WAKAZI
wa Buguruni Kwamnyamani wamenusurika
kuzama tena kutokana na maji kuingia kwenye makazi yao na kusababisha usumbufu
mkubwa baada ya mtaro wa kupitisha maji ambao haujakamilika kujengwa kuziba.
Awali
Machi 16, mwaka huu Mtaro huo ulisababisha wakazi hao kuishi katika mazingira
magumu baada ya nyumba zaidi ya 300 kujaa maji, hivyo, kumfanya Rais Jakaya
Kikwete kufika eneo hilo na kutaka baadhi ya nyumba zivunjwe na ujenzi wa mtaro
huo uanze mara moja.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani ujenzi
wa mtaro huo umekuwa wakusuasua na kusababisha maji kuingia katika makazi yao
pindi mvua zinaponyesha.
Mmoja
wa wakazi hao, Abdallah Mtigile alisema mvua zilizonyesha juzi jioni
zilisababisha maji kuingia katika makazi yao na kusabisha hofu kubwa na
uhalibifu wa mali zao.
“Tunahitaji
msaada wa haraka kutokana na mvua ambazo zimeanza kunyesha kwani mtaro huu
haupeleki maji kabisa mvua kidogo tu unaziba,” alisema Mtigile.
Alisema
hali hiyo imewafanya kutokwenda kazini kwa kuhofia familia zao kupoteza maisha
kwa mafuriko kutokana na mvua zilizoanza kunyesha.
“Tunahitaji
Rais Magufuli aje aone kupuuzwa kwa agizo la Rais Kikwete, hakuna
anayetusikiliza kilio chetu ...tuko hatarini kwa kuwa mamlaka ya hali ya hewa
imesema kutakuwepo na mvua kubwa msimu huu,” alisema Mtigile.
Naye
Faudhia Ally alisema kuwa maji ya mvua yaliingia ndani huku yakiwa
yamechanganyika na maji ya vyooni jambo ambalo linaweza kupelekea magonjwa ya
mlipuko kama kipindupindu kuendelea kuenea eneo hilo.
“Maji
yaliyochanyika na uchafu wa vyooni yalifika mpaka mlangoni na kutufanya
tushindwe kutoka nje kwa kuhofu magonjwa ya mlipuko… huenda kipindupindu
kikaongezeka kutokana na mvua hizi,” alisema Faudhia.
Akizungumza
ofisini kwake Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mnyamani, Abdallah Mng’ae
alisema amefanya juhudi mbalimbali kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na
kupiga simu kwa viongozi wa manispaa.
“baada
ya maji kuingia kwenye makazi ya watu nilipiga simu kwa uongozi wa manispaa
wakasema hawana nafasi na kumtuma dereva wa mashine(Excavator) iliyokuwepo
kwenye eneo hilo akafika na kuzibua,” alisema Mng’ae.
Alisema
Katibu mkuu alifika eneo hilo hivi karibuni na kuwataka uongozi kumaliza ujenzi
wa mtaro huo haraka lakini mpaka sasa bado unasuasua huku mkandarasi akidai
kutolipwa fedha za ujenzi.
Alisema
ujenzi wa mtaro huo umekuwa ukijengwa kwa kitumia nondo za hali ya chini hivyo
kusababisha kubomoka kabla ya kumalizika.
“Kama
mnavyoona karavati walizotumia ni ndogo ambazo ni rahisi kuziba na haziwezi
kupitisha maji yanapokuja kwa kasi hivyo kurudi katika makazi ya watu,”
alisema.
Fichua ilishuhudia watu wakihamisha samani zao za ndani na kuyahama makazi yao.