WATAALAMU wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji wameshauriwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika kutekeleza miradi ya maji ili nchi kuangalia mikataba wanayoingia ili nchi inufaike na miradi hiyo.
Akizungumza katika ziara aliyoifanya jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso alisema wataalamu hao waangalie mikataba wanayoingia ili kuruhusu baadhi ya vifaa vya ujenzi kununuliwa nchini.
Alisema kwa sababu nchi hii kwa sasa ni ya viwanda hivyo ni vyema wanapoingia mikataba kuondoa vipengele vitakavyowafunga katika kununua baadhi ya vifaa.
"Si busara vifaa kama koki na pampu kununuliwa nje ya nchi wakati vinapatikana hapa nchini,” alisema Aweso.
Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mitaji katika viwanda vya ndani, ajira na kuongeza mzunguko wa fedha nchini.
"Pamoja na kuwa na nia njema ya kuwapatia wananchi maji safi na salama lakini pia waliangalie hili kwa manufaa ya nchi,” alisema Aweso.
Aidha aliongeza kuwa bado kuna changamoto ya kuwapo kwa makandarasi wasiokidhi vigezo ambao hutekeleza miradi chini ya kiwango.
“Bado tuna changamoto ya makandarasi wanaopewa miradi 'kiushemeji shemeji' jambo ambalo linasababisha kushindwa kuteteleza kwa kiwango hivyo kama wizara tutawatapisha fedha hizo na kuzirudisha katika miradi," alisema Aweso.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(Dawasa), Modester Mushi alisema wanatarajia kuwaunganishia maji wateja 376,000 katika visima vya Mpera na Kimbiji.
Mwisho