Jumatatu, 4 Januari 2016

NYUMBA ZILIZOWEKEWA X ZAFIKIA 5522



ZOEZI la uwekaji wa alama ya X katika nyumba zilizojengwa  mabondeni jana limeendelea huku nyumba  zaidi ya 3000 zilizojengwa katika bonde la mto Msimbazi ziliwekewa X.
Imeelezwa kuwa tangu kuanza kwa zoezi hilo la uwekaji wa alama hiyo katika  nyumba zilizojengwa mabondeni nyumba zaidi ya 5000  zimewekewa  X  na kwamba kutokana na idadi hiyo inaonyesha kuwa nyumba nyingi zitaathiriwa na bomoa bomoa hiyo.
Kutokana  na vurugu zilizofanyika juzi wakati wa kuanza kwa zoezi hilo la kuweka X katika nyumba hizo za mabondeni, Jeshi la Polisi lililazimika kuimarisha ulinzi ili kuwawezesha wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kuendelea na zoezi hilo la uwekaji wa alama.
Wakati wa zoezi hilo polisi pamoja na wafanyakazi wa NEMC walilazimika kutembea kwa miguu kutoka Jangwani kuelekea Buguruni Alhamza kwenda na kurudi kutokana na kuwa maeneo hayo hakuna barabara za kupia magari kwa sababu ya ubovu wa miundombinu.
Polisi hao walionekana kupita kila kona huku wakiwa na mabomu ya machozi pamoja na bunduki hali ambayo ilisababisha wananchi kuanza kuzungumza maneno ya kejeli kuwa Chama Cha Mapinduzi ‘(CCM) ni ile ile’ na ‘acha waisome namba CCM mbele kwa mbele’.
Wakati zoezi hilo linaendelea wapo baadhi ya askari walikuwa wakizunguka maeneo ya Round about ya Kigogo ili kuhakikisha kwamba wananchi  hawafanyi vurugu zozote kama kuchoma matairi na kufunga barabara.
Akizungumza baada ya kumaliza zoezi hilo kwa jana Ofisa Mazingira Mwandamizi kutoka NEMC Arnold Kusiraga alisema kuwa zoezi hilo la jana wameweka nyumba zaidi ya 3000 ambapo tangu waanze zimefikia takribani 5500.
“Inavyoonekana nyumba zitakazovunjwa zitakuwa nyingi tofauti na makadirio ya kwanza kwani kwa sasa tumefanya kazi kama robo tu lakini nyumba ni nyingi na maeneo yaliyobaki  bado mengi,”alisema.
Aidha alitaja maeneo ambayo yaliwekewa alama jana kuwa ni Jangwani, Kigogo mbuyuni, Kigogo Sambusa, Mapera, Dampo na Buguruni Alhamza.
Hata hivyo alisema zoezi la kubomoa nyumba linaendelea leo katika maeneo ya Bonde la Mkwajuni hadi Daraja la Sarender ambapo Machine za kubomolewa zimeongezwa kutokana tatu hadi kufikia nane.
Alisema zoezi la kuweka X  linaendelea leo katika maeneo ya Buguruni Kwamnyamani hadi Segerea.
Alisema maeneo mengine yatakayoathiriwa na bomobomoa hiyo ni wale waliojenga kandokando ya mito ambapo aliitaja baadhi ya mito hiyo kuwa ni Mto Msimbazi, Mzinga, Kizinga, Mto Ng’ombe, Tegeta, Mbezi, Mpiji, Mineva na Nyakasangwe

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni