Jumapili, 1 Mei 2016

watumishi wa serikali mkoa wa Dar kujengewa nyumba



WAFANYAKAZI wa serikali wa mkoa wa Dar es Salaam wameahidiwa kujengewa nyumba katika viwanja vyao ili kuondokana na kero za kodi za nyumba.
Akizungumza katika maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi ilivyofanyika kimkoa jijini Dar es Salaam Mkuu wa Mkoa wa huo, Paul Makonda alisema wafanyakazi wamekuwa wakipata taabu nyingi kutokana na mishahara kutokidhi mahitaji ya kodi za nyumba na gharama za maisha.
Alisema mishahara wanayopata haiwezi kutosha kuhimili mazingira ya maisha ya jiji la Dar es Salaam.
“Sisi kama serikali ya mkoa tumekaa na kufikiri kuona namna ya kutafuta watu watakaowajengea nyumba ndani ya miezi sita katika viwanja vyenu nanyi mtalipa taratibu,” alisema Makonda.
Alisema tayari wamenza kutengeneza baadhi ya ramani ambazo wafanyakazi hao watachagua wanazozitaka.
“Mtalipa taratibu kwa kuwa nyinyi ni watumishi wa umma na mimi kama mkuu wa mkoa nitawadhamini,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa katika hatua za uboreshaji wa mazingira ya kufanyia kazi wameanza na walimu ambao ni kundi kubwa kwa kuwawezesha kusafiri bure.
“Lengo langu halikuwa kuishia katika usafiri wa daladala bali utasaidia hata katika mabasi yaendayo kasi japo nilisikitika sana kusikia baadhi ya viongozi wenu kutoa kauli ya kukataa eti kwa sababu wanadai wanamalimbiko na nyongeza ya mishahara.
Leo umenikuta mwenge unaniomba nauli ya kwenda posta kwa daladala mimi nakwambia nina  gari unaanza kutoa sababu za kuwa huna chakula,” alisema Makonda.
Aidha alisema katika kuhakikisha jiji la Dar es Salaam wanatarajia kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo.
“Niwaombe viwanda wanaotengeneza mifuko hiyo watubadilishie mifuko hii wa ndani ya siku 90,” alisema Makonda.  
Awali akisoma Risala kwa mgeni Rasmi, Mratibu wa maadhimisho hayo, Elias Chizingwa alisema wafanyakazi wa mkoa huo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo mishahara duni isiyokidhi mahitaji hasa katika jiji la Dar es Salaam, wafanyakazi kukatwa kodi mara tatu, baadhi ya waajiri kuchelewesha kupeleka michango katika mifuko ya hifadhi za jamii.
“Changamoto nyingine ni mazingira magumu ya kufundishia walimu, baadhi ya waajiri kutokuvitambua vyama vya wafanyakazi na baadhi ya makampuni ya wawekezaji wa nje kuwanyanyasa wafanyakazi wazalendokwa kuwafanyisha kazi kwa masaa zaidi 18,” alisema  Chizingwa.
mwisho

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni