Jumanne, 1 Desemba 2015

BUGURUNI WANUSURIKA MAFURIKO



WAKAZI wa Buguruni  Kwamnyamani wamenusurika kuzama tena kutokana na maji kuingia kwenye makazi yao na kusababisha usumbufu mkubwa baada ya mtaro wa kupitisha maji ambao haujakamilika kujengwa kuziba.
Awali Machi 16, mwaka huu Mtaro huo ulisababisha wakazi hao kuishi katika mazingira magumu baada ya nyumba zaidi ya 300 kujaa maji, hivyo, kumfanya Rais Jakaya Kikwete kufika eneo hilo na kutaka baadhi ya nyumba zivunjwe na ujenzi wa mtaro huo uanze mara moja.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani ujenzi wa mtaro huo umekuwa wakusuasua na kusababisha maji kuingia katika makazi yao pindi mvua zinaponyesha.
Mmoja wa wakazi hao, Abdallah Mtigile alisema mvua zilizonyesha juzi jioni zilisababisha maji kuingia katika makazi yao na kusabisha hofu kubwa na uhalibifu wa mali zao.
“Tunahitaji msaada wa haraka kutokana na mvua ambazo zimeanza kunyesha kwani mtaro huu haupeleki maji kabisa mvua kidogo tu unaziba,” alisema Mtigile.
Alisema hali hiyo imewafanya kutokwenda kazini kwa kuhofia familia zao kupoteza maisha kwa mafuriko kutokana na mvua zilizoanza kunyesha.
“Tunahitaji Rais Magufuli aje aone kupuuzwa kwa agizo la Rais Kikwete, hakuna anayetusikiliza kilio chetu ...tuko hatarini kwa kuwa mamlaka ya hali ya hewa imesema kutakuwepo na mvua kubwa msimu huu,” alisema Mtigile.
Naye Faudhia Ally alisema kuwa maji ya mvua yaliingia ndani huku yakiwa yamechanganyika na maji ya vyooni jambo ambalo linaweza kupelekea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kuendelea kuenea eneo hilo.
“Maji yaliyochanyika na uchafu wa vyooni yalifika mpaka mlangoni na kutufanya tushindwe kutoka nje kwa kuhofu magonjwa ya mlipuko… huenda kipindupindu kikaongezeka kutokana na mvua hizi,” alisema Faudhia.
Akizungumza ofisini kwake Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mnyamani, Abdallah Mng’ae alisema amefanya juhudi mbalimbali kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kupiga simu kwa viongozi wa manispaa.
“baada ya maji kuingia kwenye makazi ya watu nilipiga simu kwa uongozi wa manispaa wakasema hawana nafasi na kumtuma dereva wa mashine(Excavator) iliyokuwepo kwenye eneo hilo akafika na kuzibua,” alisema Mng’ae.
Alisema Katibu mkuu alifika eneo hilo hivi karibuni na kuwataka uongozi kumaliza ujenzi wa mtaro huo haraka lakini mpaka sasa bado unasuasua huku mkandarasi akidai kutolipwa fedha za ujenzi. 
Alisema ujenzi wa mtaro huo umekuwa ukijengwa kwa kitumia nondo za hali ya chini hivyo kusababisha kubomoka kabla ya kumalizika.
“Kama mnavyoona karavati walizotumia ni ndogo ambazo ni rahisi kuziba na haziwezi kupitisha maji yanapokuja kwa kasi hivyo kurudi katika makazi ya watu,” alisema.
Fichua ilishuhudia watu wakihamisha samani zao za ndani na kuyahama makazi yao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni