Jumanne, 14 Julai 2015

WANAOGAWA VIWANJA JANGWANI KUKIONA



MANISPAA ya Ilala imesema itawachukulia hatua watu wanaogawa viwanja kwa wamachinga katika eneo la jangwani kwa madai kuwa wameruhusiwa na uongozi kufanya hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Isaya Mngurumi alisema hawajamruhusu mtu yeyote kugawa viwanja bali waliwaruhusu kupanga chini bidhaa zao kama wanavyofanya katika mitaa ya kariakoo.
“Nimetuma timu kuwatafuta watu wanaogawa maeneo hayo kwani waliokimbilia huko si walengwa ni wajanja wachache tu,” alisema Mngurumi.
Alisema walikaa na uongozi wa manispaa ili kutafuta eneo la wafanyabiashara wadogo ndipo wakateua jangwani kuwa sehemu ya muda wakiwa bado wanaandaa masoko rasmi.
“Tumechagua jangwani upande wa kushoto wa barabara kama unaelekea kigogo kama sehemu ya muda kabla hatujaweka miundombinu ya vyoo wamevamia na kugawana bila ruksa ya manispaa,” alisema Mngurumi.
Alisema upande wa kulia wa barabara ni eneo la huduma za kijamii hasa uwanja wa mikutano ya hadhara na stendi ya mabasi yaendayo kasi.
Aidha alisema wako katika mkakati wa kujenga masoko ambayo yatawasaidia wafanyabiashara hao wadogo kuwa katika maeneo ya kudumu ya kufanyia shughuli zao.
Aliyataja masoko hayo kuwa ni Kisutu, Buguruni na Mchikichini ambapo wanaongea na wadau mbalimbali ili kupata mikopo kwa ajili ya ujenzi.
“Tumeingia mkataba na Benki ya TIB ili kujenga soko la kisutu kwa gharama ya sh. bilioni 11,” alisema.
mwisho  
         

TAHADHARI YATOLEWA KWA WANUNUA ARDHI



MKUU wa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani Abdallah Kihato amewatahadharisha watu wanaokwenda kununua ardhi katika wilaya yake hasa vijiji vinavyopakana na Ilala kuwa makini na matapeli wanaovamia maeneo hayo.
Akizungumza na Blog hii jana ofisini kwake, Kihato alisema kumeibuka malalamiko mengi hasa katika kijiji cha Tambani kuwepo matapeli wanaovamia mashamba yasiokuwa yao na kukata viwanja na kuuzia watu kwa madai kuwa eneo hilo liko Ilala.
“Ni muhimu kwa wanunuzi kufuata taratibu zote za ununuzi wa ardhi kwa kuwashirikisha viongozi wa kijiji ili kuthibitisha kama muuzaji ni eneo lake,” alisema kihato.
Alisema wanazo idara za ardhi kwa kila ngazi na upo utaratibu kwa mnunuzi na muuzaji kufika ofisi za kijiji kutambuliwa.
“Wakati mwingine watu wetu wanaingia katika migogoro hiyo kutokana na kuwa na haraka, wanakosa udadisi hawawezi hata kujiridhisha kwa majirani,” alisema Kihato.
Alisema wamekubaliana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuwa na kikao cha pamoja cha kamati za ulinzi na usalama kutokana na lawama nyingi za uvamizi kuripotiwa kutokea maeneo ya Wilaya hiyo.
“Migogoro mingi imetokana na kuharibiwa kwa ramani ya mwaka 1974 inayoonyesha mipaka ya wilaya hizi mbili,” alisema.
Alisema hati nyingi zimeandikwa kuwa kijiji cha Tambani kiko Ilala kitu ambacho si kweli hakuna mtaa huo katika wilaya hiyo.
Migogoro hiyo ya ardhi katika eneo hilo imesababisha watu wawili kupoteza maisha yao kutokana na mapigano kati ya wakazi na jamii ya Wakurya wanaodaiwa kuvamia maeneo ambayo si ya kwao.
mwisho

Jumatano, 8 Julai 2015

TAKATAKA SASA KUTENGENEZWA MBOLEA



HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imeingia makubaliano na Jiji la Humburg  la Uingereza kujenga mtambo wa kuchakata taka katika eneo la Mabwepande.
Ujenzi wa mtambo huo utagharimu    Sh bilioni 3.5.
Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda wakati wa uzinduzi wa soko la wafanyabiashara wadogo Sinza.
“Tayari tumepata kiwanda ambacho tutakitumia kuchakata taka za ‘organic’ ambazo zitatengenezwa mbolea ambayo tutaitumia kwa   matumizi mbalimbali.  Mradi huo tunatarajia utatengeneza ajira zaidi ya 1,000,” alisema Mwenda.
Akizindua soko hilo, alisema litasaidia kupunguza idadi ya wafanyabiashara wasiokuwa na maeneo maalum ikizingatiwa lina vizimba 512.
“Kunzia KESHO mnaruhusiwa kuanza kufanya biashara kwa sababu soko hili tumelijenga si mapambo tunataka kukabiliana na changamoto ya wafanyabiashara kutokuwa na maeneo maalum pamoja na ukosefu wa ajira.  Vipo vizimba 512 kwa maana hiyo tutapunguza kwa kiasi changamoto hii,” alisema.
Alisema manispaa hiyo pia imeanza ujenzi wa soko jingine kubwa eneo la Mburahati litakalogharimu Sh bilioni 1.8  kwa ajili ya   wafanyabiashara wa bidhaa ndogo ndogo.
  Meneja msimamizi wa soko hilo, Elichilia Mushi alisema   limejengwa kwa mfumo wa kisasa ili kuboresha huduma za wafanyabiashara hao.
“Tumepanga wafanyabiashara kulingana na aina ya bidhaa aliyonayo, lengo letu ni kuwavutia watu wengi zaidi na kuboresha huduma ya soko hili kuwa tofauti na mengine.  Pia tunazingatia suala la usafi,” alisema.
Alisema katika kutekeleza hilo zimewekwa sheria, kanuni na utarabu ambao utawasaidia kuboresha usafi ndani ya soko hilo.

MFUMUKO WA BEI WAENDELEA KUPAA



MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa mwezi juni, 2015 umeongezeka hadi asilimia 6.1 ukilinganisha na asilimia 5.3 kwa Mei mwaka huu.
Hii inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2015 ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Mei 2015.
          
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo alisema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya vyakula na zisizo za vyakula katika kipindi kilichoishia juni mwaka huu.

Alisema fahirisi (kipimo) za bei zimeongezeka hadi 158.12 Mei, 2015 kutoka 148.98 juni, 2014.

"Mfumuko wa bei umeendelea kuongezeka pia kutokana  na ongezeko la bei za mafuta hasa petrol kwa asilimia 5.2 na diesel kwa kwa asilimia 4.5.


"Mfano mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kama zilizoonyesha kuongezeka mwezi juni 2015 zikilinganishwa na bei za juni,2014 ni pamoja na mchele kwa asilimia 31.5, mahindi kwa asilimia 8.1,unga wa muhogo asilimia 3.7, nyama asilimia 3.1, samaki asilimia 12.0 na maharage asilimia 11.6. alisema Kwesigabo.

Kwesigabo alisema mfumuko wa bei kwa bidhaa  zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa kwa mfumuko wa bei mwezi juni 2015 zikilinganishwa na bei za juni 2014 na pamoja na bei za mavazi wanaume kwa asilimia 3.6, mavazi ya wanawake asilimia 2.6,vyakula kwenye migahawa kwa asilimia 3.5, na huduma za malazi kwa asilimia 3.1.


"Mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.2 mwezi juni, ukilinganisha na 0.4 kwa mwezi mei mwaka huu mwaka huu," alisema.

Alisema uwezo wa shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma umefikia shilingi 63 na senti 24 mwezi juni, mwaka huu kutoka Septemba, 2010 ikilinganishwa na shilingi 63 na senti 35 mwezi Mei mwaka huu.

Alisema hata hivyo mfumuko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ambapo kenya umeongezeka kwa asilimia 7.03 kutoka asilimia 6.87 mwezi mei 2015 na Uganda kubaki 4.90 kama ilivyokuwa mwezi mei mwaka huu.

Aidha amewaomba wananchi kutoa ushirikiano wa dhati kwa ofisi za takwimu za mikoa wakati wa ukusanyaji wa takwimu mbalimbali kwa lengo la kutoa taarifa zilizo sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.



Jumatatu, 6 Julai 2015

HUKUMU YA POLISI YAWAACHA NDUGU WA MLALAMIKAJI HOI



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mkuranga imemwachia huru askari polisi mwenye namba 3949 Cpl Innocent Haule, ambaye alikuwa akikabiliwa na shitaka la kumpiga na kumjeruhi Abdul Jongo kwa kutumia rungu.
Askari huyo aliachiwa huru juzi na mahakama hiyo kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake pasi kuacha shaka yoyote.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Agnes Mchome alikiri kuwepo mahakamani hapo ushahidi uliothibitisha kijana kupigwa na askari huyo.
“Kutokana na ushahidi wa daktari umeonyesha kweli alipigwa kichwani na kitu kizito na kumsababishia majeraha,” alisema Mchome.
Alisema katika ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo hakuna sehemu iliyoonyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na dhamira ya kumpiga na wala hakuna zana iliyoletwa mahakamani na kudaiwa kutumiwa na mshtakiwa.
“Upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa pasi kuacha shaka yoyote, hivyo mahakama inamwachia huru mshitakiwa,” alisema Hakimu huyo.
Awali akisoma shitaka hilo mbele ya hakimu mkazi, wakili wa serikali Debora John alidai kuwa mnamo disemba 26, 2010 katika eneo la Vikindu wilayani humo, mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kumpiga na rungu Abdu Jongo na kumsababishia jeraha kichwani.
Hukumu hiyo iliacha maswali mengi hasa kwa ndugu wa mlalamikaji kwa kuwa hakimu alikiri kuwepo ushahidi ulioonyesha dhahiri kupigwa.
mwisho