Jumanne, 1 Desemba 2015

BUGURUNI WANUSURIKA MAFURIKO



WAKAZI wa Buguruni  Kwamnyamani wamenusurika kuzama tena kutokana na maji kuingia kwenye makazi yao na kusababisha usumbufu mkubwa baada ya mtaro wa kupitisha maji ambao haujakamilika kujengwa kuziba.
Awali Machi 16, mwaka huu Mtaro huo ulisababisha wakazi hao kuishi katika mazingira magumu baada ya nyumba zaidi ya 300 kujaa maji, hivyo, kumfanya Rais Jakaya Kikwete kufika eneo hilo na kutaka baadhi ya nyumba zivunjwe na ujenzi wa mtaro huo uanze mara moja.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani ujenzi wa mtaro huo umekuwa wakusuasua na kusababisha maji kuingia katika makazi yao pindi mvua zinaponyesha.
Mmoja wa wakazi hao, Abdallah Mtigile alisema mvua zilizonyesha juzi jioni zilisababisha maji kuingia katika makazi yao na kusabisha hofu kubwa na uhalibifu wa mali zao.
“Tunahitaji msaada wa haraka kutokana na mvua ambazo zimeanza kunyesha kwani mtaro huu haupeleki maji kabisa mvua kidogo tu unaziba,” alisema Mtigile.
Alisema hali hiyo imewafanya kutokwenda kazini kwa kuhofia familia zao kupoteza maisha kwa mafuriko kutokana na mvua zilizoanza kunyesha.
“Tunahitaji Rais Magufuli aje aone kupuuzwa kwa agizo la Rais Kikwete, hakuna anayetusikiliza kilio chetu ...tuko hatarini kwa kuwa mamlaka ya hali ya hewa imesema kutakuwepo na mvua kubwa msimu huu,” alisema Mtigile.
Naye Faudhia Ally alisema kuwa maji ya mvua yaliingia ndani huku yakiwa yamechanganyika na maji ya vyooni jambo ambalo linaweza kupelekea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kuendelea kuenea eneo hilo.
“Maji yaliyochanyika na uchafu wa vyooni yalifika mpaka mlangoni na kutufanya tushindwe kutoka nje kwa kuhofu magonjwa ya mlipuko… huenda kipindupindu kikaongezeka kutokana na mvua hizi,” alisema Faudhia.
Akizungumza ofisini kwake Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mnyamani, Abdallah Mng’ae alisema amefanya juhudi mbalimbali kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kupiga simu kwa viongozi wa manispaa.
“baada ya maji kuingia kwenye makazi ya watu nilipiga simu kwa uongozi wa manispaa wakasema hawana nafasi na kumtuma dereva wa mashine(Excavator) iliyokuwepo kwenye eneo hilo akafika na kuzibua,” alisema Mng’ae.
Alisema Katibu mkuu alifika eneo hilo hivi karibuni na kuwataka uongozi kumaliza ujenzi wa mtaro huo haraka lakini mpaka sasa bado unasuasua huku mkandarasi akidai kutolipwa fedha za ujenzi. 
Alisema ujenzi wa mtaro huo umekuwa ukijengwa kwa kitumia nondo za hali ya chini hivyo kusababisha kubomoka kabla ya kumalizika.
“Kama mnavyoona karavati walizotumia ni ndogo ambazo ni rahisi kuziba na haziwezi kupitisha maji yanapokuja kwa kasi hivyo kurudi katika makazi ya watu,” alisema.
Fichua ilishuhudia watu wakihamisha samani zao za ndani na kuyahama makazi yao.

WALIOUNGUA MOTO KUTIBIWA BURE



HOSPITALI ya Aga khani inatarajia kufanya upasuaji bure kwa  wanawake na watoto walioungua na kushindwa kuvitumia baadhi ya viungo hivyo wenye matatizo hayo wafike Disemba 12, mwaka huu katika hoptali ya Dar es Salaam.
Akizungumza na FICHUA, Ofisa Mawasiliano wa hospitali hiyo, Edna Mullumba alisema upasuaji huo utafanywa na jopo la madaktari wa kike kutoka nchi mbalimbali.
“Upasuaji huo utafanywa kwa wanawake na watoto wa jinsia ya kike tu kwa kuwa mradi huo unaitwa Women to women hivyo watoto wa kiume watatibiwa kwa sababu za msingi tu,” alisema Edna.
Alisema wagonjwa hao watafanyiwa upasuaji na kuweza kuvitumia viungo ambavyo viliungua.
Alisema matibabu hayo yatahusisha makovu yatokanayo kwa kuungua moto na kusababisha sehemu ya mwili kushindwa kutumika kama mkono, kiwiko na bega.
“Watatibiwa pia walioungua sura na kukwamisha uwezo wa mwanamke kufumba na kufumbua macho, kufungua na kufunga mdomo pamoja na kugeuza shingo ama kichwa,” alisema Edina.
Alisema yatatibiwa pia majeraha ya miguu yanayosababisha mgonjwa kushindwa kutembea ama kutembea kwa shida kuungua sura na kuungua kifua.
mwisho   

WAANDISHI WAITAKA MAHAKAMA KUWATENGEA ENEO LAO



WAANDISHI wa habari za mahakama nchini wameitaka mahakama kuandaa mazingira rafiki na sehemu bora zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Akisoma mapendekezo yaliyotolewa katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari za mahakamani yaliyomalizika juzi, mmoja wa waandishi hao, Kulwa Mzee alisema wamekuwa wakipata shida kupata sehemu ya kufanyia kazi zao hivyo kuitaka mahakama kuandaa eneo hilo.

Alisema ili kuboresha kuanzishwe mtandao wa waandishi na mahakama utakaosaidia upatikanaji wa vitu muhimu kama takwimu, hukumu na usajili.

“Tunaziomba Mahakama na Baraza la Habari Nchini(MCT) kuanzisha mafunzo endelevu ya waandishi wa habari za mahakama ambayo yatashirikisha pia wahariri ili kuepuka makosa kutokana na kutojua lugha za kimahakama,” alisema Kulwa.
Alisema katika mapendekezo yao wamewataka Majaji na Mahakimu kutoa nakala za hukumu pamoja na muhtasari kwa waandishi.
“Tunapendekeza Mahakama na MCT kushawishi uanzishwaji wa madawati ya habari za mahakamani katika vyumba vya habari ili kuwasaidia waandishi,” alisema Kulwa.
Kwa upande wake Jaji Kiongozi, Shaban Lila alisema mafunzo hayo ni muhimu katika kujenga mahusiano mazuri kati ya vyombo vya habari na mahakama.
Alisema mhimili wa Mahakama uliwahi kupewa tuzo ya kufuli lililofungwa kuonyesha kuwa walikuwa wagumu kutoa habari zao.
“Tunahitajiana, wote tunafanya kazi kwa ajili ya jamii hivyo tushirikiane kwa kutoa habari zilizosahihi, fasaha na kwa wakati,”alisema Lila.
Alisema Mahakama imekuwa ikilalamikia uandishi wenye mapungufu huku waandishi wakilalamika ugumu wa kupata habari.
“Waandishi wamekuwa wakitumia maneno ya kuhukumu katika uandishi wao kabla kesi haijatolewa hukumu na kusababisha usumbufu kwa jamii walioaminishwa tofauti na hukumu iliyotolewa,” alisema Lila.
Jaji Lila alisema si kwamba mahakama wanakwepa kuambiwa kasoro zao bali ziwakilishwe kwa lugha za staha bila kuwashambulia majaji na mahakimu.
“Hakuna Jaji anayeweza kuamua anavyotaka yeye, anaamua kutokana na sheria na ushahidi, kama kuna tatizo ni upungufu wa sheria husika na si Jaji,” alisema Jaji Lila.
Mwisho


    

Jumatatu, 16 Novemba 2015

bomoa bomoa kurasini wakazi hali tete



WAKAZI wa Kurasini Shimo la Udongo wamejikuta wakikosa makazi baada ya nyumba 45 walizokuwa wakiishi kubomolewa ili kupisha upanuzi wa bandari na ujenzi wa maegesho ya malori.
Ubomoaji huo ulifanyika jana, saa moja asubuhi hali iliyosababisha wananchi wa eneo hilo kujikuta wakitawaliwa na vilio, simanzi kutokana na kuharibiwa kwa mali zao zilikuwemo ndani ya nyumba hizo.
Wakati kazi hiyo ikiendelea polisi walikuwa wameimarisha ulinzi katika eneo hilo, wakishirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambao walikuwa na jukumu la kuzuia kutokea kwa tatizo la umeme kwa nyumba zilizokuwa na nishati hiyo.
Bomoabomoa hiyo iliwanufaisha vibaka waliokuwa wakivamia na kupora vitu wakati kazi ya ubomoaji ilipokuwa ikiendelea huku vijana wengine walinufaika na ajira ya uokoaji kwa kulinda mali zao.
Akizungumza na FICHUA Diwani aliyemaliza muda wake, Wilfred Kimati alisema, ubomoaji huo umefanyika kinyume cha sheria kwakuwa wananchi bado walikuwa wakidai malipo yao.
Alisema eneo hilo lilifanyiwa tathimini na mthamini kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi ambapo wananchi wa eneo hilo walikuwa 161 na walitakiwa kulipwa fidia ya Sh. Bilioni 16.
Kimati alisema eneo hilo limechukuliwa na mwekezaji kampuni ya Easy Netwotk Solution ambao walikubali kulipa fidia stahili na eneo hilo litumiwe kwa maegesho ya magari makubwa.
“Tumebaini Manispaa ya Temeke ina vitabu viwili vya tathmini ambapo malipo yaliyofanywa yakionyesha kuwepo makato makubwa kwenye fidia hali iliyosababisha baadhi ya wenye nyumba 64 kufungua mashauri mahakamani kugomea fidia hiyo wakidai walipwe iliyokuwa imepangwa na wizara,”alisema Kimati.
Kimati alisema eneo hilo lina nyumba 165 ambapo nyumba 45 ndiyo zimebomolewa zikiwemo zilizokuwa kwenye zuio la Mahakama jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria.
Kwa upande wake, mwananchi James Mwakalobo alilalamikia nyumba yake kubomolewa wakati ikiwa na zuio la mahakama.
Naye, Mwenyekiti wa mtaa huo, Rajabu Nkumilwa alisema, manispaa hiyo imekiuka kwakuwa wananchi wake walikuwa na madai ya msingi.
Alisema wananchi wanalia na upunjwaji wa fidia kwakuwa wengine wamelipwa kiwango cha chini Sh. Milioni 27 hadi Mil.188 wakati nyumba hizo zilikuwa na hatimiliki na thamani kubwa.
“Wananchi walikubali uhakiki wa malipo ya fidia ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi lakini cha ajabu manispaa ya Temeke nao wameingilia kati na kupunja fidia za wananchi hawa,”alisema Nkumilwa.
Akijibu hoja hizo Mkurugenzi wa Temeke, Photidas Kagimbo alisema ubumoaji wa eneo hilo ulikuwa sahihi kwakuwa notisi ilianzia Juni 10 mwaka huu na ilikuwa ya siku 60 na hadi jana wanafanya ubomoaji ilikuwa ni siku 150.
Alisema wananchi wenyewe walisaini mkataba wa malipo na wengi wao wamepokea malipo hayo kilichobaki ni kulibadili eneo hilo kuwa la kisasa kwa ajili ya matumizi kusudiwa.
“ Wananchi wamedhamiria kuendelea kuishi katika eneo hilo huku wakijua kuwa ni kunyume…lakini taratibu zimefuatwa na ubomoaji utaendelea ili miradi mingine iendelee na kuongeza pato la taifa,”alisema Kagimbo.
Naye, Kaimu Mthamini wa manispaa hiyo, Victor Ndonne alisema mradi huo ulibuniwa na manispaa tangu mwaka 2006 na tangu wakati huo kumekuwa na hatua mbalimbali za utwaji maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo.
Alisema manispaa ilimwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili itolewe idhini ya kufanya mapitio ya mradi huo.
Ndonne alisema katibu mkuu alitoa idhini ya mapitio ya mradi huo ambapo manispaa kwa kushirikiana na mthamini Mkuu wa Serikali walitengua uhalali wa kitabu cha kwanza na kukubaliana kwa pamoja kutumika kwa kitabu cha pili.
“Mapitio yalifanyika baada ya mwekezaji kulalamika gharama ya mradi huku kuna miradi mingine imefanyika kipindi kama hicho na gharama zake zilikuwa chini,”alisema Ndonne.
Waandishi wa Mtanzania walishuhudia tingatinga T 502 CZP, T 202 CFN, T 159 BED na T 205 DCS zikiwa katika eneo hilo zikiendelea na ubomoaji huku baadhi ya wananchi wakiwa wanalinda mali zao nje wakiwa wamekosa makazi.

Jumanne, 10 Novemba 2015

NANI WAZIRI WA KILIMO?

SEKTA ya kilimo ni moja ya sekta muhimu hapa nchini ambayo hapo zamani tuliita kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wetu.
Mara baada ya nchi yetu kupata Uhuru, Serikali ilitoa kipaumbele cha kwanza katika kuendeleza kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.
 Kilimo kiliajiri zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wote kwa mazao ya katani, kahawa na pamba yaliongoza kulipatia Taifa fedha za kigeni taifa hili.
kwa sasa ajira inayotokana na kilimo imeshuka hadi asilimia 80 tu ya watanzania ambapo pato la fedha za kigeni kutokana na mazao ya kibiashara limeshuka kutokana na kukosekana mipango na utekelezaji wa sera zinazosimamia sekta hii.

Katika awamu ya kwanza kumekuwapo kaulimbiu na maazimio mbalimbali kama vile “Chakula ni Uhai”, “Siasa ni Kilimo”,“Kilimo cha Kufa na Kupona”, “Mvua za Kwanza ni za Kupandia” ili kuhamasisha maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha kilimo cha ujamaa.
Awamu ya Pili iliongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi ambapo tulishuhudia mageuzi ya kiuchumi ambayo yalikuwa kichocheo kikubwa katika maendeleo ya kilimo ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya mwaka 1983.
Awamu ya tatu ya uongozi ilikuwa chini ya Rais Benjamin William Mkapa ambapo katika awamu hiyo kilimo kilipata msukumo wa kipekee kwa kuonyesha mwelekeo Katika awamu hiyo kutokana na
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kilimo na Mifugo ya mwaka 1997 na uanzishwaji wa Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo ulishuhudia kilimo kikikua kutoka chini ya asilimia 3 hadi asilimia 6 kulinganisha na awamu zilizotangulia.

Awamu ya nne ya uongozi ambayo ipo chini ya Rais Dk. Jakaya Kikwete, licha ya kilimo kuendelea kupewa kipaumbele kikubwa, kwa kaulimbiu mbadala ya kilimo kwanza pamoja na utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika (CRMP) ambazo zimekuwa chachu ya kuleta mapinduzi ya kijani hapa nchini lakini lengo halikutimia ipasavyo kutokana na

Licha ya hayo Jambo kubwa la kujivunia kutokana na kilimo ni kuwa
kwa sasa asilimia 95 ya mahitaji ya Taifa ya chakula kinazalishwa hapa hapa nchini kwa Serikali kuweka mfumo wa kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi wakati upungufu unapotokea ili kukabiliana na baa la njaa. Takwimu zinadhihirisha kwamba akiba ya Taifa ya Chakula imekuwa ikiongezeka kila mwaka na uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unatarajia kufikia tani 400,000.

Kwa takribani miongo mitano na ushei ya Uhuru wa nchi yetu, pamoja na kuwa na changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kiuchumi, kilimo chetu kimeendelea kuwa nguzo kuu na mhimili wa kujitoshereza kwa chakula tu.
Lakini iwapo tutakuwa na uthubutu wa kuwekeza inavyopaswa katika kilimo tutaweza si tu kujitoshereza kwa chakula bali pia kupiga hatua za maendeleo kwa sekta hiyo adhimu, pengine kiasi cha kurudisha tija kubwa ya pato la kigeni inayoweza kupatikana kwa kurekebisha mikakati ya mazao ya kibiashara kwa kulenga mahitaji ya sasa ya soko.

Kimsingi baadhi ya maeneo muhimu yanayopaswa kuangaziwa na awamu ya tano ya serikali ili kukirudishia kilimo hadhi yake kamili ni pamoja na tathmini muafaka ya kilichosababisha kudorora kwa sekta hiyo, ili kubaini nini kifanyike kiutekelezaji ili kufikia ufanisi wa hali ya juu.
Mathalan, baadhi ya maeneo muhimu yanayopaswa kutazamwa upya ni pamoja na upatikanaji nafuu wa pembejeo ambao umekuwa ukisuasua kutokana na gharama kuwa kubwa ukilinganisha na uwezo wa wakulima wetu.
Uwekezaji muafaka wa mbinu za kisasa za kilimo kwa kuzingatia matumizi ya nyenzo, mbolea, kubaini aina ya mazao yanayofaa kulimwa katika ardhi husika pamoja na kuboresha weledi wa maafisa ughani katika kusimamia kiklimo cha kimapinduzi, kitakacholitoa taifa letu katyika kilimo cha mazoea kwa ajili ya chakula lakini kikakidhi pia mahitaji ya kibiashara na kiuchumi.

Kwa historia ya sekta hiyo hapa nchini kuna mengi tunayoweza kutohoa kutokana na utekelezaji wa miaka iliyopita, mojawapo ni kuwepo kwa mashamba ya ushirikika kwa kuwa kimsingi licha ya mengi kati ya mashamba hayo kufa kifo cha asili lakini bado vyama vya ushirikika vipo. Ni suala la kugeuza tu mashamba yaliyokuwa katyika muundo huo hata yaliyomilikiwa na serikali, kuwa mikononi mwa wakulima lakini msisitizo ukiwekwa katika upatikanaji masoko ya kuuzia mazao yatakayovunwa.

Hayo yakitekelezwa vyema dhima nzima ya uwepo wa viwanda ili vitumie ghafi muhimu inayozalishwa kwa kilimo, ndipo itaweza kutimia kikamilifu kwa kuwa soko la dunia la kilimo kwa sasa limeegemea bidhaa zitokanazo na kilimo zilizokuwa tayari kwa matumizi na si ghafi inayopaswa kuandaliwa kuwa bidhaa.
hiyo mikakati ya serikali ya awamu ya tano iliyojinasibu kufufua viwanda wakati wa kampeni itatimia si kwa kuangalia upande huo tu, bila kuhusisha kilimo kwa kuwa ilidhihirika wazi wakati wa awamu ya kwanza zao la pamba lilikuwa na soko kubwa la ndani kutokana na kuwepo viwanda vingi vya kuzalisha nguo, kabla ya ziada kuuzwa nje na kutupatia fedha za kigeni.

Kuwekeza kwenye viwanda sanjari na kilimo kuna faida nyingi kwa kuwa tumezungukwa na masoko yaliyo tayari kupokea bidhaa zetu katika jumuiya zinazotuzunguka ikiwemo SADC na EAC anvayo kwa sasa ina soko kubwa zaidi kwa kuwa inajumuisha nchi tano, tofauti na ilivyokuwa awali ilipoundwa na nchi tatu.
Tukienda mbali zaidi kuna fursa za kimataifa kama ule mpango wa AGOA ambao bado unatuwezwesha kupata pato kubwa la kigeni nchini Marekani, bila gharama ya tozo la ushuru wa kuingiza bidhaa nchini humo.

