Jumatatu, 17 Aprili 2017

tatizo la maji kwa wakazi wa Dar na Kibaha limetatuliwa na DAWASA

WAKAZI wa Wilaya za Kibaha mkoani Pwani Ubungo na Ulala mkoani Dar es Salaam wameondokana na adha ya upatikanaji wa maji baada ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kuwasha Mtambo mpya wa Ruvu juu juzi jioni.
Taarifa iliyotolewa na DAWASA imedai kuwa wamewasha mtambo huo baada ya kazi ya kuunganisha umeme wa kutosha kukamilika Aprili 15, mwaka huu.
DAWASA imedai kuwa kazi ya kuwasha pampu kubwa mpya katika Mtambo wa Ruvu Juu sasa imekamilika rasmi na  sasa mtambo huo utaanza kuzalisha lita milioni 196 kwa siku.
Taarifa hiyo imedai kuwa kazi mbalimbali zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma maji na ufungaji wa pampu mpya, maeneo mapya ya kusafisha maji, mitambo ya kuchuja maji, maeneo ya kuchuja matope na tenki kubwa la kuhifadhi maji safi. 

“Kituo kipya cha kusukuma maji safi na salama kilijengwa sambamba na mabomba makuu ya kusafirishia maji hayo yenye jumla ya urefu  wa kilomita 70 kutoka Mlandizi hadi Dar es salaam,” ilidai taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo pia ilidai kuwa tenki jipya lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 limejengwa eneo la Kibamba lenye muinuko na kutoka hapo maji yatashuka kwa nguvu ya mtiririko hadi katika matenki ya Kimara.

“Kazi iliyokuwa imebaki ni kuongeza nguvu ya umeme ili pampu hizo mpya ziweze kufanya kazi ambayo imekamilika, ukaguzi umefanyika na pampu moja baada ya nyingine ziliwashwa ili kuhakiksha mfumo mzima sasa unafanya kazi. 

“Hadi kufika juzi jioni Aprili17,  maji yalikuwa yanaingia katika matenki yote kwa kupitia mabomba mapya bila matatizo,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa mtambo huo wa maji wa Ruvu Juu sasa unapokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo kituo kidogo cha umeme Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55 MVA ambapo inawezesha pampu zote mpya zilizofungwa kuwashwa kwa wakati mmoja. 

“Mikataba ya jumla ya dola za Marekani 99 ya upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara, ujenzi wa tanki kubwa lenye ujazo wa lita million 10, ofisi kwa ajili ya shighuli za uendeshaji wa huduma na nyumba za watumishi wa mtambo ilisainiwa mwaka 2014.
Fedha hizo ilikuwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India,” ilidai taarifa hiyo. 

Kazi inayopewa msukumo mkubwa kwa sasa  ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji yaliyoongezeka ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na jitihada na uwekezaji uliofanywa na serikali yao.


Maeneo yanayonufaika ni pamoja na miji ya Kibaha, Mlandizi na baadhi ya Vitongoji vyake karika mkoa wa pwani na maeneo yote yaliyopo jorani na barabara ya Morogori yaani Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo,Malamba mawili, Msigani, Msakuzi, Makabe, Kibangu, External, Makuburi, Tabata, Segerea, Buguruni na Vingunguti.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni