Jumatatu, 16 Novemba 2015

bomoa bomoa kurasini wakazi hali tete



WAKAZI wa Kurasini Shimo la Udongo wamejikuta wakikosa makazi baada ya nyumba 45 walizokuwa wakiishi kubomolewa ili kupisha upanuzi wa bandari na ujenzi wa maegesho ya malori.
Ubomoaji huo ulifanyika jana, saa moja asubuhi hali iliyosababisha wananchi wa eneo hilo kujikuta wakitawaliwa na vilio, simanzi kutokana na kuharibiwa kwa mali zao zilikuwemo ndani ya nyumba hizo.
Wakati kazi hiyo ikiendelea polisi walikuwa wameimarisha ulinzi katika eneo hilo, wakishirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambao walikuwa na jukumu la kuzuia kutokea kwa tatizo la umeme kwa nyumba zilizokuwa na nishati hiyo.
Bomoabomoa hiyo iliwanufaisha vibaka waliokuwa wakivamia na kupora vitu wakati kazi ya ubomoaji ilipokuwa ikiendelea huku vijana wengine walinufaika na ajira ya uokoaji kwa kulinda mali zao.
Akizungumza na FICHUA Diwani aliyemaliza muda wake, Wilfred Kimati alisema, ubomoaji huo umefanyika kinyume cha sheria kwakuwa wananchi bado walikuwa wakidai malipo yao.
Alisema eneo hilo lilifanyiwa tathimini na mthamini kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi ambapo wananchi wa eneo hilo walikuwa 161 na walitakiwa kulipwa fidia ya Sh. Bilioni 16.
Kimati alisema eneo hilo limechukuliwa na mwekezaji kampuni ya Easy Netwotk Solution ambao walikubali kulipa fidia stahili na eneo hilo litumiwe kwa maegesho ya magari makubwa.
“Tumebaini Manispaa ya Temeke ina vitabu viwili vya tathmini ambapo malipo yaliyofanywa yakionyesha kuwepo makato makubwa kwenye fidia hali iliyosababisha baadhi ya wenye nyumba 64 kufungua mashauri mahakamani kugomea fidia hiyo wakidai walipwe iliyokuwa imepangwa na wizara,”alisema Kimati.
Kimati alisema eneo hilo lina nyumba 165 ambapo nyumba 45 ndiyo zimebomolewa zikiwemo zilizokuwa kwenye zuio la Mahakama jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria.
Kwa upande wake, mwananchi James Mwakalobo alilalamikia nyumba yake kubomolewa wakati ikiwa na zuio la mahakama.
Naye, Mwenyekiti wa mtaa huo, Rajabu Nkumilwa alisema, manispaa hiyo imekiuka kwakuwa wananchi wake walikuwa na madai ya msingi.
Alisema wananchi wanalia na upunjwaji wa fidia kwakuwa wengine wamelipwa kiwango cha chini Sh. Milioni 27 hadi Mil.188 wakati nyumba hizo zilikuwa na hatimiliki na thamani kubwa.
“Wananchi walikubali uhakiki wa malipo ya fidia ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi lakini cha ajabu manispaa ya Temeke nao wameingilia kati na kupunja fidia za wananchi hawa,”alisema Nkumilwa.
Akijibu hoja hizo Mkurugenzi wa Temeke, Photidas Kagimbo alisema ubumoaji wa eneo hilo ulikuwa sahihi kwakuwa notisi ilianzia Juni 10 mwaka huu na ilikuwa ya siku 60 na hadi jana wanafanya ubomoaji ilikuwa ni siku 150.
Alisema wananchi wenyewe walisaini mkataba wa malipo na wengi wao wamepokea malipo hayo kilichobaki ni kulibadili eneo hilo kuwa la kisasa kwa ajili ya matumizi kusudiwa.
“ Wananchi wamedhamiria kuendelea kuishi katika eneo hilo huku wakijua kuwa ni kunyume…lakini taratibu zimefuatwa na ubomoaji utaendelea ili miradi mingine iendelee na kuongeza pato la taifa,”alisema Kagimbo.
Naye, Kaimu Mthamini wa manispaa hiyo, Victor Ndonne alisema mradi huo ulibuniwa na manispaa tangu mwaka 2006 na tangu wakati huo kumekuwa na hatua mbalimbali za utwaji maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo.
Alisema manispaa ilimwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili itolewe idhini ya kufanya mapitio ya mradi huo.
Ndonne alisema katibu mkuu alitoa idhini ya mapitio ya mradi huo ambapo manispaa kwa kushirikiana na mthamini Mkuu wa Serikali walitengua uhalali wa kitabu cha kwanza na kukubaliana kwa pamoja kutumika kwa kitabu cha pili.
“Mapitio yalifanyika baada ya mwekezaji kulalamika gharama ya mradi huku kuna miradi mingine imefanyika kipindi kama hicho na gharama zake zilikuwa chini,”alisema Ndonne.
Waandishi wa Mtanzania walishuhudia tingatinga T 502 CZP, T 202 CFN, T 159 BED na T 205 DCS zikiwa katika eneo hilo zikiendelea na ubomoaji huku baadhi ya wananchi wakiwa wanalinda mali zao nje wakiwa wamekosa makazi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni