Jumatano, 30 Novemba 2016

watembea kilomita sita kutafuta huduma za afya



WAKAZI wa kijiji cha Kibamba, kata ya Mipeko wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 6 kufuata huduma za afya katika kijiji cha Mwanambaya.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Zahanati, Mtendaji wa kijiji hicho, Ally Madenge alisema kijiji hicho hakina huduma za afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungua njiani wakielekea kutafuta huduma hiyo.
“Hali ya huduma za afya kijijini hapa ni mbaya tunalazimika kuzifuata katika kijiji cha Mwanambaya na Mkuranga… huku tukiwa na wazee na watoto jambo ambalo ni hatari,” alisema Madenge.
Alisema kwa kuliona hilo wamelazimika kualika wadau mbalimbali kufanya harambee itakayosaidia ujenzi wa zahanati kijijini hapo.
Akiongoza harambee hiyo, Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema jumla ya shilingi milioni 98 zinahitajika katika ujenzi wa Zahanati hiyo. 
“Niwahakikishie wote watakaochangia hapa kuwa hatutamvumilia yeyote atakayefanya ubadhilifu wa fedha ama vitu vitakavyochangwa hapa,” alisema Ulega.
Ulega alimtaka Diwani wa kata ya Mipeko kusimamia kila hatua ya ujenzi huo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Niwaombe vijana wa kijijini hapa mjitolee katika ujenzi huu…hatuwezi kutafuta fedha za ujenzi na za kulipa vibarua hivyo ili kupunguza gharama hata mimi nitakuja kushiriki katika kambi ya ujenzi ili tuondokane na hili,” alisema Ulega.
mwisho


Jumapili, 6 Novemba 2016

'SHERIA YA KUTETEA ABIRIA ITAFSIRIWE'

CHAMA cha Kutetea Abiria(Chakua) kimeitaka serikali kuitafsiri katika lugha ya kiswahili sheria ya kutetea abiria ya mwaka 2007 ili kuwawezesha abiria wengi kujua haki na wajibu wao wawapo katika vyombo vya usafiri.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Chakua, Francis Mugassa alisema sheria hiyo iko katika lugha ya kiingereza jambo linalosababisha abiria kukosa haki zao.
Alisema manyanyaso kwa abiria yameendelea kuwapo kutokana na kukosa ufahamu wa sheria.
“Hivi ni wangapi wanajua kusoma kiingereza kwa kuwa sheria hii haiwahusu wanaojua lugha hiyo bali ni watanzania wote hivyo tunaitaka serikali kuitafsiri na kuisambaza nchini,” alisema Mugassa.

Aidha mugassa aliwaomba wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zao katika kufikisha elimu kwa abiria.
“Tuna mkakati wa kupeleka elimu hii kwa wanafunzi mashuleni na vyuoni hivyo juhudi za wa wadau zinahitajika kutusaidia kufikia azma hii,” alisema Mugassa.
Katika hatua nyingine chakua imepokea msaada  wa vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi 860,000 kutoka katika taasisi ya Teknolojia ya Kibaha(KIT).
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, mhasibu wa KIT, Majid Ally alisema wanatambua mchango mkubwa wa Chakua katika jamii.

“Tumeona kazi zinazofanywa na chama hiki zinatupa matumaini kwa kuwa kila mmoja wetu ni abiria lakini hatukujua haki na wajibu wetu, hivyo tutoa msaada huu ili elimu iwafikie na wengine” alisema Ally.   

Jumatano, 28 Septemba 2016

majengo kale yahofiwa kupotea

IDADI ya majengokale katika jiji la Dar es Salaam yanahofiwa kupotea kutokana kukua kwa kasi kwa jiji hilo.
Akizungumza katika kongamano la urithi na uhifadhi wa majengo kale, Mkurugenzi wa Kituo cha Urithi na ubunifu Majengo Dar es Salaam, Aida Mulokozi alisema mpaka sasa majengokale yanayotambuliwa na serikali ni 25 tu.
Alisema sura ya jiji hilo imebadilika kutokana na ukuaji wa kasi hivyo kutishia urithi wa kihistoria wa majengokale.
“Leo Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji kumi yanayokuwa kwa haraka zaidi Duniani kutokana na shinikizo la uchumi maslahi ambayo yanayogongana na mamlaka dhaifu hivyo urithi wake uko katika hatari ya kupotea.
“Kasi ya maendeleo ni kubwa na kubasababisha mabadiliko ya haraka huku majengo mengi ya kihistoria kuvunjwa,” alisema Aida.
Alisema anaishauri serikali kuanzisha sheria itakayozuia majengo ya kale kubomolewa na kuachwa kama kumbukumbu.
“Kuna faida kubwa za majengo kale kama wizara ya ,aliasili na utalii wakiwekea mkazo wa kuyahifadhi na kuyatangaza,” alisema Aida.
Alisema moja ya faida kubwa ni kuongeza vivutio vya watalii ambao wengi hupenda kutembelea majengo ya kale.

“Majengo kale yamekuwa yakitumika vema kule Zanzibar kwani yamekuwa yakiingiza theruthi mbili ya pato la taifa,” alisema Aida.

Jumatano, 21 Septemba 2016

PORI LA MAJAMBAZI LAPEWA WANACHI



SERIKALI imetoa eneo la hifadhi la Pori la Vikindu lenye  ukubwa wa hekari 50, kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii za Kijiji cha Kipala Mpakani, kata ya Mwandege wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na serikali chini ya wizara ya Maliasili na Utalii na kuwa ni moja ya maeneo ambayo kwa vipindi tofauti yalitumiwa na wahalifu kama sehemu ya maficho yao kabla ya kudhibitiwa na jeshi la polisi siku chache zilizopita.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi pori hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne  Maghembe alisema serikali imeguswa na matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo zaidi elfu ya elfu kumi kukosa huduma muhimu za kijamii.
Alisema anashangaa jamii ya watu wanaohifadhi pori hilo kukosa zahanati, shule, soko na huduma nyingine za kijamii huku pori hilo likigeuka maficho ya wahalifu.
“Haiwezekani wanafunzi wanaoishi katika kijiji hiki kutembea kilomita saba kufuata shule vikindu huku wajawazito na wagonjwa kufuata huduma Mbagala,” alisema Maghembe.
Alisema baada ya kuona umuhimu wa huduma hizo ameamua kutoa eneo hilo litumuike kujenga miundombinu ya huduma za kijamii.
“Nawapa hili eneo lenye hekari 50 kwa ajili ya kujenga huduma hizo na kesho watakuja wataalamu kupima na kuainisha mipaka hivyo kuanzia sasa nalitoa kwenu,” alisema Pro. Maghembe.
Alisema atamwomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi, Williamu Lukuvi kutoa hati miliki ya eneo hilo kwa kijiji hicho.
“Baada ya miezi mitatu tutatangaza katika gazeti la serikali kuwa pori la Vikindu ni mali ya wananchi wa eneo hilo,” alisema.
Awali akitoa taarifa Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema wanafunzi wanaoishi kijijini hapo hutembea kilomita 7 kufuata shule iliyopo Kisenvule jambo linalosababisha wengi kushindwa kumaliza masomo kwa utoro.
“Huduma nyingi za jamii katika eneo hili zinapata katika kata ya Mbagala mkoa wa Dar es Salaam hivyo tunahitaji eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, Shule ya msingi na sekondari, kituo cha polisi, kituo cha mabasi na huduma nyingine za jamii,” alisema Ulega.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Amina Seif alisema eneo hilo lilikuwa hatari kwa waharifu kujificha hivyo watashirikiana na serikali kujenga miundombinu hiyo kwa haraka.
mwisho
   

Jumatano, 27 Julai 2016

KINONDONI YATUMBUA SABA



BARAZA la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni limewachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake saba kwa kuwashusha vyeo na wengine kufukuzwa kazini baada ya makosa waliyokuwa wakituhumiwa kuthibitika.
Miongoni mwa watumishi waliochukuliwa hatua ni Mhandisi Mkuu wa Manispaa Hassan Mkuya ambaye ameshushwa cheo na sasa anakuwa mhandisi wa kawaida pamoja na mwenzake Ismail Mafita aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Barabara wa Manispaa.
Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) alisema hayo jana wakati alipokuwa akisoma taarifa ya Baraza la Madiwani ambalo ndilo lilipendekeza kuchukuliwa kwa hatua hizo.
“Desemba mwaka jana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitoa tuhuma dhidi ya watumishi wa manispaa hasa idara ya uhandisi, baadae Mkurugenzi naye alichukua hatua ya kuwasimamisha kazi watumishi 18 waliotuhumiwa na kuwafungulia mashauri ya kinidhamu.
“Kati ya hao 18, tisa walikuwa wa idara ya uhandisi, nane idara ya afya na mmoja idara ya fedha. Mhandisi Mkuu alikuwa akituhumiwa kwa makosa sita likiwamo la kutokufanya usanifu uliozingatia weledi hali iliyopelekea gharama za miradi kuzidi na kushindwa kutembelea eneo la miradi na wakandarasi kusababisha hasara za barabara ya Biafra, Journalism phase 2 na ile ya Maandazi,” alisema.
Alisema tuhuma nyingine ni kutotoa cheti cha ukamilishaji kazi, hatujui miradi kama imeshajengwa , kushindwa kusimamia miradi kwa kiwango cha kuridhisha, mfereji wa basihaya kuwekwa  karavati zisizokuwa na kiwango na kuongezeka kwa gharama za miradi ya batabara bila kuzingatia taratibu za kisheria za manunuzi ya umma.
“Kati ya tuhuma hizo zipo ambazo alikutwa na hatia moja kwa moja na nyingine hakukutwa na hatia hivyo ameadhibiwa kulinga na yale aliyokutwa na hatia moja kwa moja kama mfereji wa basihaya na barabara zilizojengwa chini ya kiwango,” alisema.
Alisisitiza adhabu hizo zimetolewa baada ya uchunguzi wa kina kufanyika kwa kushirikiana na vyombo vya dola, uchunguzi ulifanyika kwa kwenda katika maeneo husika ya miradi na watuhumiwa walipewa siku 14 za kujitetea.
Alisema hata hivyo adhabu hiyo waliyopewa haizuii watumishi hao kuchukuliwa hatua zaidi ikiwamo kufikishwa mahakamani.
“Kwa sababu kama hiyo ya fedha za miradi kuzidi, iligundulika kwamba walikubali baadhi ya wakandarasi kufanya kazi huku wakiwa hawajafuata utaratibu wa manunuzi na hadi sasa tunadaiwa Sh bilioni tano, sasa hii ni hasara na baada ya hatua hii tutakutana na hao wakandarasi ili tujiridhishe kama kweli kazi ilifanyika na tutatoa taarifa ya kitakachoamriwa,” alisema.
Pamoja na hayo, daktari mmoja wa Hosptali ya Palestina, Alphonse Chiwambo amepewa onyo kali baada ya kukutwa na kosa la kuomba rushwa ya Sh 30,000 kwa mama aliyekwenda kujifungua.
“Lakini kuna watumishi wanne wa idara ya afya tumewafukuza kazi kwa makosa ya utoro na rushwa na watumishi sita kati ya tisa wa idara ya uhandisi wamerejeshwa kazini baada ya kukutwa hawana hatia,” alisema.
Alisema pamoja na hayo baraza liliridhia kwapandisha vyeo watumishi 372, kubadilisha vyeo watumishi tisa na kuwathibitisha watumishi 206 ambao wamemaliza vipindi vyao vya majaribio na kuonekana kuwa wanafaa kufanya kazi katika utumishi wa umma.


Ijumaa, 22 Julai 2016

MIL.463 kukarabati Stand ya Ubungo



HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kutumia shilingi milioni 463 katika kukifanyia ukarabati kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo.
Akizungumza na FICHUA, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema jiji limepitisha mpango wa manunuzi ambao utaruhusu kuanza kwa ukarabati huo.
Alisema ukarabati huo utahusisha ujenzi wa mifumo ya maegesho, vyoo, milango ya kuingilia na taa.
“Jana (Juzi)tumepitisha mpango wa manunuzi ambao tuna mamlaka ya kuanza kazi, na inawezekana kesho(leo) mkaona zabuni zikitangazwa katika gazeti la serikali ambazo zitajumuisha ujenzi wa maegesho, ” alisema Mwita.
Alisema sambamba na hilo wanatarajia kuanza kwa ujenzi wa vituo vitatu vya mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi katika maeneo tofauti.
“Ujenzi huo utakaofanyika kwa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi katika maeneo ya Mbezi Luisi kwa mabasi ya mikoa ya kati na magharibi, Boko Basihaya kwa mikoa ya kaskazini na Kongowe kwa mikoa ya kusini.
Mwita alisema kupanda kwa viingilio vya wasindikizaji katika stand ya ubungo kutoka shilingi 200 hadi 300 kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha.
“Bei hizi zilikuwapo tangu mwaka 1998 ni tofauti na sasa, na Faida za kuongezwa kwa shilingi mia matunda yake yataonekana baadaye kwa kupata huduma zilizo bora,” alisema Mwita.
Aidha alisema wako katika mikakati ya kuweka kulipanga upya jiji la Dar es Salaam ambapo tayari wameanza kufanya uchambuzi.
“Kwa sasa wanaendelea kufanya tathmini kwa kutumia picha za ndege hivyo kufikia Septemba, Mwaka huu tunaweza kutoa ‘masterplan’,” alisema Mwita.
                                              
mwisho

  
   

MSONDO FAMILY DAY JUMAPILI



BENDI ya Msondo Ngoma imewataka mashabiki na wapenzi wa muziki wa dansi nchini kujitokeza katika tamasha la siku ya Familia litakalofanyika Julai 31, mwaka huu katika ukumbi wa DDC Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti aliliambia DIMBA kuwa lengo ni kuwa na wasaa wa kukutana na mashabiki wao ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo na kuichangia bendi hiyo ili iweze kufanya vema.
Alisema onesho hilo litawakumbusha mashabiki kuwa bendi ipo na inaendelea kufanyakazi vizuri.
“Katika onesho hilo tunatarajia kutambulisha nyimbo mpya mbili ambazo ni ‘Masimango’ ukiwa ni utunzi wa Edo Sanga na ‘maana ya ndoa iko wapi’ ukiotungwa na mwanamuziki Athumani Kambi,” alisema Kibiriti.
mwisho