KAMPUNI ya Baga Investment imeshindwa kulipa kwa wakati posho za
baadhi ya wafanyakazi wake kwa madai ya kuidai Mamlaka ya Bandari Tanzani(TPA)
shilingi bilioni 2.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Jumbe Moshi, aliyasema hayo jana baada
ya kuwapo kwa malalamiko ya baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ambao
wanalipwa kwa siku kudai kutolipwa posho zao kwa siku 23.
Alisema ni zaidi ya miezi mitatu sasa TPA imeshindwa kuwalipa fedha
hizo hivyo kushindwa kulipa madeni yanayowakabili yakiwamo ya Benki.
“Kuchelewa kulipwa kwa wafanyakazi wetu kunatokana na TPA
kushindwa kuilipa kampuni kwa miezi mitatu jambo ambalo linarudisha nyuma
utendaji wa kampuni.
“Hali hii imetuweka katika
wakati mgumu kutokana na kampuni kudaiwa na baadhi ya Benki hali inayofanya tushindwe
kulipa na kujiendesha,” alisema Moshi.
Moshi alisema kuwa kampuni
hiyo iliingia mkataba na TPA wa kufanya kazi za ufundi wa kutengeneza maboti,
magari na udereva wa folk ambapo kampuni hiyo ilianza kazi hizo mwaka 2012.
“Tunakutana nao mara kwa
mara na wanatuomba radhi kwa kututaka tuvute subira mambo yakikaa sawa
watatulipa,”alisema Moshi.
Akizungumzia malalamiko ya wafanyakazi hao, Moshi alisema kampuni
hiyo imejitahidi kulipa posho za wiki iliyopita lakini juhudi zinaendelea
kufuatilia fedha wanazozidai TPA ili waweze kuwalipa fedha zao zote.
Aidha Moshi alisema wafanyakazi hao licha ya kulipwa kwa siku
lakini kutokana na makubaliano yao kila mmoja anapofanikiwa kuingia kazini
lazima anapelekewa makato yake NSSF.
Awali baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni hiyo ya Baga Investment,
walidai kuwa hawajalipwa posho hizo kwa siku 23 sasa.
Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka kuandikwa gazetini alisema
kila walipouliza walijibiwa kwamba chimbuko la kuchelewa huko kumesababishwa na
TPA ambayo haijailipa kampuni hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu.
Akizungumzia malalamiko hayo, Msemaji wa Bandari Janet Ruzangi
alisema madai hayo hayana ukweli kwa sababu kampuni hiyo inalipwa kwa wiki.
“Sijui mkataba wao na TPA unasemaje lakini mara nyingi malipo yao
yanakuwa kwa wiki au mwezi kwa sababu Baga Investment mpaka wameingia mkataba
na kuendesha shughuli hiyo inamaana walikuwa wanazo fedha za kutosha na siyo
mpaka walipwe,” alisema Ruzangi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni