jambo hilo na liongelewe kwa uwazi ili kuwajengea mazingira bora ya kusoma.
Siku ya hedhi duniani kwa mara ya kwanza imeadhimishwa nchini kwa maandamano ya wanafunzi wa kike kutokea Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi na kumalizikia viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.  
   

WAZAZI KAMPALA UNIVERSITY(KIU) KUANDAMANA



WAZAZI na walezi wa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi katika chuo cha kimataifa cha Kampala(KIU), wamepanga kuandamana kwenda chuoni hapo ili kupata ufafanuzi kuhusu madai ya watoto wao kuhusu usajili kamili wa kozi ya famasia.
Wakizungumza kwa wakati tofauti na MTANZANIA wazazi hao wamesema wameamua kujikusanya ili watambuane na kujua hatima ya watoto wao kielimu.
Mmoja wa wazazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Bumbuli alisema wametengeneza kundi kwenye mitandao ya simu inayowawezesha kuwasiliana ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
“Sisi ndio tunalipa ada na ndio tunaojua ada tunapata wapi, Chuo itabidi kitueleze ukweli ni lini watasajili kozi na si kutudanganya kama wanavyowaambia wanafunzi kwani sisi si watoto wadogo,” alisema Bumbuli.
Alisema ilibidi wawaambie watoto wao waahirishe muhula mpaka hapo kozi hizo zitakaposajiliwa lakini uongozi wa Chuo hicho unawakatalia kitu ambacho kinawatia hofu.
Naye Mohamed Khasimu alisema chuo kimekuwa na gharama zisizojulikana kama kulipia mitihani na gharama nyingine ambazo kipindi cha mkataba hazikuwepo hivyo wataenda chuoni hapo kabla ya mitihani kuanza ili kupata maelezo ya kina.
“Tutakutana na Uongozi wa Chuo watujibu madai ya watoto wetu kama hatutoridhika basi tutajua nini cha kufanya,” alisema Khasimu.
Alisema wototo wao wamekuwa wakikaripiwa na kutishiwa kufukuzwa chuo kila walipojaribu kuhoji usajili wa kozi.
Hivi karibuni wanafunzi wa kada ya famasia chuoni hapo waligoma kuingia darasani kuushinikiza uongozi kutoa ufafanuzi kuhusu usajili wa kozi wanazosoma pamoja na madai mengine sita.
                                                   


Jumanne, 26 Mei 2015

KESI YA MBASHA YAPIGWA TAREHE TENA



Kesi inayomkabili Mwimbaji wa nyimbo za Injili na mfanyabiashara Emmanuel Mbasha imeendelea leo katika mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kumsikiliza shahidi namba sita, Secherela Challo.
Shahidi huyo alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Flora Mjaya na Mwendesha Mashtaka Munde Kalombora.
Mbasha anadaiwa kumbaka shemeji yake (17) kati ya Mei 23 na 25, 2014 eneo la Tabata ambako alikuwa akiishi naye.
Septemba 5 mwaka jana binti huyo aliieleza Mahakama kuwa alibakwa na shemeji yake huyo kwa awamu mbili tofauti kabla ya kufanikiwa kukimbia.
Kwa sasa Kesi hiyo inasikilizwa Mahakamani hapo  kwa siri kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu ili kulinda haki ya binti huyo.
Tayari mashahidi watano akiwamo binti huyo, Flora ambaye ni mke wa Mbasha.
Daktari aliyemfanyia vipimo wamekwisha kutoa ushahidi mahakamani hapo ambapo alisema katika kufanya vipimo  hakukuwa na ushahidi wowote ulioonyesha kuwa Mbasha alimwingilia kimwili binti huyo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 16, mwaka huu itakapotajwa tena.