BARAZA la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni limewachukulia
hatua za kinidhamu watumishi wake saba kwa kuwashusha vyeo na wengine kufukuzwa
kazini baada ya makosa waliyokuwa wakituhumiwa kuthibitika.
Miongoni mwa watumishi waliochukuliwa hatua ni Mhandisi
Mkuu wa Manispaa Hassan Mkuya ambaye ameshushwa cheo na sasa anakuwa mhandisi
wa kawaida pamoja na mwenzake Ismail Mafita aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Barabara
wa Manispaa.
Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) alisema
hayo jana wakati alipokuwa akisoma taarifa ya Baraza la Madiwani ambalo ndilo
lilipendekeza kuchukuliwa kwa hatua hizo.
“Desemba mwaka jana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Paul Makonda alitoa tuhuma dhidi ya watumishi wa manispaa hasa idara ya
uhandisi, baadae Mkurugenzi naye alichukua hatua ya kuwasimamisha kazi
watumishi 18 waliotuhumiwa na kuwafungulia mashauri ya kinidhamu.
“Kati ya hao 18, tisa walikuwa wa idara ya uhandisi, nane
idara ya afya na mmoja idara ya fedha. Mhandisi Mkuu alikuwa akituhumiwa kwa
makosa sita likiwamo la kutokufanya usanifu uliozingatia weledi hali
iliyopelekea gharama za miradi kuzidi na kushindwa kutembelea eneo la miradi na
wakandarasi kusababisha hasara za barabara ya Biafra, Journalism phase 2 na ile
ya Maandazi,” alisema.
Alisema tuhuma nyingine ni kutotoa cheti cha ukamilishaji
kazi, hatujui miradi kama imeshajengwa , kushindwa kusimamia miradi kwa kiwango
cha kuridhisha, mfereji wa basihaya kuwekwa karavati zisizokuwa na kiwango na kuongezeka
kwa gharama za miradi ya batabara bila kuzingatia taratibu za kisheria za
manunuzi ya umma.
“Kati ya tuhuma hizo zipo ambazo alikutwa na hatia moja kwa
moja na nyingine hakukutwa na hatia hivyo ameadhibiwa kulinga na yale
aliyokutwa na hatia moja kwa moja kama mfereji wa basihaya na barabara
zilizojengwa chini ya kiwango,” alisema.
Alisisitiza adhabu hizo zimetolewa baada ya uchunguzi wa
kina kufanyika kwa kushirikiana na vyombo vya dola, uchunguzi ulifanyika kwa
kwenda katika maeneo husika ya miradi na watuhumiwa walipewa siku 14 za
kujitetea.
Alisema hata hivyo adhabu hiyo waliyopewa haizuii watumishi
hao kuchukuliwa hatua zaidi ikiwamo kufikishwa mahakamani.
“Kwa sababu kama hiyo ya fedha za miradi kuzidi,
iligundulika kwamba walikubali baadhi ya wakandarasi kufanya kazi huku wakiwa
hawajafuata utaratibu wa manunuzi na hadi sasa tunadaiwa Sh bilioni tano, sasa
hii ni hasara na baada ya hatua hii tutakutana na hao wakandarasi ili
tujiridhishe kama kweli kazi ilifanyika na tutatoa taarifa ya kitakachoamriwa,”
alisema.
Pamoja na hayo, daktari mmoja wa Hosptali ya Palestina, Alphonse
Chiwambo amepewa onyo kali baada ya kukutwa na kosa la kuomba rushwa ya Sh
30,000 kwa mama aliyekwenda kujifungua.
“Lakini kuna watumishi wanne wa idara ya afya tumewafukuza
kazi kwa makosa ya utoro na rushwa na watumishi sita kati ya tisa wa idara ya
uhandisi wamerejeshwa kazini baada ya kukutwa hawana hatia,” alisema.
Alisema pamoja na hayo baraza liliridhia kwapandisha vyeo watumishi
372, kubadilisha vyeo watumishi tisa na kuwathibitisha watumishi 206 ambao
wamemaliza vipindi vyao vya majaribio na kuonekana kuwa wanafaa kufanya kazi
katika utumishi wa umma.