Jumanne, 21 Novemba 2017

'kuweni wazalendo'

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Alias Kwandikwa amewataka wataalamu wa ujenzi kuwa wazalendo kwa kuokoa gharama za ujenzi wa majengo mbalimbali ili kulipunguzia mzigo taifa.
Akizungumza katika ziara yake aliyoifanya juzi katika mradi wa ujenzi wa nyumba za Wakazi wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam, Kwandikwa alisema uzalendo unahitajika hasa katika kipindi hiki taifa likiwa katika mageuzi makubwa kiuchumi.
Alisema wataalamu wanatakiwa kuwa wazalendo wakati wakisimamia miradi mbalimbali ya ujenzi ili kuokoa fedha zitakazokwenda katika miradi mingine.
“Wakati tunaangalia matumizi ya miradi ya serikali tujiulize kwenye familia zetu tunafanya hivi?,” alisema Kwandikwa.
Alisema wataalamu wa ujenzi waende kujifunza namna ya kupunguza gharama za ujenzi kwa  Wakala wa Ujenzi Tanzania(TBA) ambao katika miradi yao wamepunguza kwa kiwango kikubwa.
“Endeleeni kuokoa fedha kadri mnavyoweza baadaye mtatuambia kiasi mlichookoa ili zisaidie katika miradi mingine ya kitaifa,” alisema Kwandikwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga alisema wataendelea kufanya utafiti wa kushusha gharama za ujenzi ili kuongeza ushindani wa kibiashara.
Alisema mradi wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota utagharimu Sh Bilioni 20 mpaka kukamilika.
“Uzalendo ndio unaotufikisha hapa kwani vijana tulionao wanatanguliza maslahi ya Taifa mbele,” alisema Mwakalinga.
mwisho    


Elimu ya Ufundi changamoto kwa viwanda

TANZANIA inakabiliwa na upungufu wa walimu wa elimu ya ufundi jambo ambalo linasababisha baadhi ya vyuo vya ufundi stadi kuajiri walimu wasiokuwa na sifa zinazohitajika katika fani hiyo.
 Mpaka sasa kuna idadi ndogo ya vyuo vinavyofundisha ualimu wa ufundi stadi jambo linalosababisha kuwapo na walimu wasiokuwa na sifa katika vyuo vya elimu ya Ufundi.
Vyuo vya  mafunzo ya Ufundi stadi ni nguzo pekee ya kulisaidia taifa kuingia katika uchumi wa viwanda mwaka 2020 huku nchi ikitegemea kuingia katika uchumi wa kati.
Hivi karibuni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(NACTE) kwa kushirikiana na Kituo cha elimu ya watu wazima Kouvola kutoka nchini Finland waliandaa mkutano wa Kimataifa ili kubadilishana uzoefu kati ya nchi hizi mbili.
Mkutano huo ulibeba ujumbe wa ‘wekeza katika elimu ya ufundi ili Tanzania iweze kuingia katika uchumi wa viwanda’ umehuhudhuliwa na taasisi za elimu ya ufundi, wamiliki wa viwanda, wadau na wataalamu 30, wa sekta hiyo kutoka nchini Finland.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Elimu nchini Finland Dk.Tuija Arola anaelezea nchi hiyo ilivyoweza kuwekeza katika mafunzo ya wakufunzi wa elimu ya ufundi.
Anasema kuna umuhimu wa nchi kuwa na walimu waliobobea katika elimu ya ufundi stadi ili kuweza kutoa wahitimu waliokuwa na sifa za kukidhi soko la ajira.
“Walimu wa mafunzo ya ufundi stadi wanatakiwa kuwa na mafunzo endelevu katika kipindi chote cha ualimu wao ili kwenda na mabadiliko ya kasi ya teknolojia,” anasema Dk. Arola.
Anasema walimu wanatakiwa kutembelea katika maeneo ya viwanda kupata ujuzi mpya unaohitajika katika wakati husika.
Anasema Tanzania inatakiwa kuwekeza katika kuwaandaa wakufunzi wa mafunzo ya ufundistadi ili kufanikisha malengo ya kuwa nchi ya viwanda.
Akitolea mfano katika nchi ya Finland Arola anasema taaluma ya ualimu na ukufunzi nchini humo inathaminika na kuheshimika jambo ambalo linawaongezea nguvu wakufunzi katika kutekeleza majukumu yao.
Anasema kwa kuwa mafunzo ya wanafunzi huhamishiwa katika maeneo ya kazi hivyo wakufunzi wana wajibu wa kuratibu ushirikiano na kampuni zenye kutoa ajira kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi.
“Mkufunzi ana nafasi kubwa katika kuwezesha juhudi za kujifunza kwa mtu mmoja mmoja ili kufikia malengo yake binafsi,” anasema Dk. Arola.
Anaongeza kuwa kutokana na hali hiyo wakufunzi wa mafunzo ya ufundi wanatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha juu katika fani zao.
Anasema wakufunzi wa elimu ya ufundi wanatakiwa kutumia mbinu mbadala katika kuongeza kiwango chao cha elimu na ujuzi.
Aidha anazitaka mamlaka husika katika kusimamia elimu ya ufundi kuwatengenezea mazingira ya kazi wakufunzi hao ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha ili waweze kutimiza majukumu yao kikamilifu.
“Mabadiliko ya utendaji kazi wa walimu unahitaji kujitolea zaidi hivyo watafanikiwa iwapo tu watapata ushiriki na kuungwa mkono na mamlaka ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kifedha,” anasema Dk.Arola.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako anasema serikali inawekeza katika kuwaandaa walimu wa elimu ya ufundi ili kuwa na wataalamu wataoiwezesha nchi katika kuingia katika nchi ya viwanda.
Anasema nchi haiwezi kuingia katika uchumin wa viwanda bila kuwekeza katika raslimali watu watakaofanya kazi katika viwanda hivyo.
“Tujitathmini kuinua ubora wa elimu ya ufundi kwa kuchukua uzoefu kutoka kwa wenzetu kutoka Finland kwa kuwa wenzetu wamefanikiwa katika elimu ya ufundi,” anasema Profesa Ndalichako.
Anasema changamoto iliyopo ni muunganiko wa ubunifu unaofanywa na taasisi za mafunzo ya ufundi na viwanda.
“Changamoto ni namna ya kuunganisha ubunifu unaotolewa na taasisi za mafunzo kuingizwa katika maisha ya kawaida ya watanzania,” anasema Ndalichako.
Profesa Ndalichako anasisitiza juu ya mafunzo ya walimu na wahitimu katika taasisi za juu ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Niwaombe tufanye kazi kwa kushirikiana taasisi za mafunzo na waajiri kuangalia namna ya kupunguza utengano uliopo kwa kuwa kila mmoja anamtegemea mwenzake,” anasema Ndalichako.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk.Adolf Rutayuga anasema Baraza hilo linahakikisha kuwa wahitimu wanaotolewa na vyuo vilivyosajiliwa wanakidhi vigezo vya ajira na mahitaji ya soko.
Anasema kwa kuwa katika mkutano huo walikuwapo pia watoa maamuzi akiwamo waziri Ndalichako hivyo yatafanyiwa kazi na kupata suluhisho mapema.
“Hapa tumekuwa na viongozi wakubwa na watoa maamuzi hivyo yote yaliyozungumziwa katika mkutano huu yatapatiwa ufumbuzi kulingana na mahitaji,” anasema Dk.Rutayuga.
Anasema hii ni hatua moja ya kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kuwa waliokutana hapa ni wadau wakubwa katika sekta hiyo.
“Yamejadiliwa mengi katika mkutano huu hii ni hatua moja mbele kuelekea Tanzania ya Viwanda kwa kuwa tunaunganisha nguvu kwa maana ya Watoa Mafunzo na waajiri ama wenye viwanda,” anasema Dk. Rutayuga

Marufuku kusambaza takwimu za uchumi hila kibali

Na TUNU NASSOR 
DAR ES SALAAM 
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS ) imewaonya watu wanaotoa takwimu za Uchumi bila kuzingatia sheria ya Takwimu jambo ambalo linasababisha mkanganyiko katika jamii. 
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema hairuhusiwi kutoa takwimu hizo bila kuwa na kibali cha NBS. 
Alisema NBS haikatazi mtu binafsi wala kikundi cha watu kukusanya takwimu isipokuwa kinachotakiwa ni kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kupata kibali kutoka katika Ofisi hiyo. 
"Hatumnyimi mtu kibali cha kukusanya kuchakata na kusambaza takwimu isipokuwa kinachotakiwa ni kukusanya kulingana na misingi na sheria namba tisa ya Takwimu, " alisema Dk. Albina. 
Alisema ukusanyaji huo unahitaji weledi wa hali ya juu chini ya kanuni 10 za Takwimu za Dunia. 
" kinachonishangaza takwimu za serikali zinapotolewa mtu anasimama na kusema takwimu hizi si sahihi... Hii inatokea Tanzania pekee, hivyo asitokee mtu kupotosha takwimu za Uchumi " alisema Dk Albina. 
Alisema takwimu za Uchumi ni muhimu kwa utekelezaji wa ajenda ya Afrika ya mwaka 2063.
"Katika ajenda hii kitu kimojawapo ni ukuaji wa uchumi wa bara hilo na haiwezi kufanikiwa bila kuwa na takwimu bora za Uchumi,"  alisema Dk Albina. 
Naye Mkurugenzi wa Uchumi na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT), Johnson Nyella aliwataka wananchi wanaoshiriki katika ukusanyaji wa takwimu kutoa taarifa sahihi wanapojaza dodoso za takwimu

Jumatatu, 16 Oktoba 2017

ushahidi wa tatu watua takukuru

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) amewasilisha ushahidi mwingine kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU

Madiwani hao nane wa Chadema wamejiuzulu kwa kile walichoeleza kumuunga mkono Rais John Magufuli jambo ambalo Nassari anadai siyo kweli bali walinunuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo nje ya ofisi ya Takukuru Upanga jiji ni humo alisema huu ni ushahidi wa tatu na kadri upepelezi ukiwa unaendelea ataleta mwingine, kwani ni kama filamu ya Isidingo.

Nassari alisema alitarajia Rais Dk. John Magufuli angewachukulia hatua wateule wake wanaohusishwa katika sakata hilo ili kupisha uchunguzi uweze kufanyika kwa uhuru.

"Tunajiuliza kwa nini Rais hawachukulii hatua DED, DAS au DC wote wa Arumeru kwa kutuhumiwa, watupeleke mahakamani na tungeomba suala hili lichukuliwe kwa uzito wake," alisema Nassari

Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubunea aliyeongozana na Nassari alisema ameshiriki kuwashauri kuutoa ushahidi huo kwa umma ili jamii ijue ukweli.
"Tunachojiuliza kwa nini rais yupo kimya, kwa nini mawaziri na viongozi waliotuhumiwa Katika sakata la Almas na Tanzanite aliwasimamisha kwa nini hawa hataki," alihoji Kubenea

Jumatano, 9 Agosti 2017

atakayefanya udanganyifu vyei vya kuzaliwa na vifo kukiona



WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Bodi ya mikopo ya elimu ya juu(HESLB)wametoa onyo kali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakaofanya udanganyifu wa vyeti vya kuzaliwa na vifo ili wapatiwe mkopo.
Onyo hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa wa RITA, Emmy Hudson alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wametoa onyo hilo kutokana na kubainika kwa vyeti kughushi takribani 500 vya kuzaliwa na vifo kwa waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/17.
Alisema vyeti hivyo havikuwa katika kumbukumbu zao na hivyo walishindwa kuvitambua.
“Sheria ya vizazi na vifo inamtia hatiani mtu yeyote ambaye atatoa taarifa za uongo hivyo vyombo vya dola vitawashughulikia wanaofanya udanganyifu huu,” alisema Emmy.
Alisema kwa kushirikiana na HESLB wameanzisha mfumo maalumu wa uhakiki kwa kutumia mtandao ambapo mwombaji atatuma cheti cha kuzaliwa na vya vifo kutumia email na vitahakikiwa.
“Waombaji watatakiwa kuhakikiwa katika ofisi za wilaya zilizotoa vyeti hivyo na makao makuu ya RITA na walioko mbali watumie barua pepe ya uhakiki@rita.go.tz wakiambatanisha vyeti na risiti za benki baada ya kulipia,” alisema Emmy.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdulrazaq Badru alisema wanufaika wa mikopo wanatakiwa kuwasilisha cheti cha kuzaliwa , vyeti vya masomo na vyeti vya vifo kama alifiwa na wazazi wake.
“Nyaraka hizi ni muhimu sana katika usajili wa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ili kupata wanaostahili kunufaika,”alisema Badru.
mwisho

Jumanne, 20 Juni 2017

MEYA JACOB AZIDI KUSOTA MAHABUSU

MEYA wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob(Chadema) ameendelea kusota mahabusu baada ya kukamatwa na Jeshi la polisi jana.
Akizungumza na MTANZANIA Ofisa habari wa Chadema Tumaini Makene alisema taarifa walizonazo ni kwamba anashikiliwa na jeshi hilo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori.
Makene alisema mpaka sasa hawajui kosa analotuhumiwa Jacob japokuwa wameambiwa atakaa mahabusu kwa saa 48.
“Ni vizuri umwulize Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kuhusu kosa alilotenda Meya kwani hata sisi hatujui kinachoendelea,” alisema Makene.
Alisema viongozi wengine wa Chadema waliofika kituo cha polisi wilaya ya Ubungo walifukuzwa huku Katibu wa Chadema Wilaya hiyo, Justine Mollel, naye akikamatwa baada ya kwenda kumtembelea Jacob.
 Akizungumza na kituo cha runinga cha Azam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori alisema ameamua kumkamata Jacob kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kuwaleta wanachama wa Chadema wa kanda ya Pwani na kuwatembeza katika miradi ya maendeleo ya halmashauri.

Makori alisema kwa mujibu wa sheria na taratibu, mwenye mamlaka ya kukagua miradi ya maendeleo ni wajumbe wa kamati ya Maendeleo wa Halmashauri chini uenyekiti wa Meya ama Mwenyekiti wa Halmashauri.
“Hivyo kitendo cha Meya kutembelea miradi ya maendeleo bila madiwani wa kamati husika ni kuvunja sheria,na dawa yake ni kukaa ndani na kufunguliwa mashtaka,” alisema Makori.
Alisema ameagiza pia kukamatwa na kutiwa ndani kwa viongozi wengine waliokuwa katika msafara huo aliwamo Waziri Mkuu mstaafu na Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Pwani Frederick Sumaye kujibu ni kwanini walikwenda kutembelea miradi ya maendeleo bila idhini ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo.

“Kitendo cha Meya kutumia ukumbi na majengo ya halmashauri kukutana na viongozi wa Chadema ni kinyume na kanuni na sheria za utumishi wa umma,hivyo nimeagiza Meya huyo kukaa ndani kwa masaa 48 kabla ya kufunguliwa mashtaka,huku Sumaye na viongozi wengine wasakwe na kuwekwa ndani.

mwisho


Dk. Mashinji huyoo Ghana

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Vincent Mashinji ni mmoja wa Viongozi wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) walioalikwa kukutana na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo nchini humo, Jumatano, Juni 21, mwaka huu,
Taarifa iliyotolewa na  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Tumaini Makene imesema mwaliko huo ni sehemu ya mkutano wa umoja huo utakaofanyika mjini Accra, Ghana.
Alisema mbali ya kukutana na Rais Nana Akufo-Addo, Dk. Mashinji atakutana na Rais Mstaafu wa Ghana John Agyekum Kufuor kwenye mazungumzo yatakayofanyika Juni 20, mwaka huu, baada ya ujumbe huo wa IDU kutembelea Bunge la Ghana.
“Viongozi hao mbali ya kubadilishana uzoefu wa mazingira tofauti ya kisiasa, watatumia mkutano huo kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ambavyo nchi zao zinaweza kusimamia misingi ya kidemokrasia kwa ajili ya maendeleo na ukuaji wa kiuchumi, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kunufaika na ongezeko kubwa la vijana,” alisema Makene.
Alisema mkutano huo wa IDU ulioanza Juni 19, mwaka huu, unawakutanisha viongozi kutoka nchi mbalimbali wakiwamo viongozi kutoka Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA), miongoni mwao akiwa ni Kiongozi wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC), ambaye pia ni Mwenyekiti wa DUA Dk. Kizza Besigye kutoka Uganda, Katibu Mkuu wa DUA Charles Owiredu na Mwenyekiti wa Heshima wa DUA, Peter Mac Manu.
Katibu Mkuu Dk. Mashinji aliyeondoka Juni 18, kwa ziara hiyo ya kikazi atarejea nchini Juni 22, mwaka huu.

mwishoDk

serikali yaufyata kwa walemavu


WAZIRI wa Mambo ya ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mwigulu Nchemba leo bungeni amefunguka na kuomba radhi dhidi ya vitendo vya jeshi la polisi kutumia nguvu kubwa kupambana na watu wenye ulemavu.
Mwigulu Nchemba amekiri kuwa jeshi la polisi lilitumia nguvu kubwa mno kwa watu hao na kusema serikali wamepokea jambo hilo na kuahidi kulifanyia kazi ili siku nyingine lisijirudie.
"Kwanza naomba niombe radhi kwa jambo hili na naomba salamu zangu ziwafikie watu wenye ulemavu, ni kweli kwamba kwa kuzingatia hali yao jeshi la polisi lilitumia nguvu kubwa, ila sisi kama serikali tumeshawasiliana na TAMISEMI na kuzungumza nao juu ya mambo yao, lakini pia tumepokea jambo hili na tunalifanyia kazi ili siku nyingine jambo hili lisijirudie" alisema Mwigulu Nchemba
Mnamo tarehe 16, Juni, 2017 jijini Dar es Salaam jeshi la polisi lilitumia nguvu kubwa ikiwepo kuwapiga na kuwadhalilisha watu wenye ulemavu ambao walikuwa wamejikusanya katika barabara ya Sokoine, Posta Jijini Dar es salaam ili kwenda kumuona Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, kuwasilisha malalamiko dhidi ya askari wa usalama wa barabarani kuwakamata na kuwazuia kuingia katika jiji. Lakini pia walikuwa wakipigania haki yao ya kuwa na maeneo ya kuegesha vifaa vyao katikati ya jiji.
CHAMA cha watu wenye ulemavu mkoa wa Dar es Salaam(Chawata),wamelaani kitendo cha wao kunyanyaswa na kupigwa na Jeshi la Polisi walipokuwa wakienda kwa mkurugenzi wa manispaa ya Ilala kupeleka kero zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Hamadi Komboza alisema katika tukio hilo la  Juni 16, Mwaka huu, Mtaa wa Sokoine jijini Dar es Salaam walipigwa na kupandishwa kwenye gari kama gunia.
 “Tulikuwa tunaelekea kwa Mkurugenzi wa Ilala tulipofika njiani askari walituvamia wakarusha mabomu ya machozi na kutupiga huku wakiturusha kwenye gari lao (Difenda) kama gunia,” alisema Komboza.
Alisema walipofikishwa kituo cha polisi waliwekwa mahabusu kwa muda wa saa nane sehemu ambayo ni chafu bila kujali hali zao kwa kuwa wengine hutumia mikono kutembea.
Aliongeza walipokuwa mahabusu walipigwa marungu huku wakiombwa rushwa ya Sh. 10,000 kwa kila bajaji.
“Waliokataa mpaka sasa bajaji zao zinaendelea kushikiriwa na jeshi hilo kituo cha kati na waliolipa waliruhusiwa kutoka,” Komboza.
Mmoja wa waathirika hao GFatuma Abdallah alisema alidhalilishwa kwa kukamatwa na askari wa kiume huku nguo zake zikichanika na kuacha maungo yake wazi.
Akizungumza huku aliwa analia Fatuma alisema alipofikishwa kituo cha kati aliambiwa akaandikishwe kwa askari mwanamke wakati tayari alikuwa amedhalilishwa.
“Nilipokuwa napakizwa ndani ya gari nguo zangu zilichanika na kuacha maungo yangu wazi mbele ya wanaume,” alisema Fatuma.
Wakati huohuo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelaani tukio hilo walilofanyiwa walemavu hao.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa tume hiyo Bahame Nyanduga ilisema THBUB imefuatilia tukio hilo kwa kuzungumza na viongozi wa walemavu na mamlaka husika, hususani Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam na kuelezwa kuwa mnamo Juni 16,Mwaka huu watu wenye ulemavu wapatao 200 wakiwa na vyombo vya moto, vijulikanavyo kama “bajaji”, waliziba barabara ya Sokoine kwa madai ya kutaka Mkurugenzi asikilize madai yao yahusuyo wenzao kukamatwa kwa kuendesha vyombo vyao bila kufuata taratibu za sheria.

“Taarifa za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zilionyesha askari wa Jeshi la Polisi wakiwapiga watu hao wenye ulemavu pamoja na kwamba watu wenye ulemavu walikiuka taratibu za sheria ni wazi kwamba wakati wa kuzuia uvunjifu huo wa sheria, kulikuwa na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watu hao wenye ulemavu wakati wakikamatwa na kuingizwa kwenye magari,” alisema Nyanduga.
Alisema hakuna mtu anayepaswa kuvunjiwa haki zake wakati wa kutekeleza sheria.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya 13 (6) (e) ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
Haki hizi pia zimeainishwa ndani ya mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia,” alisema.
Alisema Tume inapenda kulikumbusha Jeshi la Polisi kwamba kukimbilia kuwapiga raia kila wanapoonekana kukinzana na sheria ni matumizi mabaya ya madaraka yao.
“Ni wajibu wa polisi kulinda usalama wa raia bila kuwadhalilisha, kuwatesa na kuwapiga. Matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa kutekeleza sheria ni uvunjifu wa sheria,” alisema Nyanduga.
Alisema pamoja na uvunjifu wa sheria uliotendwa na watu wenye ulemavu kitendo cha kuwapiga bila kuwapa muda wa kutawanyika, au kutoa hoja za malalamiko yao kupitia kwa wawakilishi wao ni kitendo cha kuwadhalilisha.
“Tume inatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuzingatia kanuni, sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku,” alisema.
Alisema ni vema kwa jeshi hilo kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara askari polisi na maafisa wake kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora wakati wa kuratibu  na kushughulikia masuala ya maandamano na mikusanyiko ya raia.
“Polisi wahakikishe kuwa maafisa na askari wake hawatumii nguvu kupita kiasi wawapo katika operesheni zinazohusu raia waliokusanyika kwa amani, na hususan watu wenye ulemavu, ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“Tume inatoa wito kwa raia kwa ujumla, wakiwemo watu wenye ulemavu, kwamba hamna mwananchi au mtu yeyote aliye juu ya sheria, na kwamba njia bora ya kutatua kero au matatizo yanayowakuta wananchi wakidai haki zao ni kwa kufuata taratibu za sheria,” alisema Nyanduga.
Alisema anawaomba viongozi wa watu wenye ulemavu wafuate taratibu hizo kufikisha hoja zao kwenye vyombo na mamlaka husika na siyo vinginevyo.
mwisho


  

Jumatatu, 17 Aprili 2017

tatizo la maji kwa wakazi wa Dar na Kibaha limetatuliwa na DAWASA

WAKAZI wa Wilaya za Kibaha mkoani Pwani Ubungo na Ulala mkoani Dar es Salaam wameondokana na adha ya upatikanaji wa maji baada ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kuwasha Mtambo mpya wa Ruvu juu juzi jioni.
Taarifa iliyotolewa na DAWASA imedai kuwa wamewasha mtambo huo baada ya kazi ya kuunganisha umeme wa kutosha kukamilika Aprili 15, mwaka huu.
DAWASA imedai kuwa kazi ya kuwasha pampu kubwa mpya katika Mtambo wa Ruvu Juu sasa imekamilika rasmi na  sasa mtambo huo utaanza kuzalisha lita milioni 196 kwa siku.
Taarifa hiyo imedai kuwa kazi mbalimbali zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma maji na ufungaji wa pampu mpya, maeneo mapya ya kusafisha maji, mitambo ya kuchuja maji, maeneo ya kuchuja matope na tenki kubwa la kuhifadhi maji safi. 

“Kituo kipya cha kusukuma maji safi na salama kilijengwa sambamba na mabomba makuu ya kusafirishia maji hayo yenye jumla ya urefu  wa kilomita 70 kutoka Mlandizi hadi Dar es salaam,” ilidai taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo pia ilidai kuwa tenki jipya lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 limejengwa eneo la Kibamba lenye muinuko na kutoka hapo maji yatashuka kwa nguvu ya mtiririko hadi katika matenki ya Kimara.

“Kazi iliyokuwa imebaki ni kuongeza nguvu ya umeme ili pampu hizo mpya ziweze kufanya kazi ambayo imekamilika, ukaguzi umefanyika na pampu moja baada ya nyingine ziliwashwa ili kuhakiksha mfumo mzima sasa unafanya kazi. 

“Hadi kufika juzi jioni Aprili17,  maji yalikuwa yanaingia katika matenki yote kwa kupitia mabomba mapya bila matatizo,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa mtambo huo wa maji wa Ruvu Juu sasa unapokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo kituo kidogo cha umeme Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55 MVA ambapo inawezesha pampu zote mpya zilizofungwa kuwashwa kwa wakati mmoja. 

“Mikataba ya jumla ya dola za Marekani 99 ya upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara, ujenzi wa tanki kubwa lenye ujazo wa lita million 10, ofisi kwa ajili ya shighuli za uendeshaji wa huduma na nyumba za watumishi wa mtambo ilisainiwa mwaka 2014.
Fedha hizo ilikuwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India,” ilidai taarifa hiyo. 

Kazi inayopewa msukumo mkubwa kwa sasa  ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji yaliyoongezeka ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na jitihada na uwekezaji uliofanywa na serikali yao.


Maeneo yanayonufaika ni pamoja na miji ya Kibaha, Mlandizi na baadhi ya Vitongoji vyake karika mkoa wa pwani na maeneo yote yaliyopo jorani na barabara ya Morogori yaani Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo,Malamba mawili, Msigani, Msakuzi, Makabe, Kibangu, External, Makuburi, Tabata, Segerea, Buguruni na Vingunguti.

Jumapili, 15 Januari 2017

E-CONNECT KUTATUA CHANGAMOTO ZA ELIMU


TAASISI ya Econnect imetengeneza mfumo wa kielektroniki wa kukusanya taarifa utakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali za elimu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Hashimu Magesa alisema mfumo huo utasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati zinazohusuidadi ya shule, idadi ya wanafunzi waliopo na walimu.
Alisema mfumo huo ambao tayari umefanyiwa majaribio katika Manispaa ya Ilala utatatua tatizo la mawasiliano kati ya utawala wa shule na wazazi.
“Kwa kutumia mfumo huu shule itakuwa na uwezo wa kutoa taarifa kwa mzazi au mlezi wa mwanafunzi husika ambaye atakuwa hajafika shuleni,” alisema Magesa.
Alisema kwa kutumia mtandao wadau wanaweza kujua mahali shule ilipo, mandhari yake, mawasiliano yake pamoja na historia fupi ya shule hiyo.
“Taarifa zitakazopatikana katika mfumo huo ni orodha ya wanafunzi kwa majina, jinsia, namba za simu za wazazi au walezi, idadi ya wanafunzi waliohama na kuhamiaidadi ya madawati na viti,idadi ya walimu kwa majina jinsia na masomo wanayofundishamuda alioanza kazi, daraja lake kiwangoo cha elimuna namba yake ya simu,” alisema Magesa.
Alisema vingine ni idadi ya walimu waliosataafu, walioko masomoni, idadi ya vyumba vya madarasa, mashimo ya vyoo, compyuta na vyumba vyake, maabara na nyumba za walimu, stoo, maji, umeme na eneo la shule kama limepimwa.

Aidha alitoa wito kwa serikali na wadau wa elimu nchini kuutumia mfumo huo kwa najaribio ndani ya mwaka ili kujiridhisha ufanisi wake.       

Alhamisi, 5 Januari 2017

WALIOUAWA KWA UJAMBAZI WALIPORA MIL.25 TAZARA


JESHI la polisi nchini limesema limebaini kuwa majambazi waliouawa katika tukio la unyanganyi katika jengo la kibiashara la White House Tower lililopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam,walihusika pia katika wizi wa  milioni 25  eneo la  Tazara katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simoni Sirro alisema baada ya kufanya tukio hilo la wizi katika eneo la Tazara, majambazi hao waliokuwa wanne, walipanga kwenda kufanya tukio lingine katika jengo la White House Tower lililopo Mikocheni. 
“Tukio hilo lilitokea jana(juzi),kwenye muda wa  saa 5:20, eneo la Mikocheni kwenye jengo la kibiashara la White Star Tower, tulipata taarifa kuna hao  majambazi ambao waliofanya tukio kwenye barabara ya Nyerere na kuchukua milioni 25,naamini walinogewa na hizo fedha wakaenda tena kufanya ujambazi.
“Baada ya kupata taarifa hiyo mapema,vijana wetu wakaenda kujipanga na walipoingia,askari wakapiga risasi ili majambazi wajisalimishe lakini nao walijibu, ndipo majibizano yalipoanza na  kuwauwa watatu na kukamata bastola moja aina ya SIG SAUER yenye namba P 229 ikiwa na risasi nne ndani ya magazine,”alisema Kamishna Sirro.
Alisema mmoja wa majambazi hao alifanikiwa kutoroka kwa kutumia usafiri wa pikipiki na jeshi hilo linaendelea kumtafuta.
Kamishna Sirro alisema wataendelea kupambana na suala la unyanganyi wa kutumia silaha katika jiji la Dar es Salaam.
Katika tukio lingine,Kamishna Sirro alisema wanamshikilia mkazi wa Tundwi Songani,kata ya Pemba Mnazi,Wilaya ya Kigamboni, Anwaz Ally kwa kukuta na bastola moja aina ya BARRETA ikiwa na risasi 23.
Alisema silaha hiyo ilipatikana baada ya kupekuliwa maungoni na kumkuta nayo ikiwa imefutwa namba huku akiwa hana kibali halali cha umiliki wa silaha hiyo.
“Mtuhumiwa huyo alipekuliwa katika chumba chake anachoishi ambapo alikutwa na risasi 23 za silaha ya BARRETA aliyokuwa ameificha ndani ya soksi.
“Mahojiano yanaendelea ili kubaini matumizi ya silaha hiyo, kwani kuna taarifa za kutumika kwa silaha hiyo kwenye matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,”alisema.


DC Awaonya mafataki

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga amewaonya wanaume wenye tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi kuwa hawatasalimika na mkono wa sheria.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi katika kata ya Mipeko, Sanga alisema wanaume wenye tabia hizo kama hawatabadilika wataishia magerezani.
“Nyinyi wanaume acheni kutamani wanafunzi na muwaogope sana maana sheria haitawaacha salama,” alisema.
Alisema katika mwaka huu anawaomba watoto wote wanaotakiwa kwenda shule wapelekwe ili kukinusuru na ujinga kizazi hicho.

“Watoto wanaotakiwa kwenda darasa la kwanza waende na waliofaulu kwenda kidato cha kwanza waende atakayeshindwa kumpeleka mwanaye shule hatua kali za sheria dhidi yake zitachukuliwa,” alisema Sanga.  

Jumanne, 3 Januari 2017

DC AHAMASISHA UTALII KUGAMBONI

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Hashimu Mgandilwa amewataka wananchi wa Dar es Salaam kuondoa dhana kuwa Fukwe zote za wilaya hiyo ni za kulipia.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufanya usafi katika maeneo ya fukwe, Mgandilwa alisema eneo la ufukwe wa Bahari ya Hindi ni   mali ya umma hivyo wasiogope kwenda kutembelea. 
Alisema kwa mujibu wa sheria eneo lililopo ndani ya mita 60 kutoka kingo za bahari ni mali ya umma na hakuna mwenye mamlaka nayo isipokuwa serikali.
“Changamoto iliyopo hapa ni ukosefu wa njia za kuingilia ambapo kwa sasa kuna njia zipo wazi na nitakutana na wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia namna ya kuweka njia zaidi za wananchi kuingia,” alisema Mgandilwa.
Aidha amewakikishia usalama wananchi na wageni watakaokwenda kutembelea katika fukwe hizo.
“Tumefanya usafi kama kuhamasisha utalii wa ndani na nje katika eneo hili kwa kuwa sasa ni sehemu ya utalii wa jiji la Dar es Salaam,” alisema Mgandilwa.
Mgandilwa alivitaja vivutio mbalimbali vilivyopo katika wilaya hiyo kuwa ni mbuyu wenye umbo la chupa ya shampeni, visiwa sita kikiwamo cha Sinda chenye mazalia ya kasa, jengo kale lililojengwa na Wajerumani. 
Aliwashukuru wanamuziki waliotoka nje na ndani ya nchi kushiriki usafi na kuhamasisha utalii wa Kigamboni.
 “Uwepo wenu hapa utaihamasisha jamii na kuitangaza Tanzania kim,ataifa,” alisema.
Naye mwanamuziki wa miondoko ya kufokafoka kutoka Marekani,Akua Naru alisema amefarijika kushiriki usafi wa fukwe na kuchangia kutoa elimu ya utalii kwa watanzania.
“Tutaitangaza vema nchi hii kwa kuwa na fukwe nzuri na utulivu mkubwa hasa kwa sisi wasanii kufanya shughuli zetu,” alisema Akua.
Naye Fred Maliki(Mkoloni) kutoka katika kundi la wagosi wa Kaya alisema amefurahi kuanza mwaka akiwa na jamii.
“Kushiriki kufanya usafi kwa vijana ina maana tunajitambua na tunaweza kuhasisha utalii kwa Wilayah ii,” alisema Mkoloni.

mwisho