Jumatano, 21 Septemba 2016

PORI LA MAJAMBAZI LAPEWA WANACHI



SERIKALI imetoa eneo la hifadhi la Pori la Vikindu lenye  ukubwa wa hekari 50, kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii za Kijiji cha Kipala Mpakani, kata ya Mwandege wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na serikali chini ya wizara ya Maliasili na Utalii na kuwa ni moja ya maeneo ambayo kwa vipindi tofauti yalitumiwa na wahalifu kama sehemu ya maficho yao kabla ya kudhibitiwa na jeshi la polisi siku chache zilizopita.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi pori hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne  Maghembe alisema serikali imeguswa na matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo zaidi elfu ya elfu kumi kukosa huduma muhimu za kijamii.
Alisema anashangaa jamii ya watu wanaohifadhi pori hilo kukosa zahanati, shule, soko na huduma nyingine za kijamii huku pori hilo likigeuka maficho ya wahalifu.
“Haiwezekani wanafunzi wanaoishi katika kijiji hiki kutembea kilomita saba kufuata shule vikindu huku wajawazito na wagonjwa kufuata huduma Mbagala,” alisema Maghembe.
Alisema baada ya kuona umuhimu wa huduma hizo ameamua kutoa eneo hilo litumuike kujenga miundombinu ya huduma za kijamii.
“Nawapa hili eneo lenye hekari 50 kwa ajili ya kujenga huduma hizo na kesho watakuja wataalamu kupima na kuainisha mipaka hivyo kuanzia sasa nalitoa kwenu,” alisema Pro. Maghembe.
Alisema atamwomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi, Williamu Lukuvi kutoa hati miliki ya eneo hilo kwa kijiji hicho.
“Baada ya miezi mitatu tutatangaza katika gazeti la serikali kuwa pori la Vikindu ni mali ya wananchi wa eneo hilo,” alisema.
Awali akitoa taarifa Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema wanafunzi wanaoishi kijijini hapo hutembea kilomita 7 kufuata shule iliyopo Kisenvule jambo linalosababisha wengi kushindwa kumaliza masomo kwa utoro.
“Huduma nyingi za jamii katika eneo hili zinapata katika kata ya Mbagala mkoa wa Dar es Salaam hivyo tunahitaji eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, Shule ya msingi na sekondari, kituo cha polisi, kituo cha mabasi na huduma nyingine za jamii,” alisema Ulega.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Amina Seif alisema eneo hilo lilikuwa hatari kwa waharifu kujificha hivyo watashirikiana na serikali kujenga miundombinu hiyo kwa haraka.
mwisho
   

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni