Jumatatu, 6 Julai 2015

DIWANI WA MBAGALA AAGA RASMI



DIWANI wa kata ya Mbagala, Manispaa ya Temeke,jijini Dar es Salaam,Aggrey Kayombo amewataka viongozi wa dini kufundisha maadili ya kitanzania hasa kwa vijana ambao kwa sasa wanakumbwa na wimbi la utandawazi na kupoteza asili yao.
Kayombo aliyasema hayo juzi katika msikiti wa Salama uliopo kizuiani Mbagala wakati akizungumza na viongozi wa Bakwata wa kata hiyo katika hafla fupi ya kuwaaga na kuwashukuru kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi cha uongozi wake.
“Viongozi wa dini mna nafasi kubwa katika kutoa elimu ya maadili kwa vijana na watoto ili waweze kuwa na tabia njema na kioo cha taifa la kesho hivyo basi timizeni wajibu huu, ” alisema Kayombo.
Alisema kuwa walimu wa dini wana nafasi kubwa kuliko viongozi wa siasa katika ulinzi wa amaani na utulivu kutokana na mafundisho yao ya kumjua Mungu na kutambuana wenyewe ambayo huleta hofu ya Mungu na hivyo kuleta amani ya nchi.
Aidha aliwaomba kuwapa ushirikiano wale wote wanaoomba kugombea uongozi kwa ngazi mbalimbali kwani  wako sahihi kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi.
“Wazee wangu nawaomba ushirikiano mlionipa mimi mpeni yeyote atakaechaguliwa kuwa kiongozi katika nafasi  yoyote  hii ndio demokrasia,” alisema Kayombo.
Awali akisoma risala kwa niaba ya viongozi hao, katibu wa Bakwata wa kata ya Mbagala, Saidi Msati alisema Diwani huyo aliweza kuwaunganisha viongozi wa dini mbalimbali ndani ya kata hiyo na kuleta mshikamano, umoja na amani ambayo imedumu muda wote alipokuwepo madarakani.

                                 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni