WAZIRI wa Mambo
ya ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mwigulu Nchemba
leo bungeni amefunguka na kuomba radhi dhidi ya vitendo vya jeshi la polisi
kutumia nguvu kubwa kupambana na watu wenye ulemavu.
Mwigulu Nchemba
amekiri kuwa jeshi la polisi lilitumia nguvu kubwa mno kwa watu hao na kusema
serikali wamepokea jambo hilo na kuahidi kulifanyia kazi ili siku nyingine
lisijirudie.
"Kwanza
naomba niombe radhi kwa jambo hili na naomba salamu zangu ziwafikie watu wenye
ulemavu, ni kweli kwamba kwa kuzingatia hali yao jeshi la polisi lilitumia
nguvu kubwa, ila sisi kama serikali tumeshawasiliana na TAMISEMI na kuzungumza
nao juu ya mambo yao, lakini pia tumepokea jambo hili na tunalifanyia kazi ili
siku nyingine jambo hili lisijirudie" alisema Mwigulu Nchemba
Mnamo tarehe
16, Juni, 2017 jijini Dar es Salaam jeshi la polisi lilitumia nguvu kubwa
ikiwepo kuwapiga na kuwadhalilisha watu wenye ulemavu ambao walikuwa
wamejikusanya katika barabara ya Sokoine, Posta Jijini Dar es salaam ili kwenda
kumuona Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, kuwasilisha malalamiko dhidi ya askari
wa usalama wa barabarani kuwakamata na kuwazuia kuingia katika jiji. Lakini pia
walikuwa wakipigania haki yao ya kuwa na maeneo ya kuegesha vifaa vyao katikati
ya jiji.
CHAMA cha watu wenye ulemavu mkoa wa Dar es
Salaam(Chawata),wamelaani kitendo cha wao kunyanyaswa na kupigwa na Jeshi la Polisi
walipokuwa wakienda kwa mkurugenzi wa manispaa ya Ilala kupeleka kero zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Makamu mwenyekiti
wa chama hicho, Hamadi Komboza alisema katika tukio hilo la Juni
16, Mwaka huu, Mtaa wa Sokoine jijini Dar es Salaam walipigwa
na kupandishwa kwenye gari kama gunia.
“Tulikuwa tunaelekea
kwa Mkurugenzi wa Ilala tulipofika njiani askari walituvamia wakarusha mabomu
ya machozi na kutupiga huku wakiturusha kwenye gari lao (Difenda) kama gunia,”
alisema Komboza.
Alisema walipofikishwa kituo cha polisi waliwekwa mahabusu
kwa muda wa saa nane sehemu ambayo ni chafu bila kujali hali zao kwa kuwa
wengine hutumia mikono kutembea.
Aliongeza walipokuwa mahabusu walipigwa marungu huku
wakiombwa rushwa ya Sh. 10,000 kwa kila bajaji.
“Waliokataa mpaka sasa bajaji zao zinaendelea kushikiriwa
na jeshi hilo kituo cha kati na waliolipa waliruhusiwa kutoka,” Komboza.
Mmoja wa waathirika hao GFatuma Abdallah alisema
alidhalilishwa kwa kukamatwa na askari wa kiume huku nguo zake zikichanika na
kuacha maungo yake wazi.
Akizungumza huku aliwa analia Fatuma alisema alipofikishwa
kituo cha kati aliambiwa akaandikishwe kwa askari mwanamke wakati tayari
alikuwa amedhalilishwa.
“Nilipokuwa napakizwa ndani ya gari nguo zangu zilichanika
na kuacha maungo yangu wazi mbele ya wanaume,” alisema Fatuma.
Wakati huohuo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
imelaani tukio hilo walilofanyiwa walemavu hao.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa tume hiyo Bahame Nyanduga
ilisema THBUB imefuatilia tukio hilo kwa kuzungumza na viongozi wa walemavu na
mamlaka husika, hususani Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam na
kuelezwa kuwa mnamo Juni 16,Mwaka huu watu wenye ulemavu wapatao 200 wakiwa na
vyombo vya moto, vijulikanavyo kama “bajaji”, waliziba barabara ya Sokoine kwa
madai ya kutaka Mkurugenzi asikilize madai yao yahusuyo wenzao kukamatwa kwa
kuendesha vyombo vyao bila kufuata taratibu za sheria.
“Taarifa za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zilionyesha
askari wa Jeshi la Polisi wakiwapiga watu hao wenye ulemavu pamoja na kwamba
watu wenye ulemavu walikiuka taratibu za sheria ni wazi kwamba wakati wa kuzuia
uvunjifu huo wa sheria, kulikuwa na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi
ya watu hao wenye ulemavu wakati wakikamatwa na kuingizwa kwenye magari,”
alisema Nyanduga.
Alisema hakuna mtu anayepaswa kuvunjiwa haki zake wakati wa
kutekeleza sheria.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977)
Ibara ya 13 (6) (e) ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa
adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
Haki hizi pia zimeainishwa ndani ya mikataba mbalimbali ya
kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia,” alisema.
Alisema Tume inapenda kulikumbusha Jeshi la Polisi kwamba
kukimbilia kuwapiga raia kila wanapoonekana kukinzana na sheria ni matumizi
mabaya ya madaraka yao.
“Ni wajibu wa polisi kulinda usalama wa raia bila
kuwadhalilisha, kuwatesa na kuwapiga. Matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa
kutekeleza sheria ni uvunjifu wa sheria,” alisema Nyanduga.
Alisema pamoja na uvunjifu wa sheria uliotendwa na watu wenye ulemavu
kitendo cha kuwapiga bila kuwapa muda wa kutawanyika, au kutoa hoja za
malalamiko yao kupitia kwa wawakilishi wao ni kitendo cha kuwadhalilisha.
“Tume inatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuzingatia kanuni, sheria,
haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake
ya kila siku,” alisema.
Alisema ni vema kwa jeshi hilo kuwapatia mafunzo ya mara kwa
mara askari polisi na maafisa wake kuhusu haki za binadamu na misingi ya
utawala bora wakati wa kuratibu na kushughulikia masuala ya
maandamano na mikusanyiko ya raia.
“Polisi wahakikishe kuwa maafisa na askari wake hawatumii nguvu
kupita kiasi wawapo katika operesheni zinazohusu raia waliokusanyika kwa amani,
na hususan watu wenye ulemavu, ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“Tume inatoa wito kwa raia kwa ujumla, wakiwemo watu wenye
ulemavu, kwamba hamna mwananchi au mtu yeyote aliye juu ya sheria, na kwamba
njia bora ya kutatua kero au matatizo yanayowakuta wananchi wakidai haki zao ni
kwa kufuata taratibu za sheria,” alisema Nyanduga.
Alisema anawaomba viongozi wa watu wenye ulemavu wafuate
taratibu hizo kufikisha hoja zao kwenye vyombo na mamlaka husika na siyo
vinginevyo.
mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni