KAMPUNI ya Platinum Credit Ltd kwa kushirikiana na
Hospitali ya mkoa ya Mwananyamala watatoa bure huduma za uchunguzi wa saratani
ya shingo ya kizazi kwa wanawake jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Lufunyo Gideon alisema
wameamua kufadhili uchunguzi huo ikiwa ni zawadi ya sikukuu ya Chrismas na
kurudisha kile walichokipata kwa jamii.
Alisema uchunguzi huo utafanyika katika hospitali ya
Mwananyamala iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kuanzia kesho hadi Disemba
21, mwaka huu.
“Tunawaomba wanawake wajitokeze kwa wingi katika kufanyiwa
uchunguzi ili waweze kutambua afya zao mapema na kupata ushauri,” alisema
Gideon.
Naye Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dk.Daniel
Nkungu alisema ni fursa kwa wanawake kujua afya zao ili kama wana ugonjwa huo
wapate matibabu mapema.
“Tatizo lililopo kwa sasa ni watu kuchelewa kugundua dalili
za awali za ugonjwa huo hivyo kugundulika ukiwa katika hatua mbaya ambayo mara
kadhaa umekisababisha vifo,” alisema Dk.Nkungu.
Alisema wahudumu wa hospitali hiyo wamejipanga vizuri
kuendesha uchunguzi huo hivyo wasiogope kwa kudhani kutakuwapo na foleni kubwa.
“Niwaombe wanawake wajitokeze kwa wingi kupima kwa kuwa
tumejipanga vizuri katika kuwapokea na kuwafanyia uchunguzi kwa haraka,”
alisema Dk.Nkungu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni