Jumapili, 4 Desemba 2016

QUALITY WAISOMA


KAMPUNI ya Quality Group inayomilikiwa na mfanyabiashara Yusuf Manji imeondolewa katika jengo iliyokuwa ikilikalia lililoko kiwanja namba 189/2 barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam kutokana na deni la malimbikizo ya ya pango la shilingi bilioni 13.
Kampuni hiyo inadaiwa kiasi hicho cha fedha kutokana na kulimbikiza deni hilo kwa miaka mingi tangu ipangishwe na mmiliki wa jengo hilo ambaye ni Mfuko wa Pensheni wa PSPF.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Operesheni wa kampuni ya Udalali ya Yono ambao ndio walipewa zabuni ya kuiondoa kampuni hiyo, Atukuzwe Muhugo alisema kazi hiyo imefanikiwa baada ya kutoa notisi ya masaa 24 kuitaka iondoke.
Alisema notisi hiyo iliisha alfajiri ya jana ndipo walipofika kuiondoa kwa nguvu lakini wafanyakazi walitii sheria na kuanza kutoa mali zao.
“Wafanyakazi wa Quality Group hawakuwa wajeuli wametii amri bila shuruti jambo lililoturahisishia kazi yetu,” alisema Atukuzwe.
Alisem jengo hilo litakuwa chini ya Yono mpaka hapo litakapokabidhiwa kwa PSPF.
Aliyataja ofisi zilizoondolewa kuwa ni Chief Exercutive officer of Quality Group Company LTD, Gaming Management Ltd, Q Consult Ltd, Quality Logistics Company Ltd na International Transit Investment Ltd .
Mmoja wa mahusika katika kampuni hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema hajajiandaa kuongea na wanahabari na hivyo kuwaomba wafike leo saa nane mchana ndipo ataongea.
“I don’t have suit, come tomorrow I will be ready to talk to you, how could I talk to you without wearing suit? Come tomorrow after lunch on 2  (siwezi kuzungumza bila kuvaa suti hivyo nawaomba mje kesho saa nane mchana ),” alisema.
Ilishuhudiwa magari aina ya Isuzu yenye namba za usajili T385 DAB na T620 DCC yakipakia vitu na kupeleka sehemu ambayo haikujulikana mara moja.
Uamuzi wa kuindoa Quality Group katika jengo hilo umetokana na kushindwa katika kesi namba 33 ya mwaka 2009 iliyofungua kampuni hiyo  katika mahakama kuu, Divisheni ya ardhi ikipinga kuondolewa.
Kesi hiyo ilimalizika Novemba 24, mwaka huu kwa mahakama kumpa haki mmiliki wa jengo hilo PSPF kutafuta dalali wa kumwondoa Quality Group.

Jaji aliyetoa hukumu hiyo aliamuru kuondolewa kwa Kampuni hiyo  na kuiacha PSPF kama mmiliki wa jengo hilo na ndipo Yono walipopewa zabuni ya kwenda kumwondoa.

Alhamisi, 1 Desemba 2016

ULEGA AAHIDI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

MBUNGE wa Mkuranga Abdallah Ulega(CCM), ameahidi kushughulikia malalamiko ya kukosekana kwa hudumu za afya katika Zahanati ya Mkamba.
Ulega aliahidi hayo wakati akizungumza na Halmashauri Kuu ya Kata ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwashukuru kwa kukisaidia chama hicho kupata ushindi.
Alisema  serikali ya CCM ni sikivu anahakika wahudumu watapatikana kwa ajili ya kuboresha huduma hiyo.
Alisema, baada ya kupokea taarifa hiyo anahakikisha anaifikisha katika sehemu husika kwa ajili ya kufanyiwa utekelezaji.
"Nitahakikisha ujumbe unawafikia wizarani kwa ajili kupatiwa wahudumu hao ambao watakuja kuondoa kero hii inayotukabili katika kata hii sitakubali kuona CCM inatiwa masingi kutokana na kushindwa kuwahudumia wananchi,"alisema Ulega.
Aidha Ulega aliahidi kuanza mara moja ujenzi wa barabara ya kutoka Kimanzichana kwenda katika kata hiyo ili kuondoa adha ya usafiri inayowakabili.
"Wazee wangu Mimi na diwani wenu tutafanya kila linalowezekana kutengeneza japo kwa dharura barabara hii ili iweze kutumika tukiwa tunasubiri fungi la serikali," alisema Ulega.
Kwa upande wake mkazi wa kata hiyo, Mikidadi Misomba alimweleza Ulega kuwa akiweza kutatua matatizo manne yanayowàkabili, wao kama wazee wa CCM watatembea kifua mbele.
"Mahitaji yetu ni manne ukitutimizia utakuwa umetuondolea aibu sisi wazee wa CCM ambayo ni kutuboreshea huduma za afya, barabara,maji na kutuondolea wavamizi wenye mifugo ambao wamekuwa wakituharibia mazao na kusababisha njaa," alisema Misomba.

nicol wapata hasara ya bil.10


KAMPUNI ya uwekezaji ya wazawa(NICOL), imeanza uchunguzi wa hasara ya shilingi bilioni 10 iliyopata baada ya kufanya uwekezaji mbaya katika kampuni mbili tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NICOL, Gideon Kaunda alisema uchunguzi huo utafanyika ndani ya wiki mbili na baada ya ripoti kukabidhiwa watawafungulia kesi mahakamani wote waliosababisha hasara hiyo.
Alisema hadi kufikia Disemba 31, 2009, kampuni hiyo ilipata hasara hiyo kutokana na kuwekeza katika kampuni ambazo baadaye zilifilisiwa na benki zilizokuwa zikizidai.
“NICOL iliwekeza Dola za Marekani Milioni mbili(sawa na shilingi bilioni nne) katika kiwanda cha kutengeneza dawa kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro ambacho kilikuwa kimekopa katika benki ya Barclays na baada ya kushindwa kulipa deni hilo benki ilikitaifisha na kusababisha fedha hizi kupotea,” alisema Kaunda.
Alisema katika uwekezaji mwingine NICOL iliwekeza shilingi bilioni tatu katika kiwanda cha samaki kilichopo Mwanza na baadaye kukiongezea shilingi bilioni tatu ambacho nacho kilikopa fedha katika Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB).
“Baada ya uwekezaji wa mwaka mmoja kilishindwa kulipa deni hilo lililosababisha kufilisiwa na benki hiyo hivyo kupoteza fedha hizo,” alisema Kaunda.
Alisema pia wamebaini kuwa kutokana na uzembe ulifanyika katika kipindi cha uongozi wa Mwenyekiti wa zamani, Felix Mosha umesababisha kampuni tanzu ya Tanzania Meat Company ltd na ile ya Mwanza kufanya ubadhilifu.
“Mbali na kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha pia kodi za serikali na michango ya watumishi katika mifuko ya hifadhi za jamii haikuwa ikipelekwa hivyo kuongeza madeni,” alisema Kaunda.
Alisema katika uchunguzi huo pia wataangalia upya mikataba ya kampuni za nje zinazonunua nyama iliyoingiwa na TMC kutokana na kuwa na mapungufu mengi.
Aidha Kaunda alisema mapema mwakani wataanza kuwekeza tena katika soko la hisa baada ya kumalizika kwa migogoro ya uongozi iliyokuwapo awali.
mwisho






Jumatano, 30 Novemba 2016

watembea kilomita sita kutafuta huduma za afya



WAKAZI wa kijiji cha Kibamba, kata ya Mipeko wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 6 kufuata huduma za afya katika kijiji cha Mwanambaya.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Zahanati, Mtendaji wa kijiji hicho, Ally Madenge alisema kijiji hicho hakina huduma za afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungua njiani wakielekea kutafuta huduma hiyo.
“Hali ya huduma za afya kijijini hapa ni mbaya tunalazimika kuzifuata katika kijiji cha Mwanambaya na Mkuranga… huku tukiwa na wazee na watoto jambo ambalo ni hatari,” alisema Madenge.
Alisema kwa kuliona hilo wamelazimika kualika wadau mbalimbali kufanya harambee itakayosaidia ujenzi wa zahanati kijijini hapo.
Akiongoza harambee hiyo, Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema jumla ya shilingi milioni 98 zinahitajika katika ujenzi wa Zahanati hiyo. 
“Niwahakikishie wote watakaochangia hapa kuwa hatutamvumilia yeyote atakayefanya ubadhilifu wa fedha ama vitu vitakavyochangwa hapa,” alisema Ulega.
Ulega alimtaka Diwani wa kata ya Mipeko kusimamia kila hatua ya ujenzi huo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Niwaombe vijana wa kijijini hapa mjitolee katika ujenzi huu…hatuwezi kutafuta fedha za ujenzi na za kulipa vibarua hivyo ili kupunguza gharama hata mimi nitakuja kushiriki katika kambi ya ujenzi ili tuondokane na hili,” alisema Ulega.
mwisho


Jumapili, 6 Novemba 2016

'SHERIA YA KUTETEA ABIRIA ITAFSIRIWE'

CHAMA cha Kutetea Abiria(Chakua) kimeitaka serikali kuitafsiri katika lugha ya kiswahili sheria ya kutetea abiria ya mwaka 2007 ili kuwawezesha abiria wengi kujua haki na wajibu wao wawapo katika vyombo vya usafiri.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Chakua, Francis Mugassa alisema sheria hiyo iko katika lugha ya kiingereza jambo linalosababisha abiria kukosa haki zao.
Alisema manyanyaso kwa abiria yameendelea kuwapo kutokana na kukosa ufahamu wa sheria.
“Hivi ni wangapi wanajua kusoma kiingereza kwa kuwa sheria hii haiwahusu wanaojua lugha hiyo bali ni watanzania wote hivyo tunaitaka serikali kuitafsiri na kuisambaza nchini,” alisema Mugassa.

Aidha mugassa aliwaomba wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zao katika kufikisha elimu kwa abiria.
“Tuna mkakati wa kupeleka elimu hii kwa wanafunzi mashuleni na vyuoni hivyo juhudi za wa wadau zinahitajika kutusaidia kufikia azma hii,” alisema Mugassa.
Katika hatua nyingine chakua imepokea msaada  wa vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi 860,000 kutoka katika taasisi ya Teknolojia ya Kibaha(KIT).
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, mhasibu wa KIT, Majid Ally alisema wanatambua mchango mkubwa wa Chakua katika jamii.

“Tumeona kazi zinazofanywa na chama hiki zinatupa matumaini kwa kuwa kila mmoja wetu ni abiria lakini hatukujua haki na wajibu wetu, hivyo tutoa msaada huu ili elimu iwafikie na wengine” alisema Ally.   

Jumatano, 28 Septemba 2016

majengo kale yahofiwa kupotea

IDADI ya majengokale katika jiji la Dar es Salaam yanahofiwa kupotea kutokana kukua kwa kasi kwa jiji hilo.
Akizungumza katika kongamano la urithi na uhifadhi wa majengo kale, Mkurugenzi wa Kituo cha Urithi na ubunifu Majengo Dar es Salaam, Aida Mulokozi alisema mpaka sasa majengokale yanayotambuliwa na serikali ni 25 tu.
Alisema sura ya jiji hilo imebadilika kutokana na ukuaji wa kasi hivyo kutishia urithi wa kihistoria wa majengokale.
“Leo Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji kumi yanayokuwa kwa haraka zaidi Duniani kutokana na shinikizo la uchumi maslahi ambayo yanayogongana na mamlaka dhaifu hivyo urithi wake uko katika hatari ya kupotea.
“Kasi ya maendeleo ni kubwa na kubasababisha mabadiliko ya haraka huku majengo mengi ya kihistoria kuvunjwa,” alisema Aida.
Alisema anaishauri serikali kuanzisha sheria itakayozuia majengo ya kale kubomolewa na kuachwa kama kumbukumbu.
“Kuna faida kubwa za majengo kale kama wizara ya ,aliasili na utalii wakiwekea mkazo wa kuyahifadhi na kuyatangaza,” alisema Aida.
Alisema moja ya faida kubwa ni kuongeza vivutio vya watalii ambao wengi hupenda kutembelea majengo ya kale.

“Majengo kale yamekuwa yakitumika vema kule Zanzibar kwani yamekuwa yakiingiza theruthi mbili ya pato la taifa,” alisema Aida.

Jumatano, 21 Septemba 2016

PORI LA MAJAMBAZI LAPEWA WANACHI



SERIKALI imetoa eneo la hifadhi la Pori la Vikindu lenye  ukubwa wa hekari 50, kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii za Kijiji cha Kipala Mpakani, kata ya Mwandege wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na serikali chini ya wizara ya Maliasili na Utalii na kuwa ni moja ya maeneo ambayo kwa vipindi tofauti yalitumiwa na wahalifu kama sehemu ya maficho yao kabla ya kudhibitiwa na jeshi la polisi siku chache zilizopita.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi pori hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne  Maghembe alisema serikali imeguswa na matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo zaidi elfu ya elfu kumi kukosa huduma muhimu za kijamii.
Alisema anashangaa jamii ya watu wanaohifadhi pori hilo kukosa zahanati, shule, soko na huduma nyingine za kijamii huku pori hilo likigeuka maficho ya wahalifu.
“Haiwezekani wanafunzi wanaoishi katika kijiji hiki kutembea kilomita saba kufuata shule vikindu huku wajawazito na wagonjwa kufuata huduma Mbagala,” alisema Maghembe.
Alisema baada ya kuona umuhimu wa huduma hizo ameamua kutoa eneo hilo litumuike kujenga miundombinu ya huduma za kijamii.
“Nawapa hili eneo lenye hekari 50 kwa ajili ya kujenga huduma hizo na kesho watakuja wataalamu kupima na kuainisha mipaka hivyo kuanzia sasa nalitoa kwenu,” alisema Pro. Maghembe.
Alisema atamwomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi, Williamu Lukuvi kutoa hati miliki ya eneo hilo kwa kijiji hicho.
“Baada ya miezi mitatu tutatangaza katika gazeti la serikali kuwa pori la Vikindu ni mali ya wananchi wa eneo hilo,” alisema.
Awali akitoa taarifa Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema wanafunzi wanaoishi kijijini hapo hutembea kilomita 7 kufuata shule iliyopo Kisenvule jambo linalosababisha wengi kushindwa kumaliza masomo kwa utoro.
“Huduma nyingi za jamii katika eneo hili zinapata katika kata ya Mbagala mkoa wa Dar es Salaam hivyo tunahitaji eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, Shule ya msingi na sekondari, kituo cha polisi, kituo cha mabasi na huduma nyingine za jamii,” alisema Ulega.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Amina Seif alisema eneo hilo lilikuwa hatari kwa waharifu kujificha hivyo watashirikiana na serikali kujenga miundombinu hiyo kwa haraka.
mwisho