NAIBU
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Alias Kwandikwa amewataka wataalamu
wa ujenzi kuwa wazalendo kwa kuokoa gharama za ujenzi wa majengo mbalimbali ili
kulipunguzia mzigo taifa.
Akizungumza
katika ziara yake aliyoifanya juzi katika mradi wa ujenzi wa nyumba za Wakazi
wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam, Kwandikwa alisema uzalendo unahitajika
hasa katika kipindi hiki taifa likiwa katika mageuzi makubwa kiuchumi.
Alisema
wataalamu wanatakiwa kuwa wazalendo wakati wakisimamia miradi mbalimbali ya
ujenzi ili kuokoa fedha zitakazokwenda katika miradi mingine.
“Wakati
tunaangalia matumizi ya miradi ya serikali tujiulize kwenye familia zetu
tunafanya hivi?,” alisema Kwandikwa.
Alisema
wataalamu wa ujenzi waende kujifunza namna ya kupunguza gharama za ujenzi
kwa Wakala wa Ujenzi Tanzania(TBA) ambao
katika miradi yao wamepunguza kwa kiwango kikubwa.
“Endeleeni
kuokoa fedha kadri mnavyoweza baadaye mtatuambia kiasi mlichookoa ili zisaidie
katika miradi mingine ya kitaifa,” alisema Kwandikwa.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga alisema wataendelea kufanya
utafiti wa kushusha gharama za ujenzi ili kuongeza ushindani wa kibiashara.
Alisema
mradi wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota utagharimu Sh Bilioni 20 mpaka
kukamilika.
“Uzalendo
ndio unaotufikisha hapa kwani vijana tulionao wanatanguliza maslahi ya Taifa
mbele,” alisema Mwakalinga.
mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni