Alhamisi, 1 Desemba 2016

nicol wapata hasara ya bil.10


KAMPUNI ya uwekezaji ya wazawa(NICOL), imeanza uchunguzi wa hasara ya shilingi bilioni 10 iliyopata baada ya kufanya uwekezaji mbaya katika kampuni mbili tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NICOL, Gideon Kaunda alisema uchunguzi huo utafanyika ndani ya wiki mbili na baada ya ripoti kukabidhiwa watawafungulia kesi mahakamani wote waliosababisha hasara hiyo.
Alisema hadi kufikia Disemba 31, 2009, kampuni hiyo ilipata hasara hiyo kutokana na kuwekeza katika kampuni ambazo baadaye zilifilisiwa na benki zilizokuwa zikizidai.
“NICOL iliwekeza Dola za Marekani Milioni mbili(sawa na shilingi bilioni nne) katika kiwanda cha kutengeneza dawa kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro ambacho kilikuwa kimekopa katika benki ya Barclays na baada ya kushindwa kulipa deni hilo benki ilikitaifisha na kusababisha fedha hizi kupotea,” alisema Kaunda.
Alisema katika uwekezaji mwingine NICOL iliwekeza shilingi bilioni tatu katika kiwanda cha samaki kilichopo Mwanza na baadaye kukiongezea shilingi bilioni tatu ambacho nacho kilikopa fedha katika Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB).
“Baada ya uwekezaji wa mwaka mmoja kilishindwa kulipa deni hilo lililosababisha kufilisiwa na benki hiyo hivyo kupoteza fedha hizo,” alisema Kaunda.
Alisema pia wamebaini kuwa kutokana na uzembe ulifanyika katika kipindi cha uongozi wa Mwenyekiti wa zamani, Felix Mosha umesababisha kampuni tanzu ya Tanzania Meat Company ltd na ile ya Mwanza kufanya ubadhilifu.
“Mbali na kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha pia kodi za serikali na michango ya watumishi katika mifuko ya hifadhi za jamii haikuwa ikipelekwa hivyo kuongeza madeni,” alisema Kaunda.
Alisema katika uchunguzi huo pia wataangalia upya mikataba ya kampuni za nje zinazonunua nyama iliyoingiwa na TMC kutokana na kuwa na mapungufu mengi.
Aidha Kaunda alisema mapema mwakani wataanza kuwekeza tena katika soko la hisa baada ya kumalizika kwa migogoro ya uongozi iliyokuwapo awali.
mwisho






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni