TAASISI ya Wakaguzi wa Ndani (IIA) Tanzania imeiomba serikali kufuata mwongozo wa kimataifa wa weledi wa ukaguzi wa ndani (International Professional Practice Framework) ili kuwawezesha kazi zao kutambulika kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa IIA Tanzania, Kafaso Millinga alisema kufuata mwongozo huo kutasaidia Wakaguzi wa Ndani kupata fursa za kufanya kazi hizo katika nchi mbalimbali.
"Tunaiomba serikali kuona umuhimu wa kuufuata mwongozo huu ambao utawasaidia wakaguzi wa ndani kutambulika kimataifa," alisema Millinga.
Alisema katika mwezi wa Mei ambao ni wa kujenga uelewa hivyo wameandaa mihadhara itakayofanyika katika vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ili kujenga uelewa wa jamii kuhusu fani hiyo.
"IIA imeandaa mihadhara itakayofanyika katika Chuo kikuu cha Ardhi (ARU), Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM).
"Lengo ni kuuelimisha umma umuhimu wa wakaguzi wa ndani ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi kwa ngazi zote za taifa," alisema Millinga.
alisema pamoja na kutembelea vyuo hivyo pia watakutana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwajengea uelewa juu ya fani hiyo.
Alitoa rai kwa jamii kujifunza na kufuatilia taarifa na ripoti mbalimbali zinazotolewa na Wakaguzi wa ndani ili waweze kupata taarifa sahihi.
"Fani ya ukaguzi wa ndani inahitaji uwajibikaji na uadilifu wa hali ya juu hivyo tunahitaji umma wa watanzania kutupa ushirikiano katika kutekeleza majukumu," alisema Millinga.
Mwisho