Na kwa kuwa kinara wa awamu ya rtanio Raisi Magufuli anatokea katika wizara ya ujenzi na awali alitumikia uchukuzi na uvuzi, tunaamini akiunganisha vyote hivyo na kunasibisha kilimo naviwanda uchumi utakuwa kwani bidhaa zinazozalishwa zinahitaji miundo mbinu bora kufikia walaji wa ndani na nchi jirani…

Lakini ili kufikia mafanikio ya kiwango cha juu kwa sekta hizo zinazotegemeana kuna haja ya makusudi ya kutathmini baadhi ya changamoto zilizosababisha kilimo kidumae zikiwemo ardhi ya kilimo kutotambulika kisheria hivyo kubadilishwa matumizi, jambo linalozalisha migogoro holela baina ya wawekezaji na wananchi wazawa waliomilikishwa maeneo kwa njia ya kurithi.
Mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kilimo kushindwa kutoa ajira kutokana na upungufu wa mvua, jangwa na kuongezeka kwa joto duniani.

 Ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika kilimo ambapo sekta nyingi zimejikita kuwekeza katika fani nyingine.

 Ushiriki hafifu wa vijana katika kilimo ambao ndio mguvu kazi na rasilimali watu kwa kuwa ndio wenye nguvu na uwezo mkubwa, kukikwepa kilimo kwa kukimbilia mijini kufanya biashara zisizo endelevi.
              
Uwezo mdogo wa wakulima kununua zana bora na pembejeo za kilimo
 Miundombinu duni katika maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo

Msukumo wa kuzalisha mazao ya nishati mbadala na madhara yake unakinzana na lengo kuu la kuzalisha mazao ya chakula kwa baadhi ya wakulima ambapo wengi huangazia kilimo cha chakula na kuachana na mazao ya biashara.

Gharama kubwa ya ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na maghara ya kuhifadhia mazao pindi yanapovunwa.

Uvamizi wa visumbufu vya mimea yanayoshindikana kudhibitiwa ambavyo ni pamoja na wadudu na magonjwa mbalim bali ya mimea.

Elimu duni walionayo wakulima pamoja na wadau wa mbalimbali wa kilimo juu ya masuala ya ushirika pamoja na vyama hivi kukosa mitaji na kubaki vikikopa mazao ya wakulima.
Usimamizi hafifu wa sera ya soko huru ambapo dhana hiyo imekuwa kinyume na matarajio ya wengi na sasa ni kama soko holela lisilokuwa na mdhibiti.
Idadi ndogo ya wataalam wa kilimo na ushirika pamoja na maslahi duni ukilinganisha na mazingira wanakohitajika kufanya kazi.
Kukosekana kwa mikopo yenye masharti nafuu ya kuendeleza kilimo kwa mabenki mengi kukwepa kukopesha sekta hiyo kwa kuichukulia kuwa Nyanja isiyotabirika katika uwezo wa kurudisha mikopo.

Kimsingi pia lazima kuwekeza kwa vivutio vya makusudi vitakavyosababisha nguvu kazi kubwa hususan vijana kujishugulisha na kilimo kama njia ya kuendesha maisha yao na kubadili mtazamo mzima juu ya sekta hiyo, kwa kurejesha hamasa za kimatendo zaidi kwa kutumia mbinu za zamani kwa mabadiliko ya kisasa kuanzia ngazi za awali kabisa za mafunzo ya vinaja wetu katika ngazi mbalimbali za elimu ili wasikikimbie kilimo badala yake wavutiwe nacho. 
Kwa kutimiza hayo na mengine muambatano naamini kauli mbiu ya HAPA KAZI TU itajisadikisha ipasavyo kwenye sekta ya kilimo maana matokeo ya kazi ni tija stahiki.
0762656400 KWA MAWASILIANO