Jumanne, 14 Julai 2015

WANAOGAWA VIWANJA JANGWANI KUKIONA



MANISPAA ya Ilala imesema itawachukulia hatua watu wanaogawa viwanja kwa wamachinga katika eneo la jangwani kwa madai kuwa wameruhusiwa na uongozi kufanya hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Isaya Mngurumi alisema hawajamruhusu mtu yeyote kugawa viwanja bali waliwaruhusu kupanga chini bidhaa zao kama wanavyofanya katika mitaa ya kariakoo.
“Nimetuma timu kuwatafuta watu wanaogawa maeneo hayo kwani waliokimbilia huko si walengwa ni wajanja wachache tu,” alisema Mngurumi.
Alisema walikaa na uongozi wa manispaa ili kutafuta eneo la wafanyabiashara wadogo ndipo wakateua jangwani kuwa sehemu ya muda wakiwa bado wanaandaa masoko rasmi.
“Tumechagua jangwani upande wa kushoto wa barabara kama unaelekea kigogo kama sehemu ya muda kabla hatujaweka miundombinu ya vyoo wamevamia na kugawana bila ruksa ya manispaa,” alisema Mngurumi.
Alisema upande wa kulia wa barabara ni eneo la huduma za kijamii hasa uwanja wa mikutano ya hadhara na stendi ya mabasi yaendayo kasi.
Aidha alisema wako katika mkakati wa kujenga masoko ambayo yatawasaidia wafanyabiashara hao wadogo kuwa katika maeneo ya kudumu ya kufanyia shughuli zao.
Aliyataja masoko hayo kuwa ni Kisutu, Buguruni na Mchikichini ambapo wanaongea na wadau mbalimbali ili kupata mikopo kwa ajili ya ujenzi.
“Tumeingia mkataba na Benki ya TIB ili kujenga soko la kisutu kwa gharama ya sh. bilioni 11,” alisema.
mwisho  
         

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni