WAANDISHI
wa habari za mahakama nchini wameitaka mahakama kuandaa mazingira rafiki na sehemu
bora zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Akisoma
mapendekezo yaliyotolewa katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari
za mahakamani yaliyomalizika juzi, mmoja wa waandishi hao, Kulwa Mzee alisema wamekuwa
wakipata shida kupata sehemu ya kufanyia kazi zao hivyo kuitaka mahakama
kuandaa eneo hilo.
Alisema
ili kuboresha kuanzishwe mtandao wa waandishi na mahakama utakaosaidia
upatikanaji wa vitu muhimu kama takwimu, hukumu na usajili.
“Tunaziomba
Mahakama na Baraza la Habari Nchini(MCT) kuanzisha mafunzo endelevu ya waandishi
wa habari za mahakama ambayo yatashirikisha pia wahariri ili kuepuka makosa
kutokana na kutojua lugha za kimahakama,” alisema Kulwa.
Alisema
katika mapendekezo yao wamewataka Majaji na Mahakimu kutoa nakala za hukumu
pamoja na muhtasari kwa waandishi.
“Tunapendekeza
Mahakama na MCT kushawishi uanzishwaji wa madawati ya habari za mahakamani katika
vyumba vya habari ili kuwasaidia waandishi,” alisema Kulwa.
Kwa
upande wake Jaji Kiongozi, Shaban Lila alisema mafunzo hayo ni muhimu katika
kujenga mahusiano mazuri kati ya vyombo vya habari na mahakama.
Alisema
mhimili wa Mahakama uliwahi kupewa tuzo ya kufuli lililofungwa kuonyesha kuwa
walikuwa wagumu kutoa habari zao.
“Tunahitajiana,
wote tunafanya kazi kwa ajili ya jamii hivyo tushirikiane kwa kutoa habari
zilizosahihi, fasaha na kwa wakati,”alisema Lila.
Alisema
Mahakama imekuwa ikilalamikia uandishi wenye mapungufu huku waandishi
wakilalamika ugumu wa kupata habari.
“Waandishi
wamekuwa wakitumia maneno ya kuhukumu katika uandishi wao kabla kesi
haijatolewa hukumu na kusababisha usumbufu kwa jamii walioaminishwa tofauti na
hukumu iliyotolewa,” alisema Lila.
Jaji
Lila alisema si kwamba mahakama wanakwepa kuambiwa kasoro zao bali ziwakilishwe
kwa lugha za staha bila kuwashambulia majaji na mahakimu.
“Hakuna
Jaji anayeweza kuamua anavyotaka yeye, anaamua kutokana na sheria na ushahidi,
kama kuna tatizo ni upungufu wa sheria husika na si Jaji,” alisema Jaji Lila.
Mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni