Jumapili, 15 Januari 2017

E-CONNECT KUTATUA CHANGAMOTO ZA ELIMU


TAASISI ya Econnect imetengeneza mfumo wa kielektroniki wa kukusanya taarifa utakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali za elimu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Hashimu Magesa alisema mfumo huo utasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati zinazohusuidadi ya shule, idadi ya wanafunzi waliopo na walimu.
Alisema mfumo huo ambao tayari umefanyiwa majaribio katika Manispaa ya Ilala utatatua tatizo la mawasiliano kati ya utawala wa shule na wazazi.
“Kwa kutumia mfumo huu shule itakuwa na uwezo wa kutoa taarifa kwa mzazi au mlezi wa mwanafunzi husika ambaye atakuwa hajafika shuleni,” alisema Magesa.
Alisema kwa kutumia mtandao wadau wanaweza kujua mahali shule ilipo, mandhari yake, mawasiliano yake pamoja na historia fupi ya shule hiyo.
“Taarifa zitakazopatikana katika mfumo huo ni orodha ya wanafunzi kwa majina, jinsia, namba za simu za wazazi au walezi, idadi ya wanafunzi waliohama na kuhamiaidadi ya madawati na viti,idadi ya walimu kwa majina jinsia na masomo wanayofundishamuda alioanza kazi, daraja lake kiwangoo cha elimuna namba yake ya simu,” alisema Magesa.
Alisema vingine ni idadi ya walimu waliosataafu, walioko masomoni, idadi ya vyumba vya madarasa, mashimo ya vyoo, compyuta na vyumba vyake, maabara na nyumba za walimu, stoo, maji, umeme na eneo la shule kama limepimwa.

Aidha alitoa wito kwa serikali na wadau wa elimu nchini kuutumia mfumo huo kwa najaribio ndani ya mwaka ili kujiridhisha ufanisi wake.       

Alhamisi, 5 Januari 2017

WALIOUAWA KWA UJAMBAZI WALIPORA MIL.25 TAZARA


JESHI la polisi nchini limesema limebaini kuwa majambazi waliouawa katika tukio la unyanganyi katika jengo la kibiashara la White House Tower lililopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam,walihusika pia katika wizi wa  milioni 25  eneo la  Tazara katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simoni Sirro alisema baada ya kufanya tukio hilo la wizi katika eneo la Tazara, majambazi hao waliokuwa wanne, walipanga kwenda kufanya tukio lingine katika jengo la White House Tower lililopo Mikocheni. 
“Tukio hilo lilitokea jana(juzi),kwenye muda wa  saa 5:20, eneo la Mikocheni kwenye jengo la kibiashara la White Star Tower, tulipata taarifa kuna hao  majambazi ambao waliofanya tukio kwenye barabara ya Nyerere na kuchukua milioni 25,naamini walinogewa na hizo fedha wakaenda tena kufanya ujambazi.
“Baada ya kupata taarifa hiyo mapema,vijana wetu wakaenda kujipanga na walipoingia,askari wakapiga risasi ili majambazi wajisalimishe lakini nao walijibu, ndipo majibizano yalipoanza na  kuwauwa watatu na kukamata bastola moja aina ya SIG SAUER yenye namba P 229 ikiwa na risasi nne ndani ya magazine,”alisema Kamishna Sirro.
Alisema mmoja wa majambazi hao alifanikiwa kutoroka kwa kutumia usafiri wa pikipiki na jeshi hilo linaendelea kumtafuta.
Kamishna Sirro alisema wataendelea kupambana na suala la unyanganyi wa kutumia silaha katika jiji la Dar es Salaam.
Katika tukio lingine,Kamishna Sirro alisema wanamshikilia mkazi wa Tundwi Songani,kata ya Pemba Mnazi,Wilaya ya Kigamboni, Anwaz Ally kwa kukuta na bastola moja aina ya BARRETA ikiwa na risasi 23.
Alisema silaha hiyo ilipatikana baada ya kupekuliwa maungoni na kumkuta nayo ikiwa imefutwa namba huku akiwa hana kibali halali cha umiliki wa silaha hiyo.
“Mtuhumiwa huyo alipekuliwa katika chumba chake anachoishi ambapo alikutwa na risasi 23 za silaha ya BARRETA aliyokuwa ameificha ndani ya soksi.
“Mahojiano yanaendelea ili kubaini matumizi ya silaha hiyo, kwani kuna taarifa za kutumika kwa silaha hiyo kwenye matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,”alisema.


DC Awaonya mafataki

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga amewaonya wanaume wenye tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi kuwa hawatasalimika na mkono wa sheria.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi katika kata ya Mipeko, Sanga alisema wanaume wenye tabia hizo kama hawatabadilika wataishia magerezani.
“Nyinyi wanaume acheni kutamani wanafunzi na muwaogope sana maana sheria haitawaacha salama,” alisema.
Alisema katika mwaka huu anawaomba watoto wote wanaotakiwa kwenda shule wapelekwe ili kukinusuru na ujinga kizazi hicho.

“Watoto wanaotakiwa kwenda darasa la kwanza waende na waliofaulu kwenda kidato cha kwanza waende atakayeshindwa kumpeleka mwanaye shule hatua kali za sheria dhidi yake zitachukuliwa,” alisema Sanga.  

Jumanne, 3 Januari 2017

DC AHAMASISHA UTALII KUGAMBONI

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Hashimu Mgandilwa amewataka wananchi wa Dar es Salaam kuondoa dhana kuwa Fukwe zote za wilaya hiyo ni za kulipia.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufanya usafi katika maeneo ya fukwe, Mgandilwa alisema eneo la ufukwe wa Bahari ya Hindi ni   mali ya umma hivyo wasiogope kwenda kutembelea. 
Alisema kwa mujibu wa sheria eneo lililopo ndani ya mita 60 kutoka kingo za bahari ni mali ya umma na hakuna mwenye mamlaka nayo isipokuwa serikali.
“Changamoto iliyopo hapa ni ukosefu wa njia za kuingilia ambapo kwa sasa kuna njia zipo wazi na nitakutana na wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia namna ya kuweka njia zaidi za wananchi kuingia,” alisema Mgandilwa.
Aidha amewakikishia usalama wananchi na wageni watakaokwenda kutembelea katika fukwe hizo.
“Tumefanya usafi kama kuhamasisha utalii wa ndani na nje katika eneo hili kwa kuwa sasa ni sehemu ya utalii wa jiji la Dar es Salaam,” alisema Mgandilwa.
Mgandilwa alivitaja vivutio mbalimbali vilivyopo katika wilaya hiyo kuwa ni mbuyu wenye umbo la chupa ya shampeni, visiwa sita kikiwamo cha Sinda chenye mazalia ya kasa, jengo kale lililojengwa na Wajerumani. 
Aliwashukuru wanamuziki waliotoka nje na ndani ya nchi kushiriki usafi na kuhamasisha utalii wa Kigamboni.
 “Uwepo wenu hapa utaihamasisha jamii na kuitangaza Tanzania kim,ataifa,” alisema.
Naye mwanamuziki wa miondoko ya kufokafoka kutoka Marekani,Akua Naru alisema amefarijika kushiriki usafi wa fukwe na kuchangia kutoa elimu ya utalii kwa watanzania.
“Tutaitangaza vema nchi hii kwa kuwa na fukwe nzuri na utulivu mkubwa hasa kwa sisi wasanii kufanya shughuli zetu,” alisema Akua.
Naye Fred Maliki(Mkoloni) kutoka katika kundi la wagosi wa Kaya alisema amefurahi kuanza mwaka akiwa na jamii.
“Kushiriki kufanya usafi kwa vijana ina maana tunajitambua na tunaweza kuhasisha utalii kwa Wilayah ii,” alisema Mkoloni.

mwisho