Na TUNU NASSOR
DAR ES SALAAM
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS ) imewaonya watu wanaotoa takwimu za Uchumi bila kuzingatia sheria ya Takwimu jambo ambalo linasababisha mkanganyiko katika jamii.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema hairuhusiwi kutoa takwimu hizo bila kuwa na kibali cha NBS.
Alisema NBS haikatazi mtu binafsi wala kikundi cha watu kukusanya takwimu isipokuwa kinachotakiwa ni kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kupata kibali kutoka katika Ofisi hiyo.
"Hatumnyimi mtu kibali cha kukusanya kuchakata na kusambaza takwimu isipokuwa kinachotakiwa ni kukusanya kulingana na misingi na sheria namba tisa ya Takwimu, " alisema Dk. Albina.
Alisema ukusanyaji huo unahitaji weledi wa hali ya juu chini ya kanuni 10 za Takwimu za Dunia.
" kinachonishangaza takwimu za serikali zinapotolewa mtu anasimama na kusema takwimu hizi si sahihi... Hii inatokea Tanzania pekee, hivyo asitokee mtu kupotosha takwimu za Uchumi " alisema Dk Albina.
Alisema takwimu za Uchumi ni muhimu kwa utekelezaji wa ajenda ya Afrika ya mwaka 2063.
"Katika ajenda hii kitu kimojawapo ni ukuaji wa uchumi wa bara hilo na haiwezi kufanikiwa bila kuwa na takwimu bora za Uchumi," alisema Dk Albina.
Naye Mkurugenzi wa Uchumi na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT), Johnson Nyella aliwataka wananchi wanaoshiriki katika ukusanyaji wa takwimu kutoa taarifa sahihi wanapojaza dodoso za takwimu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni