“TANZANIA ni wabunifu na tunahitaji ubunifu kwa maendeleo
ya nchi lakini sio ubunifu huu wa ovyo,” hiyo ni kauli iliyotolewa kwa
masikitiko na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa na wilaya
alipokuwa Singida hivi karibuni.
Kauli hii ya Rais ilikuja baada ya baadhi ya watanzania
kujaribu kubadilisha matumizi ya vitu kuwa wanavyotaka wao.
Inawezekana hali ya
umaskini wa watu wengi ndio hupelekea baadhi ya watu kubuni njia ambazo
zinawasaidia kupata vitu vya gharama nafuu tofauti na uhalisia.
Akiwa Singida Rais anasikitishwa na tabia ya baadhi ya watu
wanaotumia vyandarua ambavyo vimegawiwa bure na Serikali kwa kila kaya nchini kwa
lengo la kutokomeza malaria na wao kubadilisha lengo lililokusudiwa kwa kufugia
kuku ama kuvulia samaki na wengine wakidiriki kujengea msalani.
“Watu wetu wa ajabu sana, tumegawa vyandarua
bure ili sote tuondokane na tatizo la malaria, lakini nasikitika ninavyosikia
kuwa wengine wanavitumia kufugia kuku.
“Kweli
Tanzania inahitaji ubunifu, lakini siyo ubunifu wa namna hii wa ovyo, tuache
kutumia vyandau kufugia kuku, tuvitumie kama ilivyokusudiwa.” Anasema Kikwete.
Vidonge vinavyotibu
maradhi mbalimbali
Dawa
za kuchochea uchungu kwa wajazito zikiwamo ‘misoprostol’ , ‘oxytocin’ , `Mifecon-Mkit’
zinazopatikana kiholela kwenye maduka ya dawa zimekuwa zikitumika kwa utoaji
mimba holela ambao hufanyika bila hofu yoyote.
Vidonge
hivyo hupanua shingo ya kizazi na kusababisha hewa kupita kwenye nyumba ya
uzazi na kubomoa ukuta wa tumbo la uzazi na kuharibu mimba.
Misoprost
-200 maarufu kama ‘miso’ ni vidonge vinavyodaiwa kubadilishwa matumizi yake ya
awali na kuwa dawa za kutolea mimba.Jijini Dar es Salaam matumizi ya dawa hii
yameongezeka kwa kutolea mimba hasa kwa baadhi ya wanafunzi na wafanyabiashara
za ngono.
Dawa
ya ‘mkit’ ambalo katika mahojiano na baadhi ya wanafunzi na wafanyabiashara ya
ngono wamekuwa walisifia kwa kudai inatoa mimba yenye umri wowote hata pale
‘miso’ inaposhindwa.
Kwa upande wa dawa ya ‘oxytocin’ watumiaji kuchomwa
sindano na kurudi nyumbani kusubiri mimba iharibike.
Tembe
nyingine zinazotumiwa ni ‘arzithromycin-500’ ambazo huingizwa sehemu za siri na
nyingine humezwa. kazi ya dawa hii si kuharibu mimba bali ni kutibu kama kifua,
magonjwa ya zinaa na kukausha vidonda vilivyotokana na kushambuliwa na vimelea.
Dawa
hizi hutumika kwa maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa maduka ya dawa,
wahudumu wa afya wasio na maadili na madaktari ‘vishoka’ mitaani.
Baadhi
ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wanakiri kuwa dawa hii inawasaidia lakini
wengine walisema si wakati wote kwani wapo waliodai waliitumia lakini badala ya
kuharibu iliikomaza mimba.
Mwanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Elizabeth
Joseph anasema yeye hajawahi kutumia vidonge hivyo lakini rafiki zake
hununua kwenye maduka ya dawa na kutumia kutoa mimba.
Matumizi
ya dawa ya malaria aina ya Metakelfin yamebadilishwa na sasa ni
kutengeneza kipodozi cha kurembesha nywele. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na
shirika lisilo la kiserikali la Envirocare linalojihusisha na mpango wa
kupunguza madhara yatokanayo na bidhaa za vipodozi kwa binadamu na mazingira,
umebaini dawa ya malaria ni aina mojawapo ya kemikali inayotumika
kienyeji katika kutengeneza kipodozi cha kurembesha nywele.
Imeripotiwa
kuwa baadhi ya wafugaji wa Mkoa wa Mbeya wanatumia dawa za kupunguza makali ya
UKIMWI (ARVs) kwa ajili ya kunenepesha mifugo yao.
Kwa mara
ya kwanza habari hizo zililipotiwa na Gazeti hili Toleo Na. 4990 Januari11 , 2010.
Dawa hizo zinadaiwa kukuza haraka na kunenepesha
mifugo kama Nguruwe, ng’ombe, kuku na wengineo.
Inadaiwa kuwa
dawa ya kutibu magonjwa ya mifupa indomethacin maarufu kama indocid
imekuwa ikitumika kama sumu ya kuulia panya.
“Indocid
ni sumu nzuri sana kwa panya, ukiichanganya na chakula panya wakila wanakufa,”
anasema Asia Mohammed ambaye ni mkazi wa Uzuri ,Manzese.
Mbolea za mazao
Baadhi
ya wafugaji wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, wanatumia mbolea ya kupandia na
kukuzia mazao kulishia mifugo yao kwa madai kuwa huinenepesha. Hayo yalielezwa na
Ofisa Tarafa ya Makame, Ibrahim Ole Mario alipokuwa akizungumza katika mafunzo
ya wenyeviti 25 wa vikundi vya wakulima wa Kiteto.
Kondom za kike
Huko Rukwa baadhi ya wanawake mkoani humo wamekuwa
wakitumia kondomu za kike kwa kuzivaa kama urembo wa bangili.
SARAFU mpya ya shilingi 500 inadaiwa kutumiwa na baadhi ya
watu ambao huinunua kwa Sh 2,500 na baadaye kuiyeyusha kwa ajili ya
kutengenezea mikufu ya fedha (silver).
Benki kuu ya Tanzania ilitoa ufafanuzi kuhusu uyeyushaji wa
sarafu hiyo. Apr
29, 2015 - 500 ni chuma na asilimia 6 ni
Nickel, ameeleza Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki katika Benki Kuu ya Tanzania,
Bw. Marcian Kobello.
“Hakuna kabisa madini ya
fedha katika sarafu ya sh. 500,” anasema Bw. Kobello na kuongeza kuwa
haitegemewi kwamba mfanyabiashara yeyote anaweza kununua sarafu hiyo kwa bei ya
juu kuliko thamani yake halisi.
Maji ya betri pamoja na jikJik na maji ya betri yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kutumiwa kama malighafi na wataalamu wa kutengeneza mikorogo inayotumiwa na baadhi ya wanawake na wanaume kuchubua ngozi za miili yao.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na shirika lisilo la kiserikali la Envirocare linalojihusisha na mpango wa kupunguza madhara yatokanayo na bidhaa za vipodozi kwa binadamu na mazingira, umebaini kuwa maji ya betri pamoja na dawa ya kuondoa madoa (jik) vinatumika katika uandaaji wa mikorogo.
Mtafiti kutoka shirika hilo Issa Sen’genge anasema Swali lilikuwa kama kuna vitu vinavyotumika katika kutengeneza mchanganyiko wa kupaka kwenye ngozi au nywele, waliohojiwa walikiri kuchanganya, Metakelfin, Jik, maji ya betri na kemikali nyingine.
Matumizi hayo ya hatari yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa watumiaji.
Watanzania wamekuwa wakibadili matumizi ya vitu mbalimbali hata kama ni hatari kwa afya zao.
