CHAMA cha Kutetea Abiria(Chakua) kimeitaka serikali kuitafsiri
katika lugha ya kiswahili sheria ya kutetea abiria ya mwaka 2007 ili
kuwawezesha abiria wengi kujua haki na wajibu wao wawapo katika vyombo vya
usafiri.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Chakua,
Francis Mugassa alisema sheria hiyo iko katika lugha ya kiingereza jambo
linalosababisha abiria kukosa haki zao.
Alisema manyanyaso kwa abiria yameendelea kuwapo kutokana na
kukosa ufahamu wa sheria.
“Hivi ni wangapi wanajua kusoma kiingereza kwa kuwa sheria
hii haiwahusu wanaojua lugha hiyo bali ni watanzania wote hivyo tunaitaka
serikali kuitafsiri na kuisambaza nchini,” alisema Mugassa.
Aidha mugassa aliwaomba wadau mbalimbali kuunga mkono
juhudi zao katika kufikisha elimu kwa abiria.
“Tuna mkakati wa kupeleka elimu hii kwa wanafunzi mashuleni
na vyuoni hivyo juhudi za wa wadau zinahitajika kutusaidia kufikia azma hii,”
alisema Mugassa.
Katika hatua nyingine chakua imepokea msaada wa vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi
860,000 kutoka katika taasisi ya Teknolojia ya Kibaha(KIT).
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, mhasibu wa KIT,
Majid Ally alisema wanatambua mchango mkubwa wa Chakua katika jamii.
“Tumeona kazi zinazofanywa na chama hiki zinatupa matumaini
kwa kuwa kila mmoja wetu ni abiria lakini hatukujua haki na wajibu wetu, hivyo
tutoa msaada huu ili elimu iwafikie na wengine” alisema Ally.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni