TANZANIA inakabiliwa na upungufu wa walimu wa elimu ya ufundi jambo ambalo linasababisha baadhi ya vyuo vya ufundi stadi kuajiri walimu wasiokuwa na sifa zinazohitajika katika fani hiyo.
Mpaka sasa kuna idadi ndogo ya vyuo vinavyofundisha ualimu wa ufundi stadi jambo linalosababisha kuwapo na walimu wasiokuwa na sifa katika vyuo vya elimu ya Ufundi.
Vyuo vya mafunzo ya Ufundi stadi ni nguzo pekee ya kulisaidia taifa kuingia katika uchumi wa viwanda mwaka 2020 huku nchi ikitegemea kuingia katika uchumi wa kati.
Hivi karibuni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(NACTE) kwa kushirikiana na Kituo cha elimu ya watu wazima Kouvola kutoka nchini Finland waliandaa mkutano wa Kimataifa ili kubadilishana uzoefu kati ya nchi hizi mbili.
Mkutano huo ulibeba ujumbe wa ‘wekeza katika elimu ya ufundi ili Tanzania iweze kuingia katika uchumi wa viwanda’ umehuhudhuliwa na taasisi za elimu ya ufundi, wamiliki wa viwanda, wadau na wataalamu 30, wa sekta hiyo kutoka nchini Finland.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Elimu nchini Finland Dk.Tuija Arola anaelezea nchi hiyo ilivyoweza kuwekeza katika mafunzo ya wakufunzi wa elimu ya ufundi.
Anasema kuna umuhimu wa nchi kuwa na walimu waliobobea katika elimu ya ufundi stadi ili kuweza kutoa wahitimu waliokuwa na sifa za kukidhi soko la ajira.
“Walimu wa mafunzo ya ufundi stadi wanatakiwa kuwa na mafunzo endelevu katika kipindi chote cha ualimu wao ili kwenda na mabadiliko ya kasi ya teknolojia,” anasema Dk. Arola.
Anasema walimu wanatakiwa kutembelea katika maeneo ya viwanda kupata ujuzi mpya unaohitajika katika wakati husika.
Anasema Tanzania inatakiwa kuwekeza katika kuwaandaa wakufunzi wa mafunzo ya ufundistadi ili kufanikisha malengo ya kuwa nchi ya viwanda.
Akitolea mfano katika nchi ya Finland Arola anasema taaluma ya ualimu na ukufunzi nchini humo inathaminika na kuheshimika jambo ambalo linawaongezea nguvu wakufunzi katika kutekeleza majukumu yao.
Anasema kwa kuwa mafunzo ya wanafunzi huhamishiwa katika maeneo ya kazi hivyo wakufunzi wana wajibu wa kuratibu ushirikiano na kampuni zenye kutoa ajira kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi.
“Mkufunzi ana nafasi kubwa katika kuwezesha juhudi za kujifunza kwa mtu mmoja mmoja ili kufikia malengo yake binafsi,” anasema Dk. Arola.
Anaongeza kuwa kutokana na hali hiyo wakufunzi wa mafunzo ya ufundi wanatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha juu katika fani zao.
Anasema wakufunzi wa elimu ya ufundi wanatakiwa kutumia mbinu mbadala katika kuongeza kiwango chao cha elimu na ujuzi.
Aidha anazitaka mamlaka husika katika kusimamia elimu ya ufundi kuwatengenezea mazingira ya kazi wakufunzi hao ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha ili waweze kutimiza majukumu yao kikamilifu.
“Mabadiliko ya utendaji kazi wa walimu unahitaji kujitolea zaidi hivyo watafanikiwa iwapo tu watapata ushiriki na kuungwa mkono na mamlaka ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kifedha,” anasema Dk.Arola.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako anasema serikali inawekeza katika kuwaandaa walimu wa elimu ya ufundi ili kuwa na wataalamu wataoiwezesha nchi katika kuingia katika nchi ya viwanda.
Anasema nchi haiwezi kuingia katika uchumin wa viwanda bila kuwekeza katika raslimali watu watakaofanya kazi katika viwanda hivyo.
“Tujitathmini kuinua ubora wa elimu ya ufundi kwa kuchukua uzoefu kutoka kwa wenzetu kutoka Finland kwa kuwa wenzetu wamefanikiwa katika elimu ya ufundi,” anasema Profesa Ndalichako.
Anasema changamoto iliyopo ni muunganiko wa ubunifu unaofanywa na taasisi za mafunzo ya ufundi na viwanda.
“Changamoto ni namna ya kuunganisha ubunifu unaotolewa na taasisi za mafunzo kuingizwa katika maisha ya kawaida ya watanzania,” anasema Ndalichako.
Profesa Ndalichako anasisitiza juu ya mafunzo ya walimu na wahitimu katika taasisi za juu ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Niwaombe tufanye kazi kwa kushirikiana taasisi za mafunzo na waajiri kuangalia namna ya kupunguza utengano uliopo kwa kuwa kila mmoja anamtegemea mwenzake,” anasema Ndalichako.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk.Adolf Rutayuga anasema Baraza hilo linahakikisha kuwa wahitimu wanaotolewa na vyuo vilivyosajiliwa wanakidhi vigezo vya ajira na mahitaji ya soko.
Anasema kwa kuwa katika mkutano huo walikuwapo pia watoa maamuzi akiwamo waziri Ndalichako hivyo yatafanyiwa kazi na kupata suluhisho mapema.
“Hapa tumekuwa na viongozi wakubwa na watoa maamuzi hivyo yote yaliyozungumziwa katika mkutano huu yatapatiwa ufumbuzi kulingana na mahitaji,” anasema Dk.Rutayuga.
Anasema hii ni hatua moja ya kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kuwa waliokutana hapa ni wadau wakubwa katika sekta hiyo.
“Yamejadiliwa mengi katika mkutano huu hii ni hatua moja mbele kuelekea Tanzania ya Viwanda kwa kuwa tunaunganisha nguvu kwa maana ya Watoa Mafunzo na waajiri ama wenye viwanda,” anasema Dk. Rutayuga