Alhamisi, 22 Machi 2018

kipindupindu burahati kwa heri


-DAR ES SALAAM
WAKAZI wa Kata ya Mburahati, Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam wataondokana na magonjwa ya mlipuko baada ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa uondoshaji maji taka katika kata hiyo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Mhandisi mradi kutoka Borda ambao ndio wajenzi, Modekai Sanga alisema mradi huo ukikamilika utawanufaisha wakazi 40,000 wa Mburahati na maeneo jirani.
Alisema wakazi hao watapata huduma ya uondoshaji wa majitaka kwa gharama nafuu na hivyo kuondokana na magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa mazingira hususani majitaka.
“Katika mradi huu kutapatikana nishati ya gesi ambacho ni lita 7,000 kwa siku, Mboji na maji ya kumwagilia bustani na miti,” alisema Sanga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alisema serikali inaendeleza juhudi za ujenzi wa miradi mbalimbali ya kuondosha majitaka kwa kushirikiana na wadau.
Alisema lengo la serikali ni kuwapatia wakazi wa jiji hilo huduma ya uondoshaji majitaka kwa asilimia 30 hadi kufikia mwaka 2020.
“Miradi hiyo ni uboreshaji na upanuzi wa mfumo wa maji taka kwa jiji la Dra es Salaam ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mitambo mitatu ya kisasa ya kusafishia maji katika maeneo ya Jangwani (mita za ujazo 200,000),” alisema Makori.
Aliongeza kuwa miradi mingine ni ule wa Kurasini ambao utakuwa na uwezo wa kuondosha majitaka  mita za ujazo 11,000 na wa Mbezi Beach (16,000).
Akizungumzia mradi wa uondoshaji maji Mburahati Makori alisema Ofisi ya Mkoa huo ilisaini makubaliano na shirika lisilo la Kiserikali la Borda la nchini Marekani kujenga mradi huo.
“Mapenda niwapongeze Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(Dawasa) kwa kushirikiana na Borda kutekeleza mradi huu ambao utawanufaisha wakazi wa Mburahati,” alisema Makori.
mwisho