Jumatano, 30 Novemba 2016

watembea kilomita sita kutafuta huduma za afya



WAKAZI wa kijiji cha Kibamba, kata ya Mipeko wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 6 kufuata huduma za afya katika kijiji cha Mwanambaya.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Zahanati, Mtendaji wa kijiji hicho, Ally Madenge alisema kijiji hicho hakina huduma za afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungua njiani wakielekea kutafuta huduma hiyo.
“Hali ya huduma za afya kijijini hapa ni mbaya tunalazimika kuzifuata katika kijiji cha Mwanambaya na Mkuranga… huku tukiwa na wazee na watoto jambo ambalo ni hatari,” alisema Madenge.
Alisema kwa kuliona hilo wamelazimika kualika wadau mbalimbali kufanya harambee itakayosaidia ujenzi wa zahanati kijijini hapo.
Akiongoza harambee hiyo, Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega alisema jumla ya shilingi milioni 98 zinahitajika katika ujenzi wa Zahanati hiyo. 
“Niwahakikishie wote watakaochangia hapa kuwa hatutamvumilia yeyote atakayefanya ubadhilifu wa fedha ama vitu vitakavyochangwa hapa,” alisema Ulega.
Ulega alimtaka Diwani wa kata ya Mipeko kusimamia kila hatua ya ujenzi huo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Niwaombe vijana wa kijijini hapa mjitolee katika ujenzi huu…hatuwezi kutafuta fedha za ujenzi na za kulipa vibarua hivyo ili kupunguza gharama hata mimi nitakuja kushiriki katika kambi ya ujenzi ili tuondokane na hili,” alisema Ulega.
mwisho


Jumapili, 6 Novemba 2016

'SHERIA YA KUTETEA ABIRIA ITAFSIRIWE'

CHAMA cha Kutetea Abiria(Chakua) kimeitaka serikali kuitafsiri katika lugha ya kiswahili sheria ya kutetea abiria ya mwaka 2007 ili kuwawezesha abiria wengi kujua haki na wajibu wao wawapo katika vyombo vya usafiri.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Chakua, Francis Mugassa alisema sheria hiyo iko katika lugha ya kiingereza jambo linalosababisha abiria kukosa haki zao.
Alisema manyanyaso kwa abiria yameendelea kuwapo kutokana na kukosa ufahamu wa sheria.
“Hivi ni wangapi wanajua kusoma kiingereza kwa kuwa sheria hii haiwahusu wanaojua lugha hiyo bali ni watanzania wote hivyo tunaitaka serikali kuitafsiri na kuisambaza nchini,” alisema Mugassa.

Aidha mugassa aliwaomba wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zao katika kufikisha elimu kwa abiria.
“Tuna mkakati wa kupeleka elimu hii kwa wanafunzi mashuleni na vyuoni hivyo juhudi za wa wadau zinahitajika kutusaidia kufikia azma hii,” alisema Mugassa.
Katika hatua nyingine chakua imepokea msaada  wa vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi 860,000 kutoka katika taasisi ya Teknolojia ya Kibaha(KIT).
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, mhasibu wa KIT, Majid Ally alisema wanatambua mchango mkubwa wa Chakua katika jamii.

“Tumeona kazi zinazofanywa na chama hiki zinatupa matumaini kwa kuwa kila mmoja wetu ni abiria lakini hatukujua haki na wajibu wetu, hivyo tutoa msaada huu ili elimu iwafikie na wengine” alisema Ally.