Jumapili, 15 Mei 2016

WAJIFUNGULIA KWENYE MABOTI KWA KUKOSA VITUO VYA AFYA



WANANCHI wa Vijiji vya Koma na Kwale,  Wilayani Mkuranga mkoani Pwani, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vituo vya afya, hali inayosababisha kupoteza maisha na wanawake kujifungilia kwenye boti wakati wakifuata huduma hiyo Wilayani.

Wananchi hao walitoa malalamiko yao mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega,  juzi alipofanya ziara ya siku moja ya kutembelea visiwa hivyo  kuwashukuru wananchi kwa kumchangua kuwa mwakilishi wao pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.

Mmoja wa wanakijiji hao, Maimuna Nyakonda, alisema  kuwa wanawake wamekuwa wakipata madhara wakati wakisubiri usafiri wa boti kuwavusha na kuwapeleka Wilayani Mkuranga kwa matibabu lakini kwa bahati mbaya wamekuwa wakizalia njiani na wengine kuzalishwa na wakunga kutokana na hali ya hewa.

"Ukosefu wa zahanati katika Vijiji hivi ambavyo viko kisiwani, umesababisha sisi wanawake kudhalilika sana, tunajifungulia njiani huku mabaharia wakishuhudia pia wakati mwingine wenzetu wanapoteza maisha, hili jambo linatusononesha sana, " alisema Maimuna.

Naye Halima Said, mkazi wa kijiji cha Koma, alisema hali hiyo imesababisha wanawake wa visiwa hivyo kuendelea kutegemea huduma za wakunga ambao hawana ujuzi na kusababisha madhara kwa wanaojufungua.

"Huku tunatumia njia mbili tu kuhamia Wilayani wakati mimba inapofikia miezi nane au kama huna ndugu huko ubaki hapa, kama Mungu akisaidia kukawa na hali ya hewa nzuri bahari haijachafuka,  unaweza kufika Wilayani salama,” alisema.
Alisema kama ikishindikana wanalazimika kwenda kwa mkunga ambaye hata hivyo hawana ujuzi wa kumsafisha mama aliyejifungua vizuri.
Akizungumza tatizo hilo, Ulega alisema, tayari ameanza kujenga Zahanati katika kijiji cha Koma ambayo inatarajia kukamilika mwaka huu na katika kijiji cha Kwale ameagiza uongozi wa kijiji na halmashauri kuanzisha ujenzi ili aweze kuendeleza.

"Natambua shida mnazopata mama zangu, naahidi mwaka huu hautaisha bila zahanati hii kukamilika lakini pia naandaa utaratibu wa kujenga nyumba ya mganga,  kununua thamani zote za ndani ili mganga aje tu na nguo, awape huduma wananchi wangu wa Koma, "alisema Ulega. 
Alifafanua kuwa, katika kipindi chake cha miaka mitano ya uongozi anatarajia kujenga zahanati  na vituo vya afya 30 ili wananchi na wapate huduma ya afya iliyo bora.
 MWISHO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni