Jumanne, 21 Novemba 2017

'kuweni wazalendo'

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Alias Kwandikwa amewataka wataalamu wa ujenzi kuwa wazalendo kwa kuokoa gharama za ujenzi wa majengo mbalimbali ili kulipunguzia mzigo taifa.
Akizungumza katika ziara yake aliyoifanya juzi katika mradi wa ujenzi wa nyumba za Wakazi wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam, Kwandikwa alisema uzalendo unahitajika hasa katika kipindi hiki taifa likiwa katika mageuzi makubwa kiuchumi.
Alisema wataalamu wanatakiwa kuwa wazalendo wakati wakisimamia miradi mbalimbali ya ujenzi ili kuokoa fedha zitakazokwenda katika miradi mingine.
“Wakati tunaangalia matumizi ya miradi ya serikali tujiulize kwenye familia zetu tunafanya hivi?,” alisema Kwandikwa.
Alisema wataalamu wa ujenzi waende kujifunza namna ya kupunguza gharama za ujenzi kwa  Wakala wa Ujenzi Tanzania(TBA) ambao katika miradi yao wamepunguza kwa kiwango kikubwa.
“Endeleeni kuokoa fedha kadri mnavyoweza baadaye mtatuambia kiasi mlichookoa ili zisaidie katika miradi mingine ya kitaifa,” alisema Kwandikwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga alisema wataendelea kufanya utafiti wa kushusha gharama za ujenzi ili kuongeza ushindani wa kibiashara.
Alisema mradi wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota utagharimu Sh Bilioni 20 mpaka kukamilika.
“Uzalendo ndio unaotufikisha hapa kwani vijana tulionao wanatanguliza maslahi ya Taifa mbele,” alisema Mwakalinga.
mwisho    


Elimu ya Ufundi changamoto kwa viwanda

TANZANIA inakabiliwa na upungufu wa walimu wa elimu ya ufundi jambo ambalo linasababisha baadhi ya vyuo vya ufundi stadi kuajiri walimu wasiokuwa na sifa zinazohitajika katika fani hiyo.
 Mpaka sasa kuna idadi ndogo ya vyuo vinavyofundisha ualimu wa ufundi stadi jambo linalosababisha kuwapo na walimu wasiokuwa na sifa katika vyuo vya elimu ya Ufundi.
Vyuo vya  mafunzo ya Ufundi stadi ni nguzo pekee ya kulisaidia taifa kuingia katika uchumi wa viwanda mwaka 2020 huku nchi ikitegemea kuingia katika uchumi wa kati.
Hivi karibuni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(NACTE) kwa kushirikiana na Kituo cha elimu ya watu wazima Kouvola kutoka nchini Finland waliandaa mkutano wa Kimataifa ili kubadilishana uzoefu kati ya nchi hizi mbili.
Mkutano huo ulibeba ujumbe wa ‘wekeza katika elimu ya ufundi ili Tanzania iweze kuingia katika uchumi wa viwanda’ umehuhudhuliwa na taasisi za elimu ya ufundi, wamiliki wa viwanda, wadau na wataalamu 30, wa sekta hiyo kutoka nchini Finland.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Elimu nchini Finland Dk.Tuija Arola anaelezea nchi hiyo ilivyoweza kuwekeza katika mafunzo ya wakufunzi wa elimu ya ufundi.
Anasema kuna umuhimu wa nchi kuwa na walimu waliobobea katika elimu ya ufundi stadi ili kuweza kutoa wahitimu waliokuwa na sifa za kukidhi soko la ajira.
“Walimu wa mafunzo ya ufundi stadi wanatakiwa kuwa na mafunzo endelevu katika kipindi chote cha ualimu wao ili kwenda na mabadiliko ya kasi ya teknolojia,” anasema Dk. Arola.
Anasema walimu wanatakiwa kutembelea katika maeneo ya viwanda kupata ujuzi mpya unaohitajika katika wakati husika.
Anasema Tanzania inatakiwa kuwekeza katika kuwaandaa wakufunzi wa mafunzo ya ufundistadi ili kufanikisha malengo ya kuwa nchi ya viwanda.
Akitolea mfano katika nchi ya Finland Arola anasema taaluma ya ualimu na ukufunzi nchini humo inathaminika na kuheshimika jambo ambalo linawaongezea nguvu wakufunzi katika kutekeleza majukumu yao.
Anasema kwa kuwa mafunzo ya wanafunzi huhamishiwa katika maeneo ya kazi hivyo wakufunzi wana wajibu wa kuratibu ushirikiano na kampuni zenye kutoa ajira kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi.
“Mkufunzi ana nafasi kubwa katika kuwezesha juhudi za kujifunza kwa mtu mmoja mmoja ili kufikia malengo yake binafsi,” anasema Dk. Arola.
Anaongeza kuwa kutokana na hali hiyo wakufunzi wa mafunzo ya ufundi wanatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha juu katika fani zao.
Anasema wakufunzi wa elimu ya ufundi wanatakiwa kutumia mbinu mbadala katika kuongeza kiwango chao cha elimu na ujuzi.
Aidha anazitaka mamlaka husika katika kusimamia elimu ya ufundi kuwatengenezea mazingira ya kazi wakufunzi hao ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha ili waweze kutimiza majukumu yao kikamilifu.
“Mabadiliko ya utendaji kazi wa walimu unahitaji kujitolea zaidi hivyo watafanikiwa iwapo tu watapata ushiriki na kuungwa mkono na mamlaka ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kifedha,” anasema Dk.Arola.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako anasema serikali inawekeza katika kuwaandaa walimu wa elimu ya ufundi ili kuwa na wataalamu wataoiwezesha nchi katika kuingia katika nchi ya viwanda.
Anasema nchi haiwezi kuingia katika uchumin wa viwanda bila kuwekeza katika raslimali watu watakaofanya kazi katika viwanda hivyo.
“Tujitathmini kuinua ubora wa elimu ya ufundi kwa kuchukua uzoefu kutoka kwa wenzetu kutoka Finland kwa kuwa wenzetu wamefanikiwa katika elimu ya ufundi,” anasema Profesa Ndalichako.
Anasema changamoto iliyopo ni muunganiko wa ubunifu unaofanywa na taasisi za mafunzo ya ufundi na viwanda.
“Changamoto ni namna ya kuunganisha ubunifu unaotolewa na taasisi za mafunzo kuingizwa katika maisha ya kawaida ya watanzania,” anasema Ndalichako.
Profesa Ndalichako anasisitiza juu ya mafunzo ya walimu na wahitimu katika taasisi za juu ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Niwaombe tufanye kazi kwa kushirikiana taasisi za mafunzo na waajiri kuangalia namna ya kupunguza utengano uliopo kwa kuwa kila mmoja anamtegemea mwenzake,” anasema Ndalichako.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk.Adolf Rutayuga anasema Baraza hilo linahakikisha kuwa wahitimu wanaotolewa na vyuo vilivyosajiliwa wanakidhi vigezo vya ajira na mahitaji ya soko.
Anasema kwa kuwa katika mkutano huo walikuwapo pia watoa maamuzi akiwamo waziri Ndalichako hivyo yatafanyiwa kazi na kupata suluhisho mapema.
“Hapa tumekuwa na viongozi wakubwa na watoa maamuzi hivyo yote yaliyozungumziwa katika mkutano huu yatapatiwa ufumbuzi kulingana na mahitaji,” anasema Dk.Rutayuga.
Anasema hii ni hatua moja ya kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kuwa waliokutana hapa ni wadau wakubwa katika sekta hiyo.
“Yamejadiliwa mengi katika mkutano huu hii ni hatua moja mbele kuelekea Tanzania ya Viwanda kwa kuwa tunaunganisha nguvu kwa maana ya Watoa Mafunzo na waajiri ama wenye viwanda,” anasema Dk. Rutayuga

Marufuku kusambaza takwimu za uchumi hila kibali

Na TUNU NASSOR 
DAR ES SALAAM 
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS ) imewaonya watu wanaotoa takwimu za Uchumi bila kuzingatia sheria ya Takwimu jambo ambalo linasababisha mkanganyiko katika jamii. 
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema hairuhusiwi kutoa takwimu hizo bila kuwa na kibali cha NBS. 
Alisema NBS haikatazi mtu binafsi wala kikundi cha watu kukusanya takwimu isipokuwa kinachotakiwa ni kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kupata kibali kutoka katika Ofisi hiyo. 
"Hatumnyimi mtu kibali cha kukusanya kuchakata na kusambaza takwimu isipokuwa kinachotakiwa ni kukusanya kulingana na misingi na sheria namba tisa ya Takwimu, " alisema Dk. Albina. 
Alisema ukusanyaji huo unahitaji weledi wa hali ya juu chini ya kanuni 10 za Takwimu za Dunia. 
" kinachonishangaza takwimu za serikali zinapotolewa mtu anasimama na kusema takwimu hizi si sahihi... Hii inatokea Tanzania pekee, hivyo asitokee mtu kupotosha takwimu za Uchumi " alisema Dk Albina. 
Alisema takwimu za Uchumi ni muhimu kwa utekelezaji wa ajenda ya Afrika ya mwaka 2063.
"Katika ajenda hii kitu kimojawapo ni ukuaji wa uchumi wa bara hilo na haiwezi kufanikiwa bila kuwa na takwimu bora za Uchumi,"  alisema Dk Albina. 
Naye Mkurugenzi wa Uchumi na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT), Johnson Nyella aliwataka wananchi wanaoshiriki katika ukusanyaji wa takwimu kutoa taarifa sahihi wanapojaza dodoso za takwimu