Jumatano, 27 Julai 2016

KINONDONI YATUMBUA SABA



BARAZA la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni limewachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake saba kwa kuwashusha vyeo na wengine kufukuzwa kazini baada ya makosa waliyokuwa wakituhumiwa kuthibitika.
Miongoni mwa watumishi waliochukuliwa hatua ni Mhandisi Mkuu wa Manispaa Hassan Mkuya ambaye ameshushwa cheo na sasa anakuwa mhandisi wa kawaida pamoja na mwenzake Ismail Mafita aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Barabara wa Manispaa.
Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) alisema hayo jana wakati alipokuwa akisoma taarifa ya Baraza la Madiwani ambalo ndilo lilipendekeza kuchukuliwa kwa hatua hizo.
“Desemba mwaka jana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitoa tuhuma dhidi ya watumishi wa manispaa hasa idara ya uhandisi, baadae Mkurugenzi naye alichukua hatua ya kuwasimamisha kazi watumishi 18 waliotuhumiwa na kuwafungulia mashauri ya kinidhamu.
“Kati ya hao 18, tisa walikuwa wa idara ya uhandisi, nane idara ya afya na mmoja idara ya fedha. Mhandisi Mkuu alikuwa akituhumiwa kwa makosa sita likiwamo la kutokufanya usanifu uliozingatia weledi hali iliyopelekea gharama za miradi kuzidi na kushindwa kutembelea eneo la miradi na wakandarasi kusababisha hasara za barabara ya Biafra, Journalism phase 2 na ile ya Maandazi,” alisema.
Alisema tuhuma nyingine ni kutotoa cheti cha ukamilishaji kazi, hatujui miradi kama imeshajengwa , kushindwa kusimamia miradi kwa kiwango cha kuridhisha, mfereji wa basihaya kuwekwa  karavati zisizokuwa na kiwango na kuongezeka kwa gharama za miradi ya batabara bila kuzingatia taratibu za kisheria za manunuzi ya umma.
“Kati ya tuhuma hizo zipo ambazo alikutwa na hatia moja kwa moja na nyingine hakukutwa na hatia hivyo ameadhibiwa kulinga na yale aliyokutwa na hatia moja kwa moja kama mfereji wa basihaya na barabara zilizojengwa chini ya kiwango,” alisema.
Alisisitiza adhabu hizo zimetolewa baada ya uchunguzi wa kina kufanyika kwa kushirikiana na vyombo vya dola, uchunguzi ulifanyika kwa kwenda katika maeneo husika ya miradi na watuhumiwa walipewa siku 14 za kujitetea.
Alisema hata hivyo adhabu hiyo waliyopewa haizuii watumishi hao kuchukuliwa hatua zaidi ikiwamo kufikishwa mahakamani.
“Kwa sababu kama hiyo ya fedha za miradi kuzidi, iligundulika kwamba walikubali baadhi ya wakandarasi kufanya kazi huku wakiwa hawajafuata utaratibu wa manunuzi na hadi sasa tunadaiwa Sh bilioni tano, sasa hii ni hasara na baada ya hatua hii tutakutana na hao wakandarasi ili tujiridhishe kama kweli kazi ilifanyika na tutatoa taarifa ya kitakachoamriwa,” alisema.
Pamoja na hayo, daktari mmoja wa Hosptali ya Palestina, Alphonse Chiwambo amepewa onyo kali baada ya kukutwa na kosa la kuomba rushwa ya Sh 30,000 kwa mama aliyekwenda kujifungua.
“Lakini kuna watumishi wanne wa idara ya afya tumewafukuza kazi kwa makosa ya utoro na rushwa na watumishi sita kati ya tisa wa idara ya uhandisi wamerejeshwa kazini baada ya kukutwa hawana hatia,” alisema.
Alisema pamoja na hayo baraza liliridhia kwapandisha vyeo watumishi 372, kubadilisha vyeo watumishi tisa na kuwathibitisha watumishi 206 ambao wamemaliza vipindi vyao vya majaribio na kuonekana kuwa wanafaa kufanya kazi katika utumishi wa umma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni