Jumatano, 30 Novemba 2016

watembea kilomita sita kutafuta huduma za afya



WAKAZI wa kijiji cha Kibamba, kata ya Mipeko wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 6 kufuata huduma za afya katika kijiji cha Mwanambaya.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Zahanati, Mtendaji wa kijiji hicho, Ally Madenge alisema kijiji hicho hakina huduma za afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungua njiani wakielekea kutafuta huduma hiyo.
“Hali ya huduma za afya kijijini hapa ni mbaya tunalazimika kuzifuata katika kijiji cha Mwanambaya na Mkuranga… huku tukiwa na wazee na watoto jambo ambalo ni hatari,” alisema Madenge.
Alisema kwa kuliona hilo wamelazimika kualika wadau mbalimbali kufanya harambee itakayosaidia ujenzi wa zahanati kijijini hapo.
Akiongoza harambee hiyo, Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema jumla ya shilingi milioni 98 zinahitajika katika ujenzi wa Zahanati hiyo. 
“Niwahakikishie wote watakaochangia hapa kuwa hatutamvumilia yeyote atakayefanya ubadhilifu wa fedha ama vitu vitakavyochangwa hapa,” alisema Ulega.
Ulega alimtaka Diwani wa kata ya Mipeko kusimamia kila hatua ya ujenzi huo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Niwaombe vijana wa kijijini hapa mjitolee katika ujenzi huu…hatuwezi kutafuta fedha za ujenzi na za kulipa vibarua hivyo ili kupunguza gharama hata mimi nitakuja kushiriki katika kambi ya ujenzi ili tuondokane na hili,” alisema Ulega.
mwisho


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni