Jumanne, 20 Juni 2017

MEYA JACOB AZIDI KUSOTA MAHABUSU

MEYA wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob(Chadema) ameendelea kusota mahabusu baada ya kukamatwa na Jeshi la polisi jana.
Akizungumza na MTANZANIA Ofisa habari wa Chadema Tumaini Makene alisema taarifa walizonazo ni kwamba anashikiliwa na jeshi hilo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori.
Makene alisema mpaka sasa hawajui kosa analotuhumiwa Jacob japokuwa wameambiwa atakaa mahabusu kwa saa 48.
“Ni vizuri umwulize Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kuhusu kosa alilotenda Meya kwani hata sisi hatujui kinachoendelea,” alisema Makene.
Alisema viongozi wengine wa Chadema waliofika kituo cha polisi wilaya ya Ubungo walifukuzwa huku Katibu wa Chadema Wilaya hiyo, Justine Mollel, naye akikamatwa baada ya kwenda kumtembelea Jacob.
 Akizungumza na kituo cha runinga cha Azam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori alisema ameamua kumkamata Jacob kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kuwaleta wanachama wa Chadema wa kanda ya Pwani na kuwatembeza katika miradi ya maendeleo ya halmashauri.

Makori alisema kwa mujibu wa sheria na taratibu, mwenye mamlaka ya kukagua miradi ya maendeleo ni wajumbe wa kamati ya Maendeleo wa Halmashauri chini uenyekiti wa Meya ama Mwenyekiti wa Halmashauri.
“Hivyo kitendo cha Meya kutembelea miradi ya maendeleo bila madiwani wa kamati husika ni kuvunja sheria,na dawa yake ni kukaa ndani na kufunguliwa mashtaka,” alisema Makori.
Alisema ameagiza pia kukamatwa na kutiwa ndani kwa viongozi wengine waliokuwa katika msafara huo aliwamo Waziri Mkuu mstaafu na Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Pwani Frederick Sumaye kujibu ni kwanini walikwenda kutembelea miradi ya maendeleo bila idhini ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo.

“Kitendo cha Meya kutumia ukumbi na majengo ya halmashauri kukutana na viongozi wa Chadema ni kinyume na kanuni na sheria za utumishi wa umma,hivyo nimeagiza Meya huyo kukaa ndani kwa masaa 48 kabla ya kufunguliwa mashtaka,huku Sumaye na viongozi wengine wasakwe na kuwekwa ndani.

mwisho


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni