Jumamosi, 31 Desemba 2016

MANJI AMTIKISA MWINYI

MGOGORO wa ardhi unaohusisha vijiji vinne vya Wilaya ya Mkuranga umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Filberto Sanga  kuwataka wakazi wa vijiji hivyo kukaa vikao vya kutayarisha mihutasari kumwomba Rais kufuta hati ya shamba ambalo limekuwa likitumiwa na wananchi kwa muda mrefu.
Mgogoro huo wa eneo la ekari 2472 unahusisha vijiji vinne vya kata mbili ya Tambani na Mipeko vyenye wakazi takribani 45,000 wakiwamo Rais Mstaafu Ali Hassani Mwinyi, Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba, Jaji Hamis Msumi, Rashidi Kawawa wakihusishwa kuvamia eneo la Kareem Manji na Entias Rajuani.


Sanga aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara kati ya wananchi na kamati ya usalama ya wilaya hiyo uliokuwa na lengo la kujadili shamba hilo linaloonekana kutishia usalama wa raia pamoja na mali zao.
Alisema viongozi wa vijiji hivyo wanapaswa kuhakikisha shughuli zote za upimaji ardhi katika vijiji hivyo vilivyodaiwa kumilikiwa na wamiliki hao zinasitishwa mpaka pale taratibu mbalimbali zitakapokamilishwa.

Alisema viongozi wa vijiji hivyo wanapaswa kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya maamuzi ya aina yoyote katika vijiji hivyo pasipo kupata ruhusa na kibali kutoka katika ofisi za Serikali.
 “Anzeni vikao kujadili suala hili na kuandika muhtasari kwa ngazi za juu kuomba kufutwa umiliki wa shamba hili,” alisema Sanga.
Sanga aliwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa wako katika mikono salama kuwa hakuna atakayewaondoa katika eneo hilo bila kufuata sheria.

“Mimi mkuu wa wilaya sina ardhi ya kuwaweka watu 45,000 wanaoondolewa hapa hivyo wakija waambieni waanzie kwangu… kwani kuwagusa wananchi bila kupitia viongozi huo ni uhuni,” ali
sema.
Aliwatahadhalisha wananchi kutouza holela ardhi jambo ambao husababisha migogoro kuwa mingi.
“Acheni kuuza ardhi, niwaombe wenyeviti wasaidieni wananchi wasiuze ardhi, na kama mtu anauza eneo lake uuzaji huo ufanyike hadharani kwa yeye na mnunuzi kusimama mbele ya wananchi ili mgogoro ukitokea wao ndio wawe wa kwanza kusuluhisha,” alisema Sanga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,Mhandisi Ally Munde

Naye mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega amemuomba Rais Dk. John Magufuli kufuta hatimiliki ya shamba hilo baada ya wawekezaji hao kushindwa kuliendeleza kwa zaidi ya miaka 50 na badala yake wapewe wananchi.
 Alisema shamba hilo lilitelekezwa kwa kipindi kirefu na wawekezaji hao, hali iliyopelekea wakazi wa kata ya Tambani pamoja na Mipeko kuyaendeleza kwa kufanya ujenzi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Ulega alisema Wakazi wa maeneo hayo waliweza kutafuta hati miliki ya maeneo waliyokuwa wanamiliki kwa kipindi chote na kushangazwa na kitendo cha wamiliki hao kuwataka kutoka katika maeneo yao kwa madai kuwa wamevamia eneo hilo.
Alisema wananchi wa vijiji vya Mlamleni, Luzando, Mwanambaya pamoja na Mipeko wamekuwa katika hali ya taharuki toka walipopewa notisi ya siku 21 ya kuwataka waondoke katika maeneo hayo ambayo wameyaendeleza kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
"Mi najua Rais wetu ni msikivu na anaweza kuzifanyia kazi kero za wananchi kwa wakati, na kero hii naamini atatilia mkazo kwa sababu wameshindwa kufanya shughuli za maendeleo kwa sasa kwa sababu ya watu wawili ,” alisema Ulega.
 Hata hivyo Ulega alimueleza Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kumuagiza Ofisa Ardhi Mteule
 alimweleza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutoruhusu kampuni ya 'Ardhi Plan' kupima maeneo ya wilaya hiyo kwani kama ataruhusu kampuni hiyo kufanya upimaji watapelekea kutokea kwa vurugu ambazo zinaweza kusababisha hali ya amani na utulivu kutokuwepo katika wilaya hiyo.
Naye Mbunge wa jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega ambaye pia ni muhanga alisema walikubwa na taharuki baada ya kupokea notisi ya siku 21 ikiwataka kuondoka katika eneo hilo.
“Tutafuata taratibu na sheria kufikisha kilio chetu kwa rais kumwomba alifutite shamba hilo kwa kuwa alishindwa kuliendeleza kwa muda wa zaidi ya miaka 50,” alisema Ulega.
Alimwomba DC kumwagiza Ofisa Ardhi mteule kumpa mmiliki huyo notisi ya siku 90 ya kusudio la kulifuta shamba hilo.
“Hakuna shamba hapa, ninaona nyumba za watu tu, hivi mimi DC mstaafu nitapata wapi tena fedha za kununua kiwanja,” alisema Ulega.
Akisimulia historia ya shamba hilo la Luzando, Diwani wa kata ya Tambani, Ally Mtamilwa alisema shamba hilo lenye hati namba 1281 lilimilikiwa na kampuni ya Mzungu iliyoitwa Seneda aliyekuwa akilima mkonge kabla ya kuhamishiwa kwa Akibaru February,1952.
“Mwaka 1978 Waziri Mkuu wa wakati huo hayati, Edward Sokoine alitangaza vijiji vya nguvu kazi vikiwamo Mwanadilatu, Gezaulole,Tegeta na katika shamba hilo ili walima kipindi hicho Akibaru aliondoka muda mrefu,” alisema Mtamilwa.
Alisema baada ya watu hao kupelekwa katika mashamba ya nguvu kazi waliendelea kuishi hapo kabla ya wanaodaiwa kuwa ni wajukuu wa Akibaru ambao ni Manji na Rajuani kufika katika eneo hilo kwa madai ya kutaka kuliendeleza wakiwa na hati ya mwaka 1952.
“Baada ya kukuta wananchi wakiendelea na kilimo waliridhia kutoa ekari 1472 kwa wananchi na wao kubakiwa na ekari 1,000 ambapo mwaka 1990 walifanya tathmini ya kuwaondoa wananchi waliokuwa ndani ya ekari walizobakiza na waliondoka bila kuwalipa,” alisema Mtamilwa.
Mtamilwa alisema Manji na mwenzake walituma kampuni ya upimaji wa ardhi iitwayo Ardhi Plan kupima viwanja katika eneo hilo.
“Waliwataka wenye maeneo ambayo hayajajengwa kulipwa kila ekari shilingi milioni moja na waliojenga kupimiwa viwanja na kulipa gharama za upimaji,” alisema Mtamilwa.
Aliongeza kuwa baada ya wananchi kutokuafiki suala hilo ndipo Manji na mwenzake kupitia mwanasheria wao waliandika notisi ya siku 21 kuwataka wakazi hao kuondoka kabla ya Disemba 19, 2016.
mwisho




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni