Jumatatu, 6 Julai 2015

HUKUMU YA POLISI YAWAACHA NDUGU WA MLALAMIKAJI HOI



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mkuranga imemwachia huru askari polisi mwenye namba 3949 Cpl Innocent Haule, ambaye alikuwa akikabiliwa na shitaka la kumpiga na kumjeruhi Abdul Jongo kwa kutumia rungu.
Askari huyo aliachiwa huru juzi na mahakama hiyo kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake pasi kuacha shaka yoyote.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Agnes Mchome alikiri kuwepo mahakamani hapo ushahidi uliothibitisha kijana kupigwa na askari huyo.
“Kutokana na ushahidi wa daktari umeonyesha kweli alipigwa kichwani na kitu kizito na kumsababishia majeraha,” alisema Mchome.
Alisema katika ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo hakuna sehemu iliyoonyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na dhamira ya kumpiga na wala hakuna zana iliyoletwa mahakamani na kudaiwa kutumiwa na mshtakiwa.
“Upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa pasi kuacha shaka yoyote, hivyo mahakama inamwachia huru mshitakiwa,” alisema Hakimu huyo.
Awali akisoma shitaka hilo mbele ya hakimu mkazi, wakili wa serikali Debora John alidai kuwa mnamo disemba 26, 2010 katika eneo la Vikindu wilayani humo, mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kumpiga na rungu Abdu Jongo na kumsababishia jeraha kichwani.
Hukumu hiyo iliacha maswali mengi hasa kwa ndugu wa mlalamikaji kwa kuwa hakimu alikiri kuwepo ushahidi ulioonyesha dhahiri kupigwa.
mwisho

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